CCM Blog, Zanzibar
KAMATI Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar imependekeza majina matano kati ya wanachama 32 wa CCM waliokuwa wamechukua fomu za kuomba ridhaa ya Chama kugombea nafasi ya Urais wa Zanzibar.
KAMATI Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar imependekeza majina matano kati ya wanachama 32 wa CCM waliokuwa wamechukua fomu za kuomba ridhaa ya Chama kugombea nafasi ya Urais wa Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Saadalla (Mabodi), amesema Kamati hiyo iliyofanya kikao leo ni sehemu muhimu ya maandalizi na uchujaji wa majina ya wagombea watano wanaotakiwa kuwasilishwa katika Kamati Kuu kwa ajili ya kujadiliwa tena na kumtafuta mgombea mzuri mwenye sifa 12 zikiwemo hekima, kuaminika, kuthamini muungano na Mapinduzi ya Zanzibar.
Dk. Mabodi amesema baada ya Kamati Kuu kujadili kwa kina majina hayo matano itapendekeza majina matatu na kuyapeleka Halmashauri Kuu ya CCM Taifa ambayo itachagua jina la mtu mmoja ambaye atapeperusha bendera ya CCM kwa nafasi ya Urais wa Zanzibar.
Alisema kuwa baada ya hatua hiyo mgombea huyo atapelekwa katika Mkutano Mkuu wa CCM kwa ajili ya kuthibitishwa na kupata baraka za Wajumbe wote wa Kamati Kuu na kuendelea na michakato mingine.
Dk. Mabodi amesema baada ya kukamilika kwa mchakato huo itaendelea awamu ya pili ya uchukuaji wa fomu kwa nafasi za Ubunge, Uwakilishi na Udiwani na kufuata utaratibu wa miongozo ya CCM.
Katika maelezo yake Naibu Katibu Mkuu huyo, amewasifu viongozi kwa ukomavu wao wa kisiasa Kwa kufuata Katiba, miongozo na Kanuni za CCM kwa kutobeba wagombea mifukoni.
Amesema kuwa kikao hicho kimesisitiza usiri kwa wagombea hao kwani ndani ya Chama ikibainika miongoni mwao kuna mtu kakiuka utaratibu anaweza kuondolewa na kuchaguliwa mtu mwingine.
"Lazima tuenzi siri za vikao hivyo ni muhimu sana watu wote kuheshimu maamuzi ya vikao na kufuata utaratibu uliowekwa ndani ya CCM," alisema Dk. Mabodi.
Mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu ulianza Juni 15 hadi 30, mwaka huu ambapo jumla ya makada 32 walijitokeza kuchukua fomu hizo ambao ni Mbwana Bakari Juma, Ali Abeid Karume, Mbwana Yahya Mwinyi, Omar Sheha Mussa, Dk. Hussein Ali Mwinyi, Shamsi Vuai Nahodha, Mohamed Jafar Jumanne, Mohamed Hijja Mohamed, Issa Suleiman Nassor.
Wengine ni Prof. Makame Mnyaa Mbarawa, Mwatum Mussa Sultan, Haji Rashid Pandu, Abdulhalim Mohamed Ali, Jecha Salum Jecha, Dk.Khalid Salum Mohamed, Rashid Ali Juma, Khamis Mussa Omar, Mmanga Mjengo Mjawiri, Hamad Yussuf Masauni na Mohamed Aboud Mohamed.
Wengine ni Bakari Rashid Bakar, Mgeni Hassan Juma, Ayoub Mohamed Mahmoud, Hashim Salum Hashim, Fatma Kombo Masoud, Hasna Attai Masoud, Maalim Hamad Idd Hamad, Pereira Ame Silima, Shaame Mcha, Mussa Aboud Jumbe na Moudline Cyrus Castico.
Post a Comment