Featured

    Featured Posts

RAIS DK. MAGUFULI NA RAIS NDAYISHIMIYE WA BURUNDI WAKUBALIANA MAMBO NYETI, MJINI KIGOMA, LEO

Rais Dk. John Magufuli na Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye, leo mjini Kigoma.


Na CCM Blog, Kigoma

Rais Dk. John Magufuli na  Rais Evariste Ndayishimiye wa Burundi wamekubaliana kuimarisha na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wa nchi zao ikiwemo kuongeza biashara na uwekezaji, kuimarisha usalama, kukuza miundombinu ya usafirishaji na kubadilishana uzoefu katika rasilimali ya madini na kukuza utalii. 


Viongozi hao wamefikia makubaliano hayo katika mazungumzo rasmi waliyoyafanya katika Ikulu ndogo mkoani Kigoma baada ya kupata chakula cha mchana na pia kuzungumza na wananchi kupitia vyombo vya habari, Rais Ndayishimiye alipowasili leo asubuhi kwa ajili ya ziara ya siku moja hapa nchini kufuatia mwaliko aliopewa na Rais Dk. Magufuli.


Baada ya kuwasili na kupokewa na Rais Magufuli, Rais Ndayishimiye aliwasalimia wananchi  waliojitokeza katika mapokezi hayo na kisha wakaenda eneo la Bangwe kufungua Jengo la Kisasa la Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma na baadaye kabla ya kwenda  Ikulu ndogo ya Kigoma ambako walifanya mazungumzo hayo rasmi. 


Rais Magufuli amesema kati ya mwaka 2016 na sasa thamani ya biashara kati ya Tanzania na Burundi imeongezeka kutoka Sh. Bilioni 115.15 hadi kufikia Sh. Bilioni 201, na kwamba lengo ni kuongeza kasi na kiwango cha biashara ili nchi zote mbili zinufaike zaidi.


Amebainisha kuwa kutokana na dhamira hiyo wamekubaliana kuanza mara moja ujenzi wa kipande reli kuanzia Uvinza (Tanzania) – Msongati (Burundi) -  Gitega (Burundi) ambacho baadaye kitaungana na reli ya kati ya kiwango cha kisasa (SGR) ili kurahisisha usafirishaji wa mizigo mbalimbali ikiwemo madini aina ya Nickel ambayo yanapatikana Kabanga nchini Tanzania na Msongati nchini Burundi.


Rais Magufuli amesema, Tanzania pia imechukua hatua madhubuti za kuimarisha biashara na Burundi zikiwemo kuimarisha bandari ya Dar es Salaam na kuanza ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (SGR) itakayotoka Dar es Salaam hadi Kigoma na kuunganishwa hadi Burundi, kuimarisha uwanja wa ndege wa Kigoma, kununua ndege zinazofanya safari zake moja kwa moja hadi Bujumbura na kuimarisha bandari ya Kigoma ili iwe bandari kuu katika Ziwa Tanganyika.


Amesema juhudi nyingine ni kuimarisha barabara, kununua meli mbili mpya, moja ya mizigo yenye uwezo wa kubeba tani 4,000 na nyingine yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 400 na pia kukarabati meli za Mv Liemba na Mv Sangara ambazo amesema zitarahisisha usafirishaji wa mizigo na abiria katika ziwa Tanganyika huku  akimpongeza Rais Ndayishimiye kwa Burundi kufanikiwa kupata mkopo wa Dola milioni 23 za Marekani, kwa ajili ya kujenga Bandari ya Bujumbura.


Kwa upande mwingine, Rais Magufuli amempongeza Rais Ndayishimiye kwa kuimarisha hali ya usalama nchini Burundi na ametoa mwito kwa wakimbizi wa Burundi kurejea nchini kwao ili kuijenga nchi yao ambayo uchumi wake umeanza kukua na wadau mbalimbali wa maendeleo wameanza kurejesha uhusiano na nchi hiyo.


Kwa upande wake Rais Ndayishimiye ambaye ameongozana na Mkewe Mama Angeline, amemshukuru Rais Magufuli kwa kumkaribisha kufanya ziara yake ya kwanza nchini Tanzania na ameeleza kuwa anaiona Tanzania ni nyumbani na kwamba Burundi inaishukuru Tanzania kwa namna inavyoshirikiana nayo wakati wote na hasa kuwapa hifadhi wakimbizi wakati wa kipindi cha machafuko.


Amesema Burundi ipo tayari kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano wake na Tanzania ikiwemo kutumia Bandari ya Dar es Salaam ambayo kwa sasa inapitisha asilimia 95 ya mizigo yote ya Burundi na amempongeza. Rais Magufuli kwa namna alivyoleta mabadiliko nchini Tanzania ukiwemo mji wa Kigoma ambao umeboreshwa sana katika kipindi cha miaka mitamo ya uongozi wake.


Rais Ndayishimiye amesema kwa sasa Burundi ni shwari, Warundi wengi wanarejea nchini humo na kwamba Serikali inawahimiza wananchi kujikita kufanya kazi ili kukuza uchumi na kuijenga Burundi.


Kiongozi huyo wa Burundi ambaye ameingia nchini kwa gari kutoka nchini humo amepokelewa rasmi katika Uwanja wa michezo wa Lake Tanganyika Mjini Kigoma ambapo amepigiwa mizinga 21 na kukagua gwaride rasmi la Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lililoandaliwa kwa heshima yake. Rais Ndayishimiye aliondoka baadaye mchana kurejea nyumbani

author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana