Chama Cha Mapinduzi kimeipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Chini ya Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa usimamizi wa Uchumi imara, madhubuti na jumuishi ambao umewezesha kuingia katika kundi la nchi zenye uchumi wa kati miaka mitano kabla ya wakati.
Katibu wa NEC – Itikadi na Uenezi ameyasema hayo jana tarehe 04 Julai 2020 Katika Mkutano Mkuu Maalum wa Vyuo na Vyuo Vikuu Mkoa wa Dodoma na uliyohudhuriwa na maelfu ya vijana jijini Dodoma.
Ndg. Polepole anaeleza ni kwa namna gani Sera za CCM zimeelekeza shughuli za maendeleo zilenge kuwatoa wananchi kutoka Tabaka la umaskini na kuishi katika maisha ya staha, utu na kuwezesha ushiriki wao kwenye uzalishaji, biashara na masoko pamoja na fursa jumuishi kwa vijana na wanawake wa kipato cha chini.
Maamuzi makubwa yamefanyika yaliyopelekea uchumi imara yaliyokwenda sambamba na maamuzi ya kimkakati na sahihi kwenye sekta ya madini, usafiri na usafirishaji, viwanda na biashara na sekta nyingine nyingi.
Aidha Polepole amemshukuru na kumpongeza Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa miaka mitano ya kazi kubwa ambayo mafanikio yake yanaonekana na kupelekea kuvuka kwa haraka kulekea uchumi wa kati tofauti na ilivyotarajiwa kwenye Dira ya Maendeleo ya Taifa iliyolenga kufika huko mwaka 2025.
Chama Cha Mapinduzi kimeridhishwa na Utekelezaji wa ilani ya Uchaguzi Mkuu kwa Mwaka 2015 – 2020 na kuingia katika uchumi wa kati ikiwa ni moja ya utekelezaji wa maono ya Chama Cha Mapinduzi na Serikali yake.
Post a Comment