Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Siku za Jumamosi na Jumapili za mwishoni mwa wiki hii, zinatarajiwa kuwa na 'patashika nguo kuchanika' wakati Chama Cha Mapinduzi (CCM) kitakapokuwa kinazindua Kampeni zake za Uchaguzi wa Ubunge na Udiwani katika Majimbo ya Kawe na Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Katibu wa CCM Wilaya ya Kinondoni Sure Mwasanguti amesema leo kwamba Jumamosi Septemba 12, 2020 CCM itazindua kampeni zake katika Jimbo la Kinondoni katika mkutano wa kukata kwa shoka utakaofanyika katika Viwanja vya Biafra, Kinondoni, kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 12 jioni.
Chama Cha Mapinduzi kimemkabidhi bendera Kada wake Abbas Tariba kuipeperusha katika kugombea Ubunge jimbo hilo la Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Mwasanguti amesema, baada ya kivumbi kutimka katika jimbo hilo la Kinondoni, kesho yake Jumapili Septemba 13, 2020 kivumbi kitahamia jimbo la Kawe utakapofanyika mkutano unaotarajiwa kuwa wa kihistoria katika Viwanja vya Shule ya Msingi Bunju "A", Bunju, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Amesema, katika mkutano huo, pamoja na kuzindua kampeni zake CCM itamnadi mgombea ambaye chama kilimteua kupeperusha bendera yake katika jimbo hilo Askofu Dk. Josephat Gwajima na mkutano utarindima kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 12 jioni .
Mwasanguti amewakaribisha wanachama wa Chama Cha Mapinduzi na wananchi kwa ujumla kufika kwa wingi kwenye mikutano hiyo, huku wana CCM wakiwa katika sare zao za Chama.
Post a Comment