Makamu Rais wa kwanza wa Sudani Kusini Riek Machar na mke wake Angelina Teny wamethibitishwa kuambukizwa virusi vya corona.
Dkt. Machar alisema kwamba yeye na mke wake ambaye pia ni waziri wa ulinzi, wamepata maambukizi baada ya kutangamana na jopo la ngazi ya juu la kukabiliana na virusi hivyo nchini humo.
Machar amesema kwamba hana dalili zozote na hali yake ya afya iko sawa lakini atajiweka karantini kwa siku 14.
Wengine waliothibitishwa kuambukizwa ni walinzi kadhaa na wafanyakazi.
Mpaka sasa Sudan Kusini imerekodi waathirika 236 na vifo vinne.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisi yake: "Bado tunasubiri matokeo mengi na ni matumaini yetu kwamba kesho, tutakuwa na orodha kamili ya walioambukizwa katika jopo hili," Machar amezungumza hayo katika mkutano na wanahabari uliofanyika Jumatatu mjini Juba...Huenda daktari akatutembelea hadi atakapotuarifu kwamba wakati umewadia wa kumaliza karantini''.
Wiki jana maafisa walitangaza kwamba virusi hivyo vimefikia kwenye kambi ya waliotoroka makazi yao ambao wamekuwa wakiitaka Umoja wa Mataifa iwalinde katika mji mkuu wa Juba tangu 2013.
Nchi hiyo bado inakabiliana na baa la njaa hata baada ya Machar na Rais Salva Kiir — waliokuwa mahasimu kuunda serikali ya umoja wa taifa Februari.
Viongozi hao wawili bado hawajakubaliana masuala ya msingi kama udhibiti wa majimbo.
Uganda kugawa barakoa bure
Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema kuwa serikali itasambaza barakoa bure kwa raia wote wa Uganda walio na umri wa miaka sita na zaidi.
Kuvaa barakoa mtu anapokuwa sehemu za umma ilitangazwa mwezi Mei kuwa ni jambo la lazima .
Wakati akihutubia taifa tarehe 14 siku ya Jumatatu kuhusu mwenendo wa virusi vya Covid -19 nchini humo, Museveni pia alitangaza hatua za kupunguza makali ya amri ya kutotoka nje, ambayo itaanza kutekelezwa baada tu ya barakoa kusambazwa kwa watu.
Rais amesema usambazaji wa barakoa utafanyika kwa siku 14.
Maduka madogo nje ya maduka makubwa pia yataruhusiwa kufunguliwa, magari yanayotoa usafiri kwa Umma yatatoa huduma kwa kubeba abiria nusu ya uwezo wa magari yao, na wafanyabiashara wa vyakula nao wataruhusiwa kurejea majumbani mwao baada ya siku kuisha.
Hata hivyo, usafiri wa Umma bado umepigwa marufuku katika wilaya zilizo mipakani kwa siku 21.
Shule- kuanzia za msingi mpaka vyuo vikuu zitaruhusiwa kufunguliwa kwa wale wanaotarajiwa kumaliza masomo pekee, ili kujiandaa na mitihani yao ya kumaliza mwaka.
Hatua nyingine zote, kama kufungwa kwa mipaka ya kuingia nchi za kigeni, muda wa kurejea majumbnani, na kuzuiwa kwa mikusanyiko ya watu imeendelea kupigwa marufuku kwa siku 21 pia.
Tayari nchi ya Uganda imetekeleza amri ya kutotoka nje kwa siku 48.
Uganda imethibitisha kuwa na wagonjwa 248 wa virusi vya corona , wengi wao madereva wa malori ambao huvuka mpaka kuingia nchi jirani.
Post a Comment