Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amesema kwamba mwanawe aliambukizwa virusi vya corona lakini akapona baada ya kujitenga,kunywa malimao na kujifukiza.
Rais Magufuli amezungumza wakati akitoa salamu kwa watanzania aliposhiriki ibada ya Jumapili katika kanisa la kilutheri Usharika wa Chato mkoani Geita.
''Mtoto wangu alipata corona....mtoto wa kuzaa mimi , alijifungia kwenye chumba huko akaanza kujifukiza akanywa malimao na tangawizi, amepona yuko mzima anapiga push ups'' Alieleza.
Rais Magufuli amesema kwamba nchi ya Tanzania itafanya inachojua lakini haitakubali kushurutishwa kuchukua hatua na watu wa nje.
Kiongozi huyo amesema kwamba serikali yake haitaweka amri ya kutotoka nje kama inavyofanywa na mataifa mengine na kwamba Mwenyezi Mungu atasaidia katika kulikabili janga la corona.
Amesema kwamba wale wanaowawekea raia wao masharti ya kutotoka nje waendelee kufanya hivyo na kwamba serikali yake itawasaidia na chakula watakapomaliza .Amesema kwamba serikali yake na Jumuiya ya Afrika Mashariki pamoja na ile ya SADC zitaendelea kushirikiana.
''Na ndio maana ndugu zangu sikufunga mipaka niliheshimu majirani zangu, tumezungukwa na karibu nchi nane, ukizifungia maana yake umezinyima uchumi wao kuna baadhi ya nchi wanategemea vyakula vya Tanzania''.
Ameiambia wizara ya afya na madaktari kuwa mtu yeyote atakayefariki kwa ugonjwa wowote hata kama ni corona ni vyema aheshimiwe kwa maziko ya kawaida kwa heshima ya binaadamu.
''Kuna mambo ya hovyo yanafanyika, kila Mtu akifariki wanakimbilia kumpima corona, Mtu amefariki unampima ya nini?, nguvu za kumpima wanazo, za kumuhudumia akapona hawana, Mtu atakapofariki kwa ugonjwa wowote hata wa corona lazima azikwe kwa kawaida, corona sio Ebola" . Alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli amesema kuwa wagonjwa wa corona wamepungua nchini Tanzania kwa kiasi kikubwa.
Akieleza idadi ya wagonjwa waliopona na kuruhusiwa katika hospitali na vituo mbalimbali nchini Tanzania, Rais Magufuli amesema Mungu 'amejibu maombi' na kusisitiza kuwa tahadhari ziendelee kuchukuliwa.
Amesema kuwa ikiwa mambo yataendelea 'hivi hivi' kuanzia wiki ijayo, amepanga kufungua vyuo ili wanafunzi waendelee na masomo na michezo iendelee.
Post a Comment