*Ameongoza wizara kwa miaka 20, hakuna mwingine zaidi yake
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema Dkt. Magufuli ni kiongozi anayestahili kupewa nchi kwa sababu ana uwezo wa kuongoza.
“Dkt. Magufuli ana uwezo wa kupewa nchi kwa sababu suala la kupewa nchi siyo la mzaha. Wamejitokeza wengi lakini siku ya kupiga kura ni lazima uwe makini, umpe mtu unayemjua historia yake. Dkt. Magufuli amekuwa Waziri kwa miaka 20. Ameongoza wizara nyeti na kubwa na amekuwa na uwezo wa kuzisimamia na kuleta maendeleo,” alisema.
Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumanne, Septemba 22, 2020) wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wakazi wa kata za Lubuga na Ilungu, wilayani Magu, mkoani Mwanza kwenye mikutano ya kuwanadi wagombea wa CCM iliyofanyika akiwa njiani kuelekea jijini Mwanza.
Mheshimiwa Majaliwa ambaye amemaliza ziara yake mkoani Mara, ameingia Mwanza kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli. Alitumia fursa hiyo kumwombea kura mgombea ubunge wa jimbo la Magu, Bw. Kiswaga Destery na madiwani wengine wa jimbo hilo.
Alisema Dkt. Magufuli anastahili kupewa nchi kwa sababu ana uwezo wa kuisimamia nchi yake na kuongeza: “Tanzania imekosa maendeleo ya haraka kwa sababu kulikuwa na tabia ya watu wachache ya kula rushwa na kuwaathiri wananchi wa chini wasipate mafanikio. Tunataka kiongozi wa nchi anayeweza kupambana na rushwa na mafisadi. Na huyo ndiye kiongozi tunayemtaka.”
Kuhusu uboreshaji kwenye sekta ya afya, Mheshimiwa Majaliwa alisema sera ya tiba kwa mama mjamzito na watoto na wazee ni bure. “Huduma ya mama mjamzito kujifungua ni bure. Tumeleta fedha wilayani Magu, sh. bilioni 10.8 za kuhudumia wote hawa.”
“Tunayo Bima ya Afya na sasa tunataka tuiimarishe ili iwe ya Kitaifa. Na leo tayari tunao muswada wa Bima ya Afya, tunataka tuunganishe wafanyakazi na wananchi wa kawaida ili Watanzania wote wawe na Bima ya Afya.”
Akielezea ni kwa nini bima hiyo inapaswa kusambaa nchi nzima, Mheshimiwa Majaliwa alisema si kila mara mtu anakuwa na pesa taslimu wakati anapopata mgonjwa kwenye familia, na ndiyo maana inasisitizwa Watanzania wote wawe na Bima ya Afya.
“Unapata kadi wewe na mkeo au mumeo, na wategemezi wanne. Leo tuna watoto wanatoka Magu lakini wanasoma Chuo Kikuu cha Dodoma. Una mtoto yuko hapa lakini anasoma Chuo Kikuu Dar es Salaam, una mtoto mwingine anasoma Bwiru. Akiugua huko na kuulizwa kitambulisho, anatambulika kuwa ni mtoto wa fulani, anatibiwa.”
“Haya yote niliyoyasema, yamefanyika katika kipindi cha miaka mitano chini ya uongozi wa Dkt. John Pombe Magufuli na ndiyo sababu leo namuombea kura ili awe Rais wa nchi hii,” alisema.
Akitoa ufafanuzi kuhusu sekta ya afya, Mheshimiwa Majaliwa alisema sh. bilioni 1.4 zimetolewa kwa Wilaya ya Magu kwa ajili ya ujenzi wa vituo vitatu vya afya ambapo kituo cha afya Kahangara kilipata sh. milioni 500 na ujenzi umekamilika, kituo cha afya Lugeye kilipatiwa sh. milioni 500 na ujenzi umekamilika na kituo cha afya Kabila kilipatiwa sh. milioni 400, na ujenzi uko katika hatua za mwisho.
Kuhusu fedha zilizotolewa kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi, Mheshimiwa Majaliwa alisema sh. bilioni 10.1 zimetolewa kwa ununuzi wa dawa na vifaa tiba na kwamba kila mwezi, wilaya hiyo imekuwa ikipokea wastani sh. milioni 108. “Pia kuna magari mawili ya kubebea wagonjwa yaliletwa, moja liko Hospitali ya Wilaya na jingine liko katika kituo cha afya cha Kahangara,” alisema.
Kuhusu ujenzi wa barabara, Mheshimiwa Majaliwa alisema sh. bilioni 10 zimetolewa kupitia TARURA na TANROADS kwa ujenzi, matengenezo ya kawaida, matengenezo ya sehemu korofi na madaraja kwa barabara za Halmashauri ya Wilaya ya Magu ikiwemo ujenzi wa barabara ya lami ya Magu mjini yenye urefu wa km. 5.7 ambayo tayari imekamilika kwa sh. bilioni 2.7.
Alizitaja barabara nyingine kuwa ni ya Kisesa-Bujora yenye urefu wa km. 0.4 kwa kiwango cha lami ambayo imekamilika kwa sh. milioni 360, barabara ya Usagara-Kisesa (km. 16.14) kwa kiwango cha lami, na usanifu wa kina wa barabara ya Magu-Ngudu-Hungumalwa (km. 70). Pia alisema fedha zimetengwa kwa ajili ya usanifu wa kina wa babarara ya Mabuki- Jojiro-Ngudu (km. 28).
Post a Comment