Na Bashir Nkoromo
Maadhimisho ya siku ya kuanzishwa rasmi Shule ya Sekondari ya Kawe Ukwamani iliyopo Wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, 'Kawe Day' yaliyofanyika leo, Ijumaa, Agosti 7, 2020, katika shule hiyo yametia fora baada ya kufanyika kwa ufanisi mkubwa.
Maadhimisho hayo yaliyoanza saa 2 asubuhi yalionyesha kufana kutokana na kuhudhuriwa na mamia ya watu wakiwemo wazazi, wakuu wa shule jirani, viongozi wa ngazi mbalimbali katika Kata ya Kawe na Wadau wa maendeleo ya shule hiyo.
Sanjari na mahudhurio, Maadhimisho hayo yalinoga kutokana na Maonesho ya kitaaluma yaliyoanaliwa na walimu na wanafunzi wa shule hiyo kwa umahiri mkubwa na hasa jinsi wanafunzi katika Idara mbalimbali za masomo walivyokuwa wakieleza mambo kadhaa kwa umahiri mkubwa kila mmoja katika eneo la fani ya somo alikopangiwa.
Licha ya fani zote kuwa kivutio, lakini maonyesho kuhusu ujasiriamali na ya sayansi yalionyesha kuvutiwa wengi kiasi cha kuwashangaza baadhi ya wageni baada ya kushuhudia umahiri walioonyesha wanafunzi katika kutengeneza bidhaa mbalimbali ikiwemo nguo za batiki, vinywaji baridi, sabuni za kufulia na za kutakasa mikono kwa kutumia tekonolojia rahisi lakini ya kisasa.
Kuvutia kwa Maadhimisho hayo kulisababisha baadhi ya wazazi hasa wadau wa maendeleo kuamua kuisaidia shule kutatua baadhi ya changamoto huku zingine wakiahidi kuzifanyika kazi kwa kutafuta marafiki watakaokuwa tayari kuzitatua.
Mmoja wa Wadau aliyeonyesha kuguswa ni Davidi Kayuni ambaye aliahidi kuipatia shule kompyuta tano ili kupunguza au kutatua changamoto ya shule hiyo kuwa na kompyuta moja tu na hivyo kukwama katika uchapaji wa kazi mbalimbali.
"Baada ya kuona maonyesho yenu, kwa kweli nimeina kesho yenu ya kuwa wahandisi na wajasiriamali watakaotufikisha kwenye kuunga mkono mwito wa Rais wetu Dk. Magufuli wa kuhakikisha Tanzania tinakuwa ya uchumi wa viwanda. Kwa sababu hiyo mimi kama mdau wa maendeleo, nitaipatia shule hii kompyuta tano ili mzitumie kutafuta kwa njia ya mtandao mambo hayusuyo masomo kwa njia za kisasa", alisema Kayuni.
Mapema, akizungumza shuleni hapo jana, Mkuu wa shule hiyo Safina Egha, amesema, shule hiyo iliyoanzishwa Aprili 16, 2006 ikiwa na wananfunzi 320 na walimu sita ikiwa na majengo mawili yenye vyumba sita, kimoja kikitumika kama ofisi na vitano madarasa ya kufundishia.
Alisema, shule sasa ina majengo tisa, ikiwemo la maabara, la Maktaba na chumba cha huduma ya kwanza na faragha kwa wasichana na kuongeza kuwa shule sasa ina walimu 42 na mtaalamu mmoja wa maabara walinzi watatu, walimu 15 wanaojitolea na walimu 26 wa mazoezi huku shule ikiwa na jumla ya wananfunzi 1280 ambao kati yao wasichana ni 617.
Mkuu wa shule hiyo alizitaja changamoto zinazoikabili shule hiyo kuwa ni pamoja na ukosefu wa kompyuta, akisema iliyopo ni moja ambayo inatumiwa na Utawala na na Taaluma na hivyo kusababisha ucheleweshaji wa kazi za kila siku na kwamba shule inayo mashine ya kurudufia ambayo bado inadaiwa malipo yake.
Alisema changamoyo nyingine ni shule kuwa na matundu machache ya vyoo kulingana na idadi kubwa ya wanafunzi waliopo na pia baadhi ya sehemu za shule hazina uzio hivyo walimu kulazimika kutumia muda mwingi kuwachunga watoto.
Mkuu huyo wa shule alisema, kwa kuwa shule hiyo imeweka lengo la kupandisha ufaulu kwa asilimia 95 na kupunguza alama 0 kutoka digiti 2 hadi digiti moja na kufuta daraja sifuri kabisa, hivyo ni muhimu sana wadau wa elimu na Mamlaka zenye uwezo kutoka kipaumbele katika kusaidia kuondoa changamoto zote ambazo ni tishio katika utoaji wa elimu na makuzi ya wanafunzi.
Katima Maadhimisho hayo Mgeni rasmi alikuwa Katibu wa CCM Kata ya Kawe, Fatma Wawadhi ambaye katika hotuba yake alitoa mwito kwa wadau kuendelea kusaidia shule mbalimbali zilizomo katika Kata hiyo hasa zile zinazoonyesha uhitaji mkubwa kama Kawe Ukwamani.
Fatma ambaye alifuatana na viongozi kadhaa wa CCm katika Kata hiyo aliahidi kuwa karibu na uongozi wa Kawe Ukwamani kwa kuzichukua changamoto na kuzipeleka ngazi za juu ili kupatiwa majibu.
Mwishoni, Mkuu wa taaluma wa shule hiyo Mwalimu Chacha alitangaza wanafunzi na walimu bora na kupatiwa zawadi mbalimbali kufanya vizuri zaidi katika matokeo ya mitihani mitihani mbalimbali, ambapo kwa kitacho cha chanza walipatiwa zawadi kutokana na kuwa katika tatu bora kuwa ni 1. Josephati Peter 2. Baraka Makali 3. Christian Mwaisapula.
Kwa kidato cha Pili ni 1. Vitalisi Kimario, 2. Abubakari Mkamba, 3. Michael Marashi na Kidaco cha Tatu kuwataja kuwa ni 1Elvin Valentino, 2. Baraka Kulembelwa, 3.Rebecca Martin, huku Kidato cha Nne wakiwa ni 1.Bushir Mataja, 2. Tamia Msonda na 3.Irene Nyamhanga. KUONA PICHA MOTOMOTO ZA MAADHIMISHO HAYO, TAFADHALI BONYEZA HAPA
Post a Comment