Rais wa Marekani Donald Trump amesema kwamba anakunywa dawa ya hydroxychloroquine kujikinga dhidi ya virusi vya corona hata ingawa maafisa wa afya wametoa onyo juu ya usalama wa dawa hiyo.
Akizungumza katika Ikulu ya White House, aliwaambia wanahabari kwamba ameanza kunywa dawa hizo zinazotibu ugonjwa wa malaria na hivi karibuni imetumika kutibu ugonjwa wa ngozi.
"Nimekuwa nikiinywa kwa karibia wiki moja na nusu sasa na niko hapa, bado niko hapa," hilo lilikuwa tangazo lake la kushangaza.
Hakuna ushahidi unaoonesha kwamba dawa ya hydroxychloroquine ina uwezo wa kukabilina na virusi vya corona na wataalamu wanaonya kuwa inaweza kusababisha matatizo ya moyo.
Trump amesema nini?
Rais huyo, mwenye miaka 73, alikuwa ameitisha mkutano kwa ajili ya kuzungumzia sekta ya migahawa Jumatatu, aliposhutukiza wanahabari kwa kuwafahamisha kwamba amekuwa akinywa dawa hiyo.
"Utashangaa ni watu wangapi wanaokunywa dawa hii, hasa wafanyakazi waliomstari wa mbele katika kukabiliana na janga la virusi vya corona kabla ya wewe kuipata, wahudumu wa afya, wengi wao tu wanakunywa dawa hii," aliwaambia wanahabari. "Mimi pia ninainywa."
Alipoulizwa kuhusu faida za kunywa dawa ya hydroxychloroquine, Bwana Trump alisema: "Ushahidi wangu ndio huu: Napigiwa simu nyingi sana zinazosifu dawa hii."
Aliongeza: "Nimesikia mengi mazuri kuhusu dawa hii ya hydroxychloroquine na ikiwa siyo nzuri, nawaarifu kwamba sitadhurika."
Ingawa kuna baadhi ya watu waliothibitishwa kupata maambukizi ya virusi vya corona, rais alisema tena Jumatatu kwamba hana dalili zozote na huwa anapimwa kila wakati.
- Coronavirus: Kwa nini ni hatari kugusa uso wako
- Jinsi ya kuzuia maambukizi ya virusi vya Corona
- Majibu ya maswali 10 yanayoulizwa sana kuhusu coronavirus
- Je unaweza kupata coronavirus mara mbili?
Pia aliongeza kwamba amekuwa akinywa dawa mbadala ya madini ya zinc na pia alikunywa dawa ya azithromycin, ambayo matumizi yake ni kuzuia maambukizi na kuua bakteria mwilini.
Alipoulizwa ikiwa daktari wa Ikulu amependeeza yeye kuanza kunywa dawa hiyo ambayo bado inazua utata katika matumizi yake dhidi ya virusi vya corona, Bwana Trump alisema yeye mwenyewe ndiye aliyeomba kupewa dawa hiyo.
Dkt. Sean Conley, daktari wa rais, alisema katika taarifa iliyotolewa na Ikulu Jumatatu baadae kwamba Bwana Trump alikuwa katika hali nzuri kiafya na hana dalili zozote za virusi vya corona.
Afisa wa jeshi la wanamaji Marekani aliongeza:"Baada ya mazungumzo ya mara kadhaa yeye na mimi tulikuwa na maoni ya kuunga mkono na kupinga vilevile matumizi ya dawa hydroxychloroquine, tulihitimisha kwa kuangalia faida zilizopo kwa kunywa dawa hiyo na kuona kwamba zinazidi ile hatari iliyopo."
Maafisa wa afya Marekani wanasema nini?
"Shirika la Usimamizi wa Chakula na Dawa la Marekani mwezi uliopita lilitoa ushauri na kusema dawa ya hydroxychloroquine haijathibitishwa kuwa salama wala yenye ufanisi".
Pia shirika hilo lilionesha kwamba dawa hiyo inaweza kusababisha matatizo makubwa ya ugonjwa wa moyo kwa wagonjwa wa Covid-19.
Aidha shirika hilo lilionya dhidi ya matumizi ya dawa hiyo kwa wale ambao hawako hospitali, ambako limetoa idhini ya muda tu ya matumizi kwa baadhi ya wagonjwa.
Kituo cha Kudhibiti magonjwa Marekani kimesema kuwa hakuna dawa iliyoidhinishwa au tiba ya aina yoyote ile kwa ajili ya kuzuia au kutibu ugonjwa wa Covid-19 ambao umethibitishwa kuambukiza zaidi ya watu milioni 1.5 nchini Marekani, huku wengine 90,000 wakiaga dunia.
Utetezi wa Trump ni upi?
Akitupilia mbali taarifa za kuwa dawa hiyo ya hydroxychloroquine ina atahri zake, rais alisema: "Kile ninachoweza kuwaambia ni kwamba, hadi kufikia sasa nahisi niko sawa."
Alisema kuwa taarifa hasa pekee alizokuwa amezisikia hazikuwa za kisayansi zinazoendeshwa na watu ambao sio mashabiki wa Trump.
Bwana Trump alikuwa akizungumzia utafiti wa bunge kutoka Aprili kuhusu wagonjwa wa Covid-19 katika hospitali za wanajeshi zinazoendeshwa na serikali ya Marekani zilizopendekeza kwamba dawa ya hydroxychloroquine haikuwa na faida yoyote na huenda hata ikasababisha kiwango kikubwa cha vifo.
"Ninapata taarifa nyingi tu kuhusu dawa ya hydroxy," rais amewaambia wanahabari, na kuongeza: "kwani utapoteza nini kwa kunywa dawa hii?"
Kulingana na madaktari, dawa hiyo ina uwezo wa kusababisha dalili zengine ikiwa ni pamoja na ugonjwa wa moyo, kuanza kufikiria kuhusu kujiua na ishara za ugonjwa wa maini.
Post a Comment