Mkutano wa 40 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), unaotarajiwa kufanyika tarehe 17 Agosti, 2020 kwa njia ya mtandao (video conference) Ikulu Chamwino Jijini Dodoma.
Akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi, Brigedia Jenerali, Wilbert Ibuge amesema mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali utatanguliwa na vikao vya Kamati ya kudumu ya Maafisa Waandamizi/Makatibu Wakuu na Mkutano wa Baraza la Mawaziri itakayoanza kufanyika tarehe 10 -13 Agosti, 2020 jijini Dar es Salaam kwa njia ya mtandao (video conference).
"Kulingana na taratibu na miongozo ya uendeshaji wa SADC, nafasi ya uenyekiti hushikiliwa na nchi wanachama kwa kupokezana kwa kipindi cha mwaka mmoja mmoja. Tanzania imekuwa Mwenyekiti tangu Mwezi Agosti, 2019 na inatarajwa kukabidhi Uenyekiti kwa Jamhuri ya Msumbiji katika Mkutano huo. Aidha, itakumbukwa kuwa mara ya mwisho Tanzania ilishika nafasi hii mwaka 2003," Amesema Balozi Ibuge.
Ameongeza kuwa, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa sasa wa SADC, atakabidhi Uenyekiti kwa Mheshimiwa Philipe Jacinto Nyusi, Rais wa Jamhuri ya Msumbiji tarehe 17 Agosti 2020 jijini Dodoma kwa njia ya Video Conference.
Balozi Ibuge ameongeza kuwa, kwa kuwa kwa sasa Kiswahili ni moja kati ya lugha rasmi za mikutano ya SADC, lugha hiyo itatumika katika ngazi ya Mkutano wa Baraza la Mawaziri na ngazi ya Wakuu wa Nchi na Serikali.
Aidha, Katibu Mkuu, Balozi Ibuge amesema kuwa, kutokana na janga la COVID-19 na mwongozo uliotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) juu ya kufanya mikutano ya ana kwa ana, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania italazimika kukabidhi uenyekiti kwa njia ya mtandao ambapo Balozi wa Msumbiji hapa nchini atakabidhiwa uenyekiti kwa niaba ya nchi yake. Hali kadhalika, Balozi wa Tanzania nchini Msumbiji atakabidhi Uenyekiti kwa Serikali ya Jamhuri ya Msumbiji kwa niaba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika hatua nyingine, Balozi Ibuge amesema kuwa mkutano huo utaongozwa na kauli mbiu ambayo ni “Miaka 40 ya Kuimarisha Amani na Usalama, Kukuza Maendeleo na kuhimili Changamoto zinazoikabili Dunia” ambapo kauli mbiu hiyo inatakiwa kutekelezwa na nchi zote Wanachama.
Mkutano huo unatarajiwa kushirikisha Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka nchi 16 wanachama wa SADC wakiwa katika nchi zao. Nchi hizo ni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jamhuri ya Angola, Jamhuri ya Botswana, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Muungano wa Visiwa vya Comoro, Ufalme wa Eswatini, Ufalme wa Lesotho, Jamhuri ya Namibia, Jamhuri ya Visiwa vya Shelisheli, Jamhuri ya Afrika Kusini, Jamhuri ya Malawi, Jamhuri ya Msumbiji, Jamhuri ya Mauritius, Jamhuri ya Madagascar na Jamhuri ya Zambia, Jamhuri ya Zimbabwe.
Post a Comment