Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametuma ujumbe katika mtandao wa Twitter akiashiria mauaji ya kusikitisha yaliyofanywa na polisi ya Marekani dhidi ya Mmarekani mweusi ambaye hakuwa na silaha ya aina yoyote katika mji wa Minneapolis na kusema: Umewadia wakati wa dunia kuungana kwa ajili ya kukabiliana na ubaguzi wa rangi.
Muhammad Javad Zarif ameashiria jinsi maisha ya Wamarekani weusi yanavyopuuzwa nchini Marekani na kuandika kuwa, kwa muda mrefu sasa suala la kupambana na ubaguzi wa rangi limewekwa kando na kubakia nyuma. Amesema umefika wakati wa dunia kusimama na kupambana na ubaguzi.
Miji mbalimbali ya Marekani imekumbwa na wimbi la maandamano na machafuko makubwa yaliyochochewa na mauaji yaliyofanywa na polisi katika mji wa Minneapolis dhidi ya raia mwenye asili ya Afrika, George Floyd.
Ripoti zinasema mtu mmoja ameuawa huko Detroit, Michigan, baada ya mtu asiyejulikana kuwafyatulia risasi waandamanaji wanaopinga mauaji ya George Floyd.
Mauaji ya mwandamanaji huyo aliyekuwa na umri wa miaka 19 yametokea baada ya Rais Donald Trump wa Marekani kuchochea hisia za raia hao kwa kuwakosoa wale wanaopinga ukatili wa polisi ya nchi hiyo dhidi ya Wamarekani weusi.
Baadhi ya waandamanaji wameonekana wakichoma moto bendera za Marekani na kutoa nara zinazosema kama hakuna uadilifu hakutakuwepo amani.
Post a Comment