Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV
Rais wa Shirikisho la Kandanda nchini (TFF), Wallace Karia amefafanua kuwa fedha takriban Bilioni 1 za Kitanzania zilizotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli zilitumika katika maandalizi ya Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa vijana (AFCON U-17) zilizofanyika hapa nchini April, 2019.
Kupitia Kipindi cha Jaramba kinachorusha na Chaneli ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1), Rais Karia amethibitisha ni kweli walipewa fedha hizo na Rais Magufuli walipoitwa Ikulu baada timu ya wakubwa (Taifa Stars) kufuzu Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) yalifanyika June, 2019 nchini Misri.
"Kiukweli sisi (TFF) tulishirikiana na Serikali na kulikuwa na Kamati ya maandalizi ya Michuano hiyo ambayo ilikuwa chini ya Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe na unapokuwa mwenyeji wa Mashindano timu zote, Viongozi, Wageni wote unagharamia wewe kama mwenyeji", ameeleza Karia.
Kupitia mahojiano hayo, Rais Karia amedai kuwa Fedha hizo zilienda Baraza la Michezo nchini, amedai TFF haikupokea fedha hizo licha ya kuwepo tuhuma kwa Shirikisho hilo kutumia vibaya fedha hizo. "Fedha hazikuja TFF, bali zilitumika kwenye Maandalizi ya Michuano ile ya AFCON kwa vijana (U-17)", amedai Karia.
Karia ameeleza kuwa Shrikisho hilo Soka nchini linaamini kuhusu fedha hizo kila kitu kitawekwa wazi na Mamlaka zinazohusika kwa madai ya upotevu wa fedha hizo, amedai Kamati ya Maandalizi ya Michuano, TFF na Baraza la Michezo walisimamia maandalizi ya Michuano hiyo kiufanisi.
Karia amebainisha kuwa Tanzania iliomba kuandaa Michuano hiyo tangu mwaka 2015 wakati Serikali ya awamu ya Tano inaingia madarakani chini Rais wake, Dkt. John Magufuli, amesema baada ya maandalizi hayo Tanzania imeandika historia baada yakupata nafasi adimu yakuandaa Michuano hiyo ambayo inakuwa nadra kwa Mataifa mengi barani Afrika.
"Mimi binafsi nimefurahi suala hili kufika katika Mamlaka husika ili kubaini kila kitu kuhusu fedha hizo, suala hili limenifanya niwe huru hapa lilipofika, sisi tulifarijika na Maandalizi ya Mashindano yale, tulikuwa hatulali kuhakikisha mashindano yanafanyika", ameeleza Karia.
Hata hivyo, Karia amemshukuru Rais Magufuli kusimamia mashindano hayo, amesema Wageni waliofika kushuhudia walishukuru na kupongeza maandalizi kwa ujumla. Amedai mashindano hayo yaliyofanyika hapa nchini yalikuwa bora zaidi yaliyofanyika nyuma.
Rais wa Shirikisho la Kandanda nchini (TFF), Wallace Karia
Post a Comment