Featured

    Featured Posts

HOJA MTAMBUKA: MEMBE ACHANA NA NDOTO KUBALI YAISHE, MUDA SI RAFIKI KWAKO TENA NA HUNA UBAVU WA KUMNYANYUA DK. MAGUFILI KWENYE KITI CHA URAIS

KUNA nyakati lazima ukubali kushindwa na kuendelea na mambo mengine. Ndicho anachotakiwa kukifanya aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernad Membe hasa kutokana na namna anavyozicheza siasa zake mara kwa mara.

Kwa uwezo na maarifa ya Membe kwa taifa alipaswa kuwa mstari wa mbele kueneza mambo mazuri yanayofanywa na serikali na si kuwa sehemu ya kuanzisha taharuki zisizokuwa na mantiki kwa taifa na hasa sisi vijana, ambao tunaamini wao ndio wakutuongoza vyema na si wa kutuvuruga.


Kusambaa kwa clip ya video ikimuonyesha Membe akizungumza na baadhi ya wananchi mkoani Lindi, jimboni Mtama na kuzungumzia masuala ya uchaguzi, urais na nafasi yake ya kisiasa ni wakati wa yeye kujipima zaidi na hata kutafakari matokeo ya maneno yake kabla hajayatoa kwa umma.


Lazima tufike mahali tutenganisha chuki binafsi. Chuki binafsi ni ile ambayo unakuwa nayo na kuamini mtu fulani hafahi na anayestahili ni mimi na hakuna mwingine. Huu ni uchawi usiokuwa na sababu za msingi ambazo jamii inayoishi kwa amani na upendo inapaswa kuwa pamoja na si kufarakana pasipokuwa na sababu zozote.


Mtu mwenye kariba ya Membe anapojitokeza hadharani na kuzungumzia uhuru wa tume, mtu mwenye akili timamu lazima anajua kuna kitu ambacho kipo nyuma ya pazia, ambapo watanzania hawataki kukiona au kukifanya maana wanataka kuishi kwa amani na upendo na uchaguzi ni mchakato unaopita na maisha lazima yaendelee.


Ni jambo la kushangaza leo ndio tunaonekana watu wa kutaka mchakato huru wa uchaguzi lakini kwa miaka zaidi ya 30 walipokuwa kwenye madaraka hawakuwi kusema chochote au kueleza hayo maoni yao wanayoyaita kuwa ni sahihi kuyatoa kama sasa wanavyodai.


Membe anapaswa kukubali na kwenda na wakati kuwa huu wakati sio wake tena na Rais Dk. John Magufuli ndio rais wetu na hakuna mwingine, anapoendelea kuzungumza mambo yenye ukakasi ni kuendelea kujishushia heshima yake, ambapo ukimtazama kwa usoni unaona kabisa ni chuki binafsi aliyokuwa nayo.


Urais sio pipi kwamba kila mtu anaouwezo wa kuipata na kuila, Urais ni baraka kutoka kwa MwenyeziMungu na ndio maana Rais anakuwa mmoja tu kwa nchi nzima. Anapaswa kusadiki kuwa ndoto za Urais alizokuwa nao zimepitwa na wakati na sasa aungane na watanzania wengine kufanya kazi kwa bidii kuunga mkono falsafa za HapaKazi Tu.


Hii inatokana na sasa si wakati tena wa kutengeneza matabaka au makundi ya kumsapoti juu ya ndoto ya Urais aliyokuwa nayo, kwa kuwa kiutaratibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais kwa upande wa bara ni Dk. John Magufuli na sio mwingine yeyote na anachopaswa kukifanya ni kutulia na kuganga yajayo hasa kwa mtu kama yeye aliyewahi kushika nafasi kubwa serikalini na zenye maamuzi.


Membe anapaswa kuachana na tamaa ambazo hazina mantiki kwa jamii na zaidi zinazidi kumshushua heshima yake kwa kuwa anapigana vita ambayo yeye mwenyewe akikaa anaona kabisa kuwa hawezi kushinda na zaidi anachofanya ni kutaka kuwaharibia watu wanaomzunguka na kuonekana kama wako naye pamoja wakati sio kweli.


Ninaamini na ninajua kuwa Membe mwenyewe anafahamu kuwa hana nguvu ya kumshinda Rais kwenye sanduku la kura iwe ndani ya CCM kama anavyotaka au nje ya CCM. Hivi mambo makubwa aliyoyafanya Rais Dk. Magufuli kwa awamu ya kwanza ya miaka mitano hadi sasa, yeye binafsi angeweza?. Dk. Magufuli amekuwa mtu wa mageuzi makubwa kwa taifa hasa kuliondosha taifa kutoka kwenye umaskini wa kutengenezwa.


Njia anazopita Rais Dk. Magufuli kujenga uchumi ndio njia sahihi ambazo mataifa makubwa tunayoyaona ya mfano kwenye uchumi na kwenye vitabu imeandikwa ikiwemo Korea Kusini, Malaysia na nyinginezo kujenga uchumi imara wa nchi zao ndio wamefanya na sasa Tanzania inakwenda huko.


Natambua na tunajua mfumo wa utawala anaokwenda nao Rais Dk. Magufuli kwa watanzania umemuumiza yeye binafsi Membe au washikaji zake. Asijenge chuki binasi na kutaka kila chuki yake na mtu mwingine airithi bila sababu za msingi hasa ikizingatiwa nchi ina watu zaidi ya milioni 55, ambao nao wanapaswa kupewa kipaumbele na sio wao.


Kuna mambo yanayopaswa jamii ielewe tume huru ya uchaguzi anayoilalamikia leo Membe inatokana na yeye kukosa fursa tu na sio vinginevyo, hivi kwa mfano akiteuliwa na rais Dk. Magufuli kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa au Balozi ataitisha kikao Mtama na kudai tume huru?.


Tusiwageuze wananchi waliokuwa masikini kuwa mazuzu na kutaka kuwarisisha chuki binafsi. Membe anapaswa kuamini na kama anaota basi atambue kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Dk. John Magufuli na atakuwa rais hadi ifikapo mwaka 2025 muda wake uliowekwa kikatiba kumalizika na anachotakiwa kukifanya kwa sasa ni kukiomba msamaha CCM tu.


Hivi tuwe wakweli mafanikio yaliopo sasa kuanzia ujenzi wa miradi mikubwa ya kimaendeleo, elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari, utoaji wa mikopo elimu ya juu na ufufuaji wa miradi mingi mikubwa kufanyika ndani ya miaka mitano. Haya ni mambo yaliyopaswa kumfanya Membe kutoka kwa umma na kumwambia Rais Dk. Magufuli Akhsante na sio kuongozwa na chuki.


Kuna wakati kweli lazima jamii ielezwe ukweli na wala isidanganywe, hivi kweli UACHE kumchagua Rais Dk. Magufuli kwa kumpa kura ya NDIYO, mtu ambaye katika kipindi chake cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, mapato ya ndani yameongezeka kufikia shilingi trilioni 18.5 mwaka 2018/19 kutoka shilingi trilioni 11.0 mwaka 2014/15, sawa na ongezeko la asilimia 69.1. Huo utakuwa ni uzwazwa na upimbi.


Ni wazi kwamba ongezeko hilo limesaidia utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati pamoja na uboreshaji wa miundombinu mingine inayosaidia kuongeza mapato zaidi au tumkatae Rais Dk. Magufuli ambaye ameboresha mifumo ya kieletroniki ya ukusanyaji wa mapato ili kuweka ufanisi mkubwa wa ukusanyaji mapato.


Unapozungumzia uchumi wa kati lazima uwe umetoka kwenye mifumo ya kianalogia katika utendaji na kuhamia katika mifumo ya kidigitali ili kuongeza kasi ya utendaji na kupata matokeo chanya kwa haraka, ambapo sasa Rais Dk. Magufuli ameweza kutekeleza hilo kwa umakini mkubwa kwa kuongozwa na utashi wake binafsi na si vinginevyo.


Mafanikio yaliopo sasa katika Sera za Mapato na Matumizi za Serikali ya Awamu ya tano zimelenga kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani na kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma. Katika kutekeleza sera hizo, Serikali imejenga na kuimarisha mifumo mbalimbali ikiwemo mfumo wa Serikali wa Kielektroniki wa Ukusanyaji wa Mapato (Government e-Payment Gateway System-GePGs), Mfumo wa Usimamizi wa Utoaji wa Risiti za Kielektroniki za Kodi (Electronic Fiscal Device Management System-EFDMS), Mfumo Jumuishi wa Forodha (Tanzania Customs Intergrated System-TANCIS), Mfumo wa Ulipaji Serikalini (MUSE). Haya ni mafanikio makubwa.


Mingine ni Mfumo wa Usimamizi wa Mali za Serikali (Government Assets Management Information System-GAMIS), Mfumo wa Serikali wa Malipo ya Mishahara (Government Salary Payment Platform-GSPP), Mfumo wa Ununuzi Serikalini (Tanzanian National e-Procurement System-TANePS) na Mfumo wa Akaunti Jumuifu ya Hazina (Treasury Single Account-TSA), ambapo sasa kila kitu kinajulikana na serikali.


Uboreshwaji wa huduma za jamii, ambapo siku zote unapozungumzia ukuaji wa uchumi lazima ufungamane na maendeleo ya watu na ili kutimiza azma hiyo Serikali ya awamu ya tano imechukua hatua madhubuti katika kuboresha upatikanaji wa huduma za jamii kwa wananchi zikiwemo afya, elimu na maji katika maeneo ya mijini na vijijini ambapo sasa kuna vituo lukuki vya afya kuanzia vijijini hadi mijini.


Serikali ya awamu ya tano kwa kipindi cha miaka mitano imeboresha miundombinu ya afya kwa kujenga zahanati 1,198, vituo vya afya 487, hospitali za Halmashauri za Wilaya 71, hospitali za rufaa za Mikoa 10 na hospitali za rufaa za kanda tatu (3). Pia imeongeza bajeti ya dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kutoka shilingi bilioni 31 mwaka 2015 hadi bilioni 269 mwaka 2019.


Kutokana na kuongezeka kwa bajeti ya dawa upatikanaji wa dawa muhimu katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini umefikia asilimia 94.4 mwaka 2019/20 kutoka asilimia 36 mwaka 2014/15, huku upatikanaji wa Maji safi na salama umekuwa mkubwa kwenye kipindi hiki cha miaka mitano ya utawala wa awamu ya tano na hata kuwa na maendeleo makubwa.


Katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano, kiwango cha upatikanaji wa maji vijijini kimeongezeka kufikia asilimia 70.1 na mijini asilimia 84. Aidha, Serikali imejenga na kukarabati miundombinu ya maji 1,423 ambapo miradi 1,268 ni ya vijijini na 155 ni ya  mijini, hivi kweli tuache kumpongeza Rais Dk. Magufuli na tuanze kumkebehi huku tumsifie Membe kuwa shujaa. Hilo haliwezekani na halitatokea kamwe kaa atambue.


Katika kipindi cha serikali ya awamua ya tano ndiyo serikali imeanza kutoa elimu biala malipo baada ya huduma hiyo kusitishwa miaka mingi iliyopita. Jumla ya Sh trilioni 1.01 zimetumika kwa kipindi hicho kugharamia elimu hiyo kuanzia darasa la awali hadi kidato cha tano. Mbali na hilo serikali imeboresha miundombinu ya kufundishia ikiwemo kuongeza madarasa, maabara, nyumba za walimu, vifaa vya maabara na madawati.


Uchumi wa kati utafikiwa tu ifikapo 2025 na mkombozi wa hayo yote atakuwa rais Dk. Magufuli kwa kuwepo kwake na kutoa usimamizi madhubuti mizuri ya usafirishaji hivyo ndani ya miaka mitano Serikali inaendelea na ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zikiwemo barabara kuu, barabara za mikoa na za wilaya ambapo kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2015 hadi Aprili 2020, ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami zenye urefu wa km 2,624.27 umekamilika; ujenzi wa daraja la juu la Mfugale (Dar es Salaam) na daraja la Magufuli (mto Kilombero) umekamilika.


Pia ujenzi  wa  barabara  kuu  kwa  kiwango  cha  lami zenye urefu wa km 1,298.44 unaendelea; ujenzi wa barabara ya pete (Ubungo interchange) umefikia asilimia  77;  ujenzi  wa  barabara  ya  njia  nane kutoka  Kimara  hadi  Kibaha  (km  19.2)  umefikia asilimia 80. Tumuache mtu aliyefanya haya ambaye ni Rais Dk. Magufuli na serikali yake na kumfuata Membe eti kwa vile handsome boy! Thubutu yake.  


Nchi inafanya ujenzi wa miradi mikubwa kama ujenzi unaoendelea wa daraja la New Selander (Dar es Salaam) lenye urefu wa km  1.03  pamoja  na  barabara  unganishi  zenye urefu wa km 5.2 na umefikia asilimia 38.2, daraja la Kigongo hadi Busisi (Mwanza) lenye urefu wa km 3.2, daraja jipya mto Wami katika barabara ya Chalinze hadi Segera litakalokuwa na urefu wa m 513.5 pamoja na barabara unganishi zenye urefu wa  km  4.3  umefikia  asilimia  39  na  daraja  la Ruhuhu (Ruvuma) umefikia asilimia 86. 


Miradi ya ujenzi wa  barabara,  madaraja   na   vivuko imegharimu jumla ya shilingi trilioni 7.63 kati ya mwaka 2015/16 hadi Aprili 2020, ambazo zote zinafanyika kwa usimamizi madhubuti wa Urais wake, ambao umekuwa na faida kubwa kwa taifa lenye watu milioni 55 na sio watu wachache kama Membe anavyotaka ili mradi yeye ana chuki basi kila mtu amfuate na kumsikiliza yeye.


Rais Dk. Magufuli ameendelea na kuikuza sekta ya uchukuzi ikiwemo ujenzi wa meli mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo katika Ziwa Victoria na ujenzi wa chelezo; ukarabati wa meli ya MV Victoria na MV Butiama ambapo katika kipindi cha mwaka 2015/16 hadi Aprili, 2020  ni mafanikio makubwa kuelekea uchumi wa kati, ambao Rais ameweza na hakuna wa kumzidi kwa uchaguzi mkuu wa 2020 au kuendelea ambao Membe anataka kuwaondoa watu kwenye taswira.


Vile vile, ujenzi wa meli moja mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 200 za mizigo katika Ziwa Nyasa; ujenzi wa vivuko vya MV Kigamboni, MV Utete, kivuko cha Kigongo – Busisi, kivuko cha MV Sengerema, kivuko cha Nyamisati kwenda Mafia; na ukarabati wa meli ya mafuta ya MT Sangara katika Ziwa Tanganyika yatachagiza kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi wetu.


Kuanza ujenzi wa mradi wa kihistoria wa Reli ya Kati kwa Kiwango cha Kimataifa (Standard Gauge Railway) kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro (km 300) na kipande cha Morogoro hadi Makutupora (km 422) ni hatua muhimu kufikia uchumi wa kati, ambao Membe na kundi lake hawataki kuona na badala yake yeye anataka kutuaminisha kwenye mahitaji yake binafsi na sio mahitaji ya wengi.


Rais Dk. Magufuli ni mkombozi wetu, amekuwa nasi kwenye kutotoa kwenye shinda na ndio maana sambamba na uejnzi wa reli mpya, ufufuaji wa reli ya zamani, ambazo zota anazifanya ni mchakato muhimu kusaidia usafirishaji wa mizigo ya viwandani na mashambani, ambapo kupitia mawazo na fikra zake anatekeleza bila kuyumbishwa na mtu yeyote.


Uimarishaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kwa kununua ndege mpya 11 ni hatua muhimu kufikia uchumi wa kati kwani itaongeza ushindani wa usafiri wa anga ambao ni wa haraka na uhakika zaidi na utakuza utalii kwa kiasi kikubwa, ambapo Membe yeye hataki na yuko kwenye kuwaza Urais tu na anachopaswa kuelezwa huu ni mwaka 2020 na rais aliyeko ni John Pombe Joseph Magufuli na atakuwepo hadi 2025.


Pia, ujenzi wa mradi wa kihistoria wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (MW 2,115) katika mto Rufiji ambao hadi sasa umegharimu kiasi cha shilingi trilioni 1.42 ni jambo la msingi sana katika kuinua uchumi kwani unakwenda kuleta nishati na uhakika na kuvutia wawekezaji na uzalishaji mali, ambao toka 2015 Rais Dk. Magufuli alishasema kuwa ndoto yake ni kuiona nchi inakuwa ya viwanda.


Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Dk. Magufuli na wasaidizi wake, akiwemo Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa imeendelea kutekeleza Mpango Kazi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji nchini (The Government Roadmap for Improvement of Business and Investment Climate) na Mpango wa Kuboresha Mfumo wa Udhibiti wa Biashara (Blue Print for regulatory Reform to Improve Business Environment).


Mipango hiyo ina lengo la kuhakikisha vikwazo na kero mbalimbali za biashara na uwekezaji zinaondolewa ili kuvutia uwekezaji zaidi nchini. Rais Dk. Magufuli wewe chapa kazi achana na kina Membe, sisi mtaani tuna msemo wetu 'Mlevi anayetafuta kufa, humchokoza kila mtu', hivyo Membe ameshajifia kisiasa na anatafuta wa kumpa lawama. JPM Songa mbele 2020 mali yako Baba.
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana