Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi Humphrey Polepole akizungumza leo.
CCMCCM Blog, Dar es Salaam
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepuliza rasmi kipyenga cha mchakato wa kuwapata watakaobeba bendera ya Chama katika kugombea Urais, Ubunge, Uwakilishi na Udiwani katika kinyang'anyiro cha Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Kulingana na ratiba iliyotolewa leo na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi na Uenezi Humphrey Polepole mchakato wa kuwapata wanaoomba kugombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar utaanza siku tatu kuanzia leo.
Polepole amesema wanaotaka kuomba nafasi hizo za Urais wataanza kuchukua fomu tarehe 15/6/2020 na kuanza kutafuta wadhamini ndani ya siku 15, hadi tarehe 30/6/2020 siku ambayo ndiyo ya mwisho kurejesha fomu saa 10 jioni.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, tarehe 6 hadi 7/7/2020 Kitafanyika kikao cha Sekretarieti kuanzisha mchakato, kisha kikao hicho kitafuatiwa na Kikao cha Kamati ya Usalama na Maadili ambacho kitafanyika tarehe 8/7/2020.
Tarehe 9/7/2020 Kitafanyika Kikao cha Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM kufanya shughuli ya
kufikiria na kutoa mapendekezo kwa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) juu ya majina ya wanachama wasiozidi watano (5) tu wanaoomba kugombea urais.
Poloepole amesema, Tarehe 10/7/2020 ndiyo kitafanyika Kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na kufanya kazi ya kuchuja na kupendekeza majina matatu (3) tu ya wagombea urais yatakayokwenda kujadiliwa katika Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM ambao utafanyika tarehe 12/7/2020 kwa ajili ya kuchagua jina moja tu la mgombea urais atakayepeperusha bendere ya CCM dhidi y wagombea wa vyama vingine watakaokuwa vimejitokeza.
Kuhusu mchakato wa kupata wagombea wa Ubunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Uwakilishi kwa Zanzibar, Udiwani na viti maalum, CCM itatoa fomu kuanzia tarehe 14 hadi 17/2020 ambayo itakuwa mwisho wa kurudisha fomu saa 10 jioni.
Post a Comment