WATU lukuki hapa nyumbani Tanzania, Afrika Mashariki, Afrika na nje ya bara la Afrika, wanaguswa na msiba wa Rais wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Benjamini Mkapa. Hayati Mkapa alifariki usiku wa manane wa kuamkia Julai 24, mwaka huu, Jijini Dar es Salaam.
Binafsi nimeguswa na kifo hiki kwa sababu ni mtu niliyemfahamu kwa karibu na nilifanya naye kazi kwa miaka mine, kuanzia mwaka 1968 hadi 1972, katika magazeti ya Chama cha TANU; la Kiingereza, The Nationalist na la Kiswahili, Uhuru.
Mzee Mkapa alikuwa Mhariri Mtendaji wa magazeti yaliyokuwa yakitolewa na Kampuni ya TANU ya Mwananchi Publishing 1966 Ltd, mwandishi wa makala hii nikiwa mwajiriwa katika Idara ya Habari, Kitengo cha ‘Proof Reading’, kuanzia Januari 1968 na baadae kupanda ngazi hadi kufikia ngazi ya kuwa Mhariri wa Habari. Hivyo katika makala hii, nitaelezea jinsi nilivyomfahamu Mzee Mkapa katika utendaji wa kuyaongoza magazeti hayo mawili.
KAZI KUBWA ZA MAGAZETI YA CHAMA
Kazi kubwa ya magazeti ya The Nationalist na Uhuru, zilikuwa kama tatu hivi; Gazeti la The Nationalist, lililenga zaidi kutangaza habari za ukombozi, hasa Kusini mwa Afrika na nchi nyingine zilizokuwa chini ya ukoloni katika maeneo mengine ya Afrika na nje ya bara la Afrika. Kwa mfano, wakati huo Vietnam ya Kusini, ambayo ilikuwa katika vita ya ukombozi dhidi ya Marekani.
Marehemu Mzee Mkapa, mwaka 1968, akiwa Mhariri wa The Nationalist, alitumwa na Chama cha TANU kupeleka msaada wa chakula Vietnam, kusaidia ukombozi wa nchi hiyo. Alipeleka tani kadhaa za katoni za nyama za ng’ombe za makopo zilizosindikwa wakati huo na kiwanda cha Tanganyika Packers , kilichokuwepo Kawe, moja ya vitongoji kaskazini mwa Jiji la Dar es Salaam.
Nchi zilizokuwa katika harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika wakati huo, kuanzia miaka ya 1960 hadi miaka ya 1990 ni pamoja na Mozambique sasa Msumbiji, Southern Rhodesia (Zimbabwe), Angola, Namibia na Afrika Kusini.
Hayati Mkapa, alipokuwa akiyaongoza magazeti hayo, kazi ya pili kubwa ya magazeti ilikuwa ni kulitangaza Azimio la Arusha na misingi yake ya Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Azimio la Arusha lilitangazwa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Awamu ya Kwanza, katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na mamia ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam, katika viwanja vya Mnazi Mmoja, Februari 5, 1967. Wakati huo, marehemu Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Mzee Mkapa, alikuwa na miezi saba tangu alipoteuliwa kuwa Mhariri Mtendaji wa magazeti ya The Nationalist na Uhuru.
Kazi ya tatu kubwa ya magazeti hayo, hasa gazeti la Uhuru, ilikuwa kutoa elimu ya watu wazima au wakati huo kikijulikana kama kisomo cha Ngubaru au Kisomo Chenye Manufaa. Gazeti la Uhuru lilitenga ukurasa maalumu katika toleo lake la kila siku, kuweka makala za elimu ya watu wazima. Makala hizi ziliandikiwa na Idara ya Elimu ya Watu Wazima katika Wizara ya Elimu.
Marehemu Mkapa, alisimamia kazi hizi tatu kubwa kwa umakini na weledi, kwani ilikuwa ni mwiko kwa makala ya Elimu ya Watu Wazima ikosekane kutokana na maagizo ya TANU, chini ya uongozi wa Rais wa TANU, ambaye pia ni Rais wa Serikali, Hayati Mwalimu Nyerere.
ALIVYOUTUMIA UJUZI WAKE WA KIINGEREZA
Pia, Mhariri huyu msomi alikuwa anaandika Tahariri au kwa lugha ya wakati ule Maoni ya Mhariri kwa magazeti hayo. Pale ilipotokea kuwapa majukumu hayo wasaidizi wake, ambao ni wahariri waandamizi, alihakikisha anazipitia tahariri kabla ya gazeti kupelekwa kuchapwa mtamboni. Alikuwa makini zaidi na Tahariri iliyoandikwa kwa Kiingereza kwa ajili ya The Nationalist. Aliisoma ili kujitosheleza kama Kiingereza kilichoandikwa kilikuwa fasaha.
Tukumbuke kuwa Mzee Mkapa alikuwa bingwa wa lugha ya Kiingereza kwa kuzungumza na kuandika, kwani shahada yake ya kwanza ilikuwa ni kwa somo la Kiingereza, aliyoipata Chuo Kikuu cha Makerere, kilichopo mjini Kampala, nchini Uganda. Aliweza kuzungumza kwa lafudhi ile ile ya Waingereza.
Mzee Mkapa alitoa mafunzo kwa waandishi wa habari chipukizi, hasa wa gazeti la Kiingereza la The Nationalist ndani ya chumba cha habari. Kuna wakati alichukua muda kuzunguka ndani ya chumba kwenye madawati ya waandishi na kuwasaidia kunyoosha lugha ya Kiingereza. Hakusita kumuomba mwandishi ampishe kidogo kwenye kiti ili amsaidie mwandishi kumnyooshea habari; hasa katika ibara ya kwa kwanza (INTRO) enzi zile zilitumika ‘TYPEWRITER’ na Hayati Mkapa alikuwa hodari, mwepesi na mwenye spidi sana kuandika kwa kutumia typewriter. Na kama sikosei, alikuwa pia mjuzi wa ‘HATI MKATO’(Shorthand).
Kutokana kukimanya vizuri Kiingereza, Radio Tanzania ilimtumia sana kusoma taarifa ya habari ya Kiingereza, saa moja usiku.Taasisi hizi mbili Mwananchi Publishing na Radio Tanzania, zilikuwepo jirani umbali wa kama kilomita moja, kutoka moja hadi nyingine, katika barabara ya Pugu, sasa Nyerere. Akitoka kusoma taarifa Radio Tanzania, lazima arudi ofisini, The Nationalist, kuona kama mambo yako sawa katika mchakato wa kutoa gazeti. Kwanza alirudia kusoma Tahariri na kuangalia vichwa vya habari, hasa katika gazeti la The Nationalist.
Wakati mwingine alilazimika kubakia ofisini ili kusubiri Tahariri iliyoandikwa na Mhariri Mkuu, Mwalimu Nyerere, kutoka Ikulu. Akishaisoma na kukubaliana nayo, aliruhusu iendelee kuwekwa katika mchakato wa kuchapishwa katika gazeti.
MFUATILIAJI WA CHAKUBANGA
Kwa gazeti la Uhuru, Mzee Mkapa alihakikisha safu za mashahiri, barua za wasomaji na kibonzo (CARTOON) cha CHAKUBANGA havikosekani kwenye kila toleo. Na kwa taarifa kwa wewe unayesoma makala hii, safu hizo tatu zilikuwa zinatoa mafunzo ya maisha ya kila siku kwa jamii.
Hayati Mwalimu Nyerere, jambo la kwanza kusoma akipata gazeti la Uhuru ilikuwa ni mashairi na kufuatilia kibonzo cha Chakubanga. Mwalimu alikuwa mpenzi wa Chakubanga, ambacho kilikuwa na maneno ya mafunzo kwa lugha ya utani ya akina Chakubanga, Polo, Mzee Bushiri, Chupaki na Mama Chupaki.
Mwalimu Nyerere, pia alikuwa mtunzi maarufu wa mashairi na yalichapishwa katika gazeti la Uhuru. Msanifu Mkuu wa mashairi yaliyochapishwa katika Uhuru, alikuwa marehemu Mzee Saadani Abdul Kandoro.
Mhariri Mkapa, wakati huo alikuwa anamfuatilia mwenyewe mtu na mchoraji wa kibonzo cha Chakubanga, marehemu Christian Gregory, aliyekuwa mkazi wa Mbagala, maeneo ya Kizuani. Gregory alikuwa mfanyakazi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), kilichopo kwenye makutano ya barabara ya Samora, wakati huo ikijulikana kama Independence na baadaye mtaa wa Samora, Dar es Salaam.
Kwa faida ya kizazi kipya cha DOT COM, wakati wa utawala wa Waingereza, barabara inayoitwa Samora, sasa ilikuwa inaitwa Acacia Avenue. Baada ya Tanganyika kupata Uhuru, Desemba 9, 1961, ilibadilishwa jina na kuitwa Independence Avenue na baadae kwa heshima ya Rais wa Kwanza wa Msumbiji huru, iliyopata uhuru wake Juni, 1975, Samora Moses Machel, barabara ilibadilishwa tena jina na kuitwa Samora Avenue.
WAHARIRI WALIOMSAIDIA KUBORESHA MAGAZETI
Katika utendaji wake katika magazeti ya Nationalist na Uhuru, Mzee Mkapa alikuwa na wasaidizi mahiri waliokuwa wahariri waandamizi, ambao ni Gray Likungu Mattaka, aliyekuwa Mhariri wa Habari wa The Nationalist, lakini aliondolewa baada ya kuhusishwa na njama za uhaini kutaka kuipindua serikali ya Mwalimu Nyerere.
Baadae Mattaka na wahaini wenzake, wakiwemo Bibi Titi Mohamed, Michael Mowbrey Kamaliza, William Magori Chacha na Dunstan Lifa Chipaka, walifunguliwa mashitaka. Oscar Kambona alikuwa mmoja wa washitakiwa, lakini alikimbilia mafichoni Uingereza. Wote walipatikana na hatia na walihukumiwa na Jaji Mkuu wa kwanza baada ya uhuru, Philip Telfer Georges.
Baada ya kutumikia kifungo kwa miaka kadhaa, walipata msamaha. Jaji Mkuu, Georges, baada ya kumaliza mkataba wake, alirudi kwao Trindad na Tobago na akarithiwa na Jaji Mkuu wa kwanza mzalendo, Augustino Saidi.
Nafasi ya Mattaka ya Mhariri wa Habari, ilizibwa na Ferdinand Ruhinda, na wasaidizi wenzake wa Mhariri Mkapa walikuwa marehemu Costa Kumalija (Naibu Mhariri , The Nationalist), Damian Chokunogela a.k.a Kaka Miye (Mhariri wa Uhuru) na Nsa Kabenga Kaisi, akiwa Mwandishi Mkuu. Mkapa, Kumalija, Ruhinda na Nsa Kaisi, walikuwa wanaitana Comrade, yaani Swahiba mpambanaji kwa tafsiri yangu isiyo rasmi.
WATALAMU KUTOKA GHANA NA NIGERIA
Ili kuhakikisha gazeti la The Nationalist linatolewa kwa lugha sanifu na fasaha, Chama cha TANU kiliwaleta watalamu wa tasnia ya habari kutoka Ghana na Nigeria, ambao walisaidia sana kutoa mafunzo kwa waandishi wazalendo katika tasnia hii. Walioletwa kutoka Ghana na Nigeria kwa nyakati tofauti, kuanzia miaka ya mwisho ya 1960 ni pamoja na James Makham (Ghana), Assare (Ghana) na Nwanko na Okudo (Nigeria).
Marehemu Mzee Mkapa, akiwa Mhariri Mtendaji wa The Nationalist na Uhuru, alimkaribisha marehemu Kanyama Chiume (Waziri wa zamani wa Mambo ya Nchi za Nje wa Malawi, ambaye alisigana na Rais Hastings Kamuzu Banda wa nchi hiyo). Marehemu Chiume alikuwa ametoa mchango mkubwa sana katika harakati za ukombozi kusini mwa Afrika kwa kuandika makala za kuunga, kuhamasisha na kuchochea vita vya ukombozi. Chiume alikuwa anatumia jina la ‘Che Ng’ombo’.
MAGAZETI KUWAHISHWA KWENYE MAJUMBA YA SINEMA NA BAA
Wakati huo, kituo cha kwanza cha kufikisha magazeti kilikuwa Ikulu, Magogoni, Dar es Salaam na baadae yalisambazwa kwenye baa, katikati ya jiji, ambazo ni Makange, mtaa wa Nkurumah, klabu ya usiku ya Gateways, Splendid, New Palace, Palm Beach, Princess, Lucky Bar, White Horse, Kibarua baa namba 1 Arnautoglo, Kibarua baa namba 2 Amana na Pombe shop, Kariakoo. Pia magazeti yalisambazwa usiku huo katika majumba ya sinema ya New Chox, Avalon, Cameo, Odeon, Empire na Empress, yote katikati ya Jiji.
Gazeti la The Nationalist lilikuwa na upinzani na ushindani na gazeti la Kiingereza la The Tanganyika Standard (sasa Daily News). Hivyo watendaji wa wote wa The Nationalist walikuwa na maagizo maalumu kwamba, gazeti lazima liwe mitaani kuanzia saa moja na nusu hadi saa mbili usiku. Iilikuwa ni lazima kuwahi sokoni ili kukabili ushindani na ilikusudiwa kuwa mteja anaposikiliza Taarifa ya Habari ya Radio Tanzania, saa mbili usiku, awe tayari na gazeti la The Nationalist mkononi. Marehemu Mzee Mkapa alikuwa msimamizi wa mbele kuhakikisha hayo yanatekelezwa.
VITENDEA KAZI DUNI
Nakumbuka Mzee Mkapa alikuwa na gari aina ya kobe (Volkswagen), iliyochokachoka au kwa lugha ya zamani tungeiita mkweche. Lakini baadae ofisi ilinunua gari jipya pia aina kobe, lenye usajili namba TDT 901 na Mzee Mkapa aliitumia hadi alipoondoka 1972.
Ruhinda alikuwa na gari aina ya Morris Minor na Kumalija alikuwa na kobe pia iliyochoka, ikiwa na ngurumo mfano wa mabomu yanayolipuka na mwenyewe aliita ‘Viet Cong’, akilifafanisha na mabomu yaliyokuwa yanarindima wakati kwenye vita vya ukombozi nchini Vietnam Kusini, ambapo wananchi walikuwa wanapambana na majeshi ya Marekani, ambayo hatimaye yalivurumishwa na kusalimu amri na kukimbia kurudi Marekani, mwaka 1975.
Ushindi huo wa wapiganaji wa vita vya msituni wa Vietnam, ulizifanya nchi hizo mbili, Vietnam Kaskazini na Kusini, ziungane na mji wa Saigon, uliokuwa makao makuu ya Vietnam Kusini, ulibadilishwa jina na kuitwa Ho Chi Minh, kwa heshima ya kiongozi wa nchi hiyo, aliyeongoza vita vya msituni, Comrade Ho Chi Minh.
HAKUISAHAU UHURU
Mzee Mkapa, hata alipoondoka baada ya kuteuliwa kuwa Mhariri Mtendaji wa magazeti ya Serikali ya Daily na Sunday News, na baadae kushika nyadhifa mbalimbali, hakuyasahau magazeti ya Chama, ambako alianzia kazi ya uandishi wa habari.
Ushahidi ni alipokuwa Rais wa Awamu ya Tatu, uongozi wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo, ulimuomba kukutana naye ili kumueleza changamoto katika uendeshaji wa magazeti hayo. Mzee Mkapa bila kinyongo, alikubali na akawakaribisha kuonana naye, Ikulu, Dar es Salaam.
Timu ya waandishi waandamizi watatu, wakiongozwa na Mhariri Mtendaji, Said Nguba, Naibu Mhariri Mtendaji, Josiah Mufungo na Mwandishi wa makala hii (Joe Nakajumo), ambaye alikuwa Mhariri wa Habari, walikutana na Rais Mkapa, ambaye pia wakati huo alikuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi.
Uongozi wa Uhuru ulimwelezea matatizo na changamoto za uendeshaji magazeti; makubwa yakiwa ni madeni sugu yaliyolimbikizwa na wizara na taasisi mbalimbali za serikali. Tatizo lingine lilikuwa ni ukosefu wa magari ya kufanyia kazi.
Mara moja, Rais Mkapa alitoa maelekezo kwa wizara na taasisi za serikali kulipa madeni na wengi walianza kutekeleza maelekezo yake. Kwa kusaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa magari, Mwenyekiti Mkapa aliyanunulia magazeti ya Uhuru, gari dogo aina ya Suzuki, ambalo kwa kweli lilisaidia kuimarisha utendaji wa kazi.
ALIPENDELEA KUVAA KIMAO
Hayati Mkapa, wakati akiwa Mhariri Mtendaji wa magazeti hayo ya Chama, alipendelea kuvaa shati la ’mkogo’, kwa majina mengine Kimao, Chou En Lai na Haki ya Mungu. Kivazi hicho kilivaliwa sana na maofisa wa serikali, taasisii za umma na wanasiasa.
Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ndicho kilikuwa kivazi chake rasmi. Hii ilitokana na kuwaiga Wachina, wakiongozwa na Mwenyekiti, Mao Tse Tung. Kwa wakati huo wa vita baridi, wananchi wa Jamhuri ya Watu wa China walikuwa na urafiki mkubwa na wa karibu na Tanzania katika bara la Afrika.
Kwa kumalizia makala hii, namshukuru sana marehemu Hayati Benjamin William Mkapa, aliyezaliwa mwaka 1938 na kufariki mwaka huu wa 2020, kwa kunipokea na kunipa nafasi kufanyakazi katika magazeti aliyoyaongoza na kunifanya nikulie na kuzeekea kwenye tasnia ya habari. Kwa sasa baada ya kustaafu, naendelea na taaluma ya uandishi wa habari nikiwa mwandishi wa kujitegemea. Napatikana kwenye simu namba 0784291434.
MWENYEZI MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU BENJAMIN MKAPA MAHALI PEMA PEPONI.
Post a Comment