Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Ndugu Gerald M. Kusaya anawatangazia wanachuo na wakufunzi kuwa Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo (MATI) vimefunguliwa rasmi tarehe 01 Juni, 2020 kufuatia agizo la Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli alilotoa tarehe 21 Mei, 2020.
Wanafunzi wote wa Vyuo vya Mafunzo ya Kilimo nchini wanatakiwa kuendelea kuripoti vyuoni kwa ajili ya kuendelea na masomo yao. Wizara inawataka wanafunzi wote kuhakikisha wanakuwepo vyuoni ifikiapo tarehe 08 Juni, 2020 na itakapofika tarehe 10 Juni, 2020 Wakuu wa Vyuo vyote wachukue hatua za kinidhamu na kitaaluma kwa wanafunzi ambao watakuwa hawajaripoti vyuoni. Aidha, Wakuu wa Vyuo vyote vya Kilimo wanatakiwa wafanye maboresho ya kalenda ya masomo kwa kuzingatia maagizo ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) yaliyotolewa tarehe 22 Mei, 2020
Wizara ya Kilimo inasisitiza kuwa watumishi na wanafunzi wote vyuoni waendelee kuzingatia kanuni zote za kujikinga na ugonjwa wa homa kali ya mapafu (COVID -19) kama zilivyotolewa katika mwongozo wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu ameelekeza wazabuni wote wanaotoa huduma ya chakula vyuoni, waendelee kutoa huduma hiyo ili kuhakikisha chakula kinapatikana muda ambao wanafunzi watakuwa wakiendelea na masomo yao.
Imetolewa na;
Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Kilimo
DODOMA
05 Juni, 2020
Post a Comment