Spika wa Bunge la Marekani maarufu kama ‘Congress’, Nancy Pelosi amemlima barua nzito Rais Donald Trump kwa kutaka atoe maelezo kuhusu ongezeko kubwa la matumizi ya majeshi dhidi ya raia wanaoandamana kwa uhuru ndani ya nchi hiyo.
Katika barua hiyo ambayo iliandikwa tarehe 4 Juni, Spika Pelosi amesema kuwa wameshuhudia wanajeshi kwenye ngazi za Lincoln Memorial na sehemu nyingine za jiji la Washington, yalipo makao makuu ya taifa hilo.
==>>Tafsiri ya barua ya Spika Nancy Pelosi kwa Donald Trump ni kama ifuatayo;
Mpendwa Mheshimiwa Rais,
Nchini kote, Wamarekani wanaandamana kwa amani kudai kikomo cha muendelezo wa ukandamizaji wa haki kwa misingi ya rangi ya ngozi na ukatili wa polisi ambao umeua wamarekani wasio na hatia, kama tulivyoona hivi karibuni kwenye mauaji ya George Floyd.
Inashtusha kuwa katika makao makuu ya taifa letu, maelfu ya watu ambao wametoka kuandamana kwa amani wamekumbana na maofisa usalama kutoka vitengo mbalimbali vya usalama, wakiwamo maofisa usalama ambao hawajulikani wanatoka idara gani ya usalama.
Tumewaona wanajeshi katika ngazi za Lincoln Memorial. Tumeshuhudia maofisa wa Idara ya Magereza wakiwa Lafayette Square. Tumewaona maofisa wa Hifadhi za Wanyamapori wakiwatimua waandamanaji wa amani. Majimbo kadhaa yameleta maofisa wao wa jeshi la akiba hapa Washington. Hii ikiwa ni nyongeza kwa maofisa wengine wakiwamo wa FBI ambao wanafanya shughuli zao katika makao makuu ya taifa letu.
Tunapata shaka na ongezeko la matumizi ya majeshi na kukosekana kwa uwazi kunakoweza kupelekea machafuko. Ninakuandikia kuomba orodha kamili ya idara zote zinazohusika na maelezo ya majukumu na wajibu wa majeshi na rasilimali nyingine za taifa zinazotumika kwenye mji wa Washington. Bunge na Wamarekani wanahitaji kufahamu ni nani anayeongoza shughuli hizo, upi mnyororo wa amri, misheni ni nini, na kwa mamkala yapi haswa majeshi ya akiba kutoka katika majimbo mengine yanafanya shughuli zake kwenye makao makuu.
Kufanya hali kuwa mbaya zaidi, baadhi ya maofisa wamekataa kujitambulisha na wamewekwa kazini bila kuwa na alama za utambulisho, baji na majina. Kitendo cha maofisa kufanya kazi bila kuwa na utambulisho kinaondoa uwajibikaji, inaongeza kutoaminika kwa serikali na shaka na kunapingana na kanuni ya utaratibu wa kihaki na uhalali wakati huu wa tahadhari katika historia ya taifa letu.
Hata Idara ya Haki ilishawahi kusema kuwa kuruhusu maofisa kutekeleza majukumu yao bila utambulisho kutajenga ‘’kutoaminika na kuondoa uwajibikaji’’, na ‘’inapeleka ujumbe kwa wanajamii kuwa bila utambulisho, maofisa wanaweza kutenda bila kujali kuwajibika’’. Siku za hivi karibuni maofisa wastaafu wengi wa ngazi za juu wa Idara ya Haki wamesemea wasiwasi hu una kuonya kuwa kuruhusu maofisa usalama wa taifa kufanya kazi bila utambulisho kunaweza kuleta athari kubwa ya juhudi za kufuatiliwa mienendo yao na kushindwa kutuma ujumbe kuwa matumizi mabaya ya nafasi zao hakutovumiliwa.
Kadiri waandamanaji wa amani wanavyoendelea kutoka kuheshimu kumbukumbu ya George Floyd na kudai mabadiliko, ni lazima tuhakikishe kuwa usalama na haki zao za kikatiba zinaheshimiwa.
Post a Comment