Mlalamikiwa katika shauri hilo, Peter Joseph ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kijiji hicho cha Igombwe akizungumzia mgogoro huo.
Na Dotto Mwaibale, Singida
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ( TAKUKURU) Wilaya ya Ikungi mkoani Singida imefanikiwa kuokoa ng’ombe saba wenye thamani ya sh.milioni 3.5 na shamba la ekari 36 mali ya Jumanne Athuman mkazi wa Kitongoji cha Mfumbuahumba Kijiji cha Germani Kata ya Igombwe wilayani humo.
Akizungumza mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo wakati wa kumkabidhi ng’ombe hao pamoja na sh.150,000, Mkuu wa TAKUKURU wa Wilaya hiyo, Erick Nyoni alisema mali hiyo ilikuwa ni ya Jumanne Athumani lakini kutokana na mgogoro wa ardhi kati yake na Peter Joseph ambao uliwafikisha baraza la ardhi la kata Joseph alifanikiwa kushinda kesi baada ya kudaiwa kughushi nyaraka ya kijiji ambayo ilikuwa ikionesha eneo hilo la mgogoro alikabidhiwa na Serikali ya kijiji cha Igombwe wakati sio kweli.
“Mlalamikaji Jumanne Athumani alipofika ofisini kwetu kulalamika tulifanya uchunguzi wa kina na kubaini ile nyaraka ilighushiwa na kupelekea baraza la ardhi kumpa ushindi na hata alipokata rufaa kwenda baraza la ardhi la wilaya pia lilimpa ushindi Peter Joseph” alisema Nyoni.
Kutokana na ushindi huo ilimlazimu Jumanne Athumani kuliachia eneo hilo la ekari 36 lakini kutokana na uchungu aliokuwa ilikuwa vigumu kwake kuondoka.
Nyoni alisema baada ya kuona hatoki kwenye eneo hilo Joseph alikwenda kumshitaki kwa madai kuwa amevamia ambapo alifungwa miaka miwili na baada ya kutoka gerezani alifunguliwa tena kesi ya madai ambayo ilisababisha ng’ombe wake tisa wachukuliwe na Peter Joseph.
“Mkuu wa wilaya leo utamkabidhi ng’ombe saba, sh.150,000 ya gharama za zile hukumu zilizotolewa pamoja na ekari zake 36 ndugu Athumani” alisema Nyoni.
Akimkabidhi ng’ombe hao Mpogolo alimshukuru mkuu wa TAKUKURU wa wilaya hiyo na wafanyakazi wenzake wote kwa kazi wanayoifanya wilayani humo ambapo katika kipindi kifupi wameweza kufanya kazi kubwa ya kurejesha haki za watu zilizopotea na fedha zilizochukuliwa na vyama vya msingi.
“Leo hii ni sehemu ya ishara kwani wamekwisha wahi kurejesha ng’ombe kama hawa katika Jimbo la Singida Mashariki na sasa wamerejesha ng’ombe saba, ekari 36 pamoja na uhuru wa ndugu Jumanne Athumani” alisema Mpogolo.
Mpogolo alisema mtoaji wa hukumu hiyo alitoa kwa haki baada ya kupata ushahidi ambao ulikuwa batili kwenye vyombo vya sheria.
Alisema tuendelee kumpongeza Rais John Magufuli kwa kuwa ndiye aliyeamua kuifanyia mabadiliko mapya TAKUKURU na kuipa majukumu mengine ya ziada kwani tulizoea kuona wakishughulika na watu waliokuwa wakitoa na kupokea rushwa lakini sasa inafanya kazi nyingi ya kutafuta haki hata kama mtu atakuwa aliipoteza kwa miaka mingi lengo likiwa ni kurudisha haki kwa watanzania.
Mpogolo alitumia fursa hiyo kuomba wahusika na jamii kwa ujumla kuangalia uhalali wa nyaraka mbalimbali zinazopelekwa mahakamani kwani zingine zinakuwa batili na kuweza kupindisha haki.
Jumanne Athumani akipokea ng’ombe hao aliishukuru serikali ya awamu ya tano kwa hatua mbalimbali za kuwasaidia wanyonge kwani katika kipindi cha miaka tisa alikuwa katika mateso makali baada ya kupokwa haki yake.
Kwa upande wake Peter Joseph ambaye alikuwa ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Igombwe aliyekuwepo kwenye makabidhiano hayo alikiri kuwepo kwa mgogoro wa ardhi dhidi yake na Athumani na kudai haki ilikuwa ni yake ila changamoto iliyojitokeza ni wajumbe kughushi saini ndio kuliko sababisha ipotee licha ya awali kupata ushindi.
Joseph alimshukuru mkuu wa wilaya na TAKUKURU wilayani humo kwa kumaliza mgogoro huo na kusema jambo hilo halitajirudia tena na akashauri sasa kuanza kwenda kanisani kusali akimaanisha kutubu.
Post a Comment