Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, Kanali Michael Ngayalina, akimuongoza Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), kukagua jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe, alipotembelea na kukagua ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya hiyo, Mkoa wa Kigoma.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb), akipokea taarifa ya mradi ya ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Buhigwe mkoani Kigoma, kutoka kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Bw. Rashid Mchata, wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo ambayo Serikali inatoa fedha kuigharamia, alipokuwa ziarani mkoani humo.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango (Mb) (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Wilaya ya Buhigwe na mafundi wanaojenga Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya hiyo baada ya kukagua jengo hilo mkoani Kigoma.Taswira ya Jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe mkoani Kigoma inavyoonekana kwa sasa.
……………………………………………………………………………………
Na: Josephine Majura na Peter Haule KIGOMA
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt Philip Isdor Mpango (Mb), ameupongeza uongozi wa mkoa wa Kigoma na Wilaya ya Buhigwe kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe inayojengwa katika eneo la Bwega, Tarafa ya Manyovu, wilayani Buhigwe mkoani Kigoma na kuagiza Jengo hilo likamilike kabla ya mwezi wa kumi ili wananchi wa wilaya hiyo waanze kupata huduma kwenye jengo hilo jipya.
Dkt. Mpango ametoa pongezi hizo alipotembelea na kukagua ujenzi wa jengo hilo jipya la Ofisi ya MKuu wa Wilaya mpya ya Buhigwe ambalo hadi kukamilika kwake litagharimu shilingi bilioni 1.1
“Nakupongeza Mkuu wa Wilaya na timu yako yote kwa usimamizi mzuri wa Fedha za Serikali, lazima tujenge Makao Makuu ya Wilaya ambayo yataishi kwa miaka mingi, kwa hiyo nimefurahi jengo ninavyoliona hata kama sio Mhandisi lakini ninaona lina ubora”. alisisitiza Dkt. Mpango.
Alimtaka Mkuu wa Wilaya kuendelea kusimamia rasilimali fedha zinazotolewa na Serikali kama alivyofanya kwenye mradi wa ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ili thamani ya fedha za miradi inayotekelezwa ilingane na thamani ya fedha zilizotolewa.
Kwa upande wake, Meneja mradi huo Masawika Kachenje, akisoma taarifa ya ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe amesema kuwa hadi sasa kiasi cha shilingi milioni mia tano (500,000,000) ambazo Serikali zilitoa kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa mradi huo kimetumika kukamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi.
Aliongeza kuwa kiasi cha shilingi milioni (550,000,000), kimebaki ili kukamilisha kiasi cha sh. Bilioni 1.1 ikiwa ni gharama ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi jengo zima, ambapo mipango ya Wilaya ilikuwa kukamilisha ujenzi huo ifikapo mwezi Julai tarehe 15 mwaka 2020.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Buhigwe Kanali, Michaeli Ngayalina, amemshukuru Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Mpango, kwa kutembelea na kukagua baadhi ya miradi inayotekelezwa kwa Fedha za Serikali na kuahidi kuzisimamia vizuri fedha zote zinazotolewa na Serikali kukamilisha miradi ya maendeleo.
Kanali Ngayalina, amemuomba Dkt. Mpango kusaidia upatikanaji wa Fedha zilizobaki ili waweze kukamilisha ujenzi wa ofisi hiyo kama ilivyopangwa kwenye ratiba.
Post a Comment