Ametoa pongezi hizo jana,alipotembelea mradi wa maji wa Milonde kijiji cha Milonde kata ya Matemanga unaotarajia kuhudumia wananchi wapatao 3,600 wa vijiji vinne vya kata ya Matemanga unaotekelezwa kwa wakala wa maji vijijini Ruwasa.
Mradi huo ulioanza kujengwa mwezi April kwa gharama ya shilingi milioni 215,212,257.13 hata hivyo kutokana na matumizi na usimamizi mzuri hadi sasa fedha zilizotumika ni shilingi milioni 44,571,372.25 na kubakiwa na shilingi milioni 170,940,884.88.
Mndeme,amefurahishwa namna Ruwasa wilaya ya Tunduru inavyotumia vizuri fedha za miradi ya maji ilizopewa na Serikali kuu kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa miradi mbalimbali ya maji, ikilinganisha na miradi inayotekelezwa katika wilaya nyingine za mkoa huo.
Alisema, mradi wa maji Milonde ni kati ya miradi bora ya maji inayojengwa na Ruwasa katika mkoa huo, kwani licha ya fedha zilizotumika kuwa kidogo,lakini umekamilika kwa asilimia 90.
“hapa lazima niwe mkweli,nimevutiwa sana na mradi huu wa maji wa Milonde,kwani licha ya ubora wake lakini gharama zilizotumika ni kidogo,nakupongeza sana meneja wa Ruwasa wa wilaya ya Tunduru na Mkurugenzi wa Ruwasa mkoa wa Ruvuma kwa kusimamia vizuri mradi huu,nawaomba hizo fedha zilizobaki zipelekeni zikafanye kazi katika maeneo mengine yaliyobaki”alisema Mndeme.
Alisema, mradi wa maji Milonde umetokana na maombi ya wananchi kwa Rais Magufuri alipopita katika kijiji hicho mwaka jana ambao walimweleza juu ya kero ya muda mrefu ya maji safi na salama, ambaye naye aliwaagiza viongozi wa mkoa wa Ruvuma kushughulikia kero hiyo haraka.
Alisema,wananchi wa Milonde hawana budi kumpongeza Rais Dkt John Magufuri na Serikali kwa kutoa fedha zilizosaidia kutatua kero ya maji na amewataka kutunza mradi ili uwe endelevu na kuleta manufaa.
Mndeme ambaye ni msimamizi wa fedha zinazotolewa na Serikali kwa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo katika mkoa huo alisema, Rais Dkt John Magufuri amedhamiria kumaliza kero mbalimbali za wananchi ikiwemo kero ya maji,elimu,Afya na miundombinu ya barabara kwa lengo la kurahisha maisha ya Watanzania.
Alisema, hayo yote yatafanikiwa iwapo watendaji waliopewa dhamana watekeleza majukumu waliyopewa pia wananchi kushiriki bega kwa bega kwenye ujenzi wa miradi husika.
Kwa upande wake,meneja wa Ruwasa wilaya ya Tunduru Primy Damas alimweleza mkuu wa mkoa kuwa, mradi huo unahusisha pia upanuzi wa mradi wa maji Matemanga, na umegharamiwa na Serikali kuu kupitia wizara ya maji na kutekelezwa na wakala wa maji na Usafi wa Mazingira Tunduru.
Alisema, Utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji ulianza mwezi April 2020 na unatarajia kukamilika mwezi Julai.
Damas alisema, ujenzi wa mradi unahusisha ukarabati wa tenki la kuhifadhia maji lita 100,000,uchimbaji mitaro,ujenzi wa vituo vya kuchotea maji,nyumba ya mitambo,ufungaji umeme wa Rea na ujenzi wa uzio kwenye nyumba ya mitambo na pampu.
Alisema, kazi zilizofanyika hadi sasa ni ukarabati wa tenki kwa asilimia 85,ujenzi wa vituo vitano vya kuchotea maji,nyumba ya mitambo na uzio eneo la nyumba ya mitambo na tenki kazi iliyokamilika kwa asilimia 80.
Aidha alitaja kazi zilizosalia ni kufunga miundombinu ya umeme, kuchimba mitaro, kulaza mabomba na kufunga pampu ya kusukuma maji kwenda kwenye tenki la juu.
Damas alimweleza Mkuu wa mkoa kuwa,miundombinu ya mradi huo inajumuisha vijiji vinne vya Matemanga,Milonde,Changarawe na Jaribuni na ameishukuru Serikali,viongozi ngazi ya kijiji,kata na wananchi wote waliotoa ushirikiano katika kipindi chote cha Utekelezaji wa mradi huo.
Post a Comment