Mtaalam wa maabara kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Jesca Mlay akimweleza Bilionea Saniniu Laizer namna ambavyo maabara ndogo iliyopo katika banda la JKCI inavyofanya kazi ya huduma za vipimo vya damu vilivyotolewa kwa wananchi wanaotembelea banda hilo alipotembelea banda la JKCI wakati wa Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa leo Jijini Dar es Salaam
………………………………………………………………………………
Na Mwandishi Maalum
Bilionea Saniniu Laizer aipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa huduma za ushauri na upimaji wa magonjwa ya moyo wanazozitoa kwa wananchi wanaotembelea banda la Taasisi hiyo wakati wa Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.
Pongezi hizo amezitoa leo alipotembelea banda la JKCI kwa ajili ya kuona huduma wanazozitoa pamoja na kupata elimu ya lishe na magonjwa ya moyo.
Lazier alisema huduma zinazotolewa ni nzuri kwani zinaokoa maisha ya watu wenye matatizo ya moyo ambao baada ya afya zao kuimarika watakua sehemu ya kukuza uchumi wa nchi yetu.
Kwa upande wake Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Pedro Pallangyo alimshukuru bilionea Laizer kwa kutembelea katika banda lao na kujionea huduma mbalimbali za upimaji na ushauri wa magonjwa ya moyo zinazotolewa.
Dkt. Pedro ambaye pia ni mtafiti wa magonjwa ya moyo alisema ugeni wa Bilionea Laizer katika banda la hilo utawavutia wananchi wengi kufanya vipimo vinavyotolewa na Taasisi hiyo.
Dkt. Pedro alisema mwitikio wa wananchi katika banda la JKCI kwa ajili ya kufanya uchunguzi umekua ukiongezeka mwaka hadi mwaka kwa miaka minne ambayo taasisi hiyo imeshiriki maonyesho Sabasaba.
Mbali na huduma za upimaji wa afya ya moyo na magonjwa mengine sugu, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete pia imejikita kuhakikisha inatoa elimu ya kutosha kwa jamii ili iweze kufahamu sababu hatarishi za magonjwa ya moyo na magonjwa mengine sugu.
“Tulichojifunza katika ushiriki wetu kwenye maonyesho haya ni kuwa wananchi wengi wana shauku ya kujua afya zao ila wengi hawajui ni wapi na kwa namna gani wataweza kufika sehemu stahiki kufanya uchunguzi.
“Uzito mkubwa na shinikizo la damu yameonekana kuwa ni matatizo mawili makubwa ambayo yanakuwa kwa kasi mwaka hadi mwaka katika jamii ya kitanzania.
Ni rai yetu kwa taifa zima kuwa kinga ni bora kuliko tiba hivyo jamii nzima ivalie njuga sababu hatarishi za magonjwa sugu ikihusisha uzito sahihi, ulaji unaofaa, mazoezi ya mara kwa mara, kunywa pombe kwa kiasi au kuacha kabisa, na kutovuta sigara,”. alisema Dkt. Pedro.
Hadi sasa jumla ya watu 1940 wamefanyiwa vipimo katika banda hilo ambapo vipimo vya viashiria vya magonjwa ya moyo ambavyo ni uzito, urefu, sukari mwilini na shinikizo la damu (BP) vimefanyika bila malipo na vipimo vya damu, ECG na ECHO wananchi wanachangia kiasi kidogo cha fedha.
Post a Comment