Featured

    Featured Posts

RAIS WA TANZANIA DK. MAGUFULI AKABIDHI UENYEKITI WA SADC KWA RAIS WA MSUMBIJI FILIPE NYUSI, IKULU CHAMWINO, DODOMA, LEO

Mwenyekiti aliyemaliza muda wake wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Rais wa tanzania Dk. John akikabidhi Uenyekiti wa Jumuiya hiyo kwa Balozi wa Msumbiji hapa nchini Monica Patricio Clemente ambaye alipokea kwa niaba ya Rais wa Msumbiji Filipe Jacinto Nyusi, Ikulu ya Chamwino, Dodoma, leo

Ikulu, Chamwino, Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 17 Agosti, 2020 amekabidhi uenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwa Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Mhe. Filipe Jacinto Nyusi baada ya kuongoza Jumuiya hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita.

Makabidhiano hayo yamefanyika katika mkutano wa 40 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika kwa njia ya mtandao kwa kuwaunganisha viongozi wakuu 16 kutoka nchi wanachama ambapo Mhe. Rais Magufuli amekabidhi uenyekiti akiwa Ikulu, Chamwino Mkoani Dodoma.

Katika mkutano huo, Rais wa Jamhuri ya Malawi Mhe. Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa SADC akipokea kijiti kutoka Mhe. Rais Nyusi, Rais wa Jamhuri ya Botswana Mhe. Mokgweetsi Masisi amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya SADC (SADC Organ) na Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini Mhe. Matemela Cyril Ramaphosa amechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa SADC Organ.

Akizungumza kabla ya kukabidhi uenyekiti wa SADC, Mhe. Rais Magufuli amewashukuru Wakuu wa Nchi na Serikali wa nchi zote wanachama wa SADC kwa ushirikiano waliouonesha katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wake ambapo SADC imepiga hatua kubwa katika kutimiza malengo yake makuu.

Mhe. Rais Magufuli ameyataja baadhi ya maeneo ambayo yamepata mafanikio makubwa wakati wa uongozi wake kuwa ni kuendelea kusimamia amani, ulinzi, utawala bora na demokrasia ambapo licha ya kuwa Jumuiya iliyokuwa na amani zaidi ikilinganishwa na Jumuiya zingine, nchi 5 za Botswana, Msumbiji, Namibia, Mauritius na Malawi zimefanya uchaguzi kwa amani.

Eneo jingine ni kuimarisha utengamano wa kiuchumi ambapo mfumo wa kutambu asili ya bidhaa (e-certificate on rules of origin) umeanzishwa, Baraza la Biashara la SADC limeanzishwa, megawati 3,595 za umeme zimeongezwa na kuingizwa katika gridi za nchi wanachama, na pia Tanzania/Zambia na Malawi/Msumbiji zimeingia katika makubaliano ya kusafirisha umeme.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amesema katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita SADC imeweza kutengeneza ajenda mpya za ndani ya Jumuiya ambapo Dira ya SADC ya mwaka 2050 imeandaliwa na pia mpango elekezi wa maendeleo ya kikanda wa 2020 – 2030 umekamilika.

Mafanikio mengine ni kusimamia kwa ukaribu uondoaji wa vikwazo dhidi ya Zimbabwe, kuingiza lugha ya Kiswahili kuwa miongozi mwa lugha 4 rasmi za SADC na kuiongoza Jumuiya bila kutetereka katika kipindi kigumu cha janga la virusi vya Corona (Covid-19) ambapo Tanzania iliendelea kuzihudumia nchi wanachama likiwemo jukumu muhimu la kusambaza dawa za binadamu.

Wakuu wa Nchi na Serikali walioshiriki mkutano huo wametoa salamu za pole kwa Mhe. Rais Magufuli na Watanzania wote kwa kuondokewa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Hayati Benjamin William Mkapa ambaye wamemuelezea kuwa alikuwa kiongozi hodari aliyeipenda SADC na kuzisimamia vizuri ajenda za Jumuiya hiyo hata baada ya kustaafu uongozi wake.

Wakuu wa Nchi na Serikali pia wamempongeza Mhe. Rais Magufuli kwa uongozi wake wa mwaka mmoja ambapo SADC imepiga hatua kubwa na wameahidi kuendeleza juhudi kubwa alizozianzisha katika kusimamia ajenda za Jumuiya kwa ustawi wa uchumi, ulinzi, usalama, amani, ustawi na ustawi wa wananchi.
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana