Na Said Mwishehe, Michuzi TV-Geita
MAELFU ya Watanzania katika maeneo mbalimbali nchini na hasa ambako Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Dk.John Magufuli amefanya mikutano yake ya kampeni kuelekea uchaguzi Mkuu wameeleza wazi namna ambavyo wamekuwa wakifurahishwa na utendaji kazi wake katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na sasa wamesema lazima wampe miaka mitano mingine.
Wamesisitiza wanaamini katika miaka mitano ijayo wanatarajia makubwa zaidi kutoka kwa Dk.Magufuli na kupitia ahadi zake zikiwemo zile ambazo ziko kwenye Ilani ya Uchaguzi Mkuu zimeweka wazi mipango ya Serikali anayoingoza iwapo atapata nafasi, hivyo ambacho wao wanasubiri ni Oktoba 28 ifike wakapige kura ambayo itamrudisha madarakani.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti watanzania hao wamefafanua nchi kwa sasa imepiga hatua kubwa chini ya uongozi wa Rais Magufuli na kwa mazingiga hayo hawaoni sababu ya kumpa mwigine kwani katika wagombea wote 15 ambao wanawania nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu hakuna hata mmoja ambaye anafikia robo ya sifa alizonazo mgombea urais kwa tiketi ya CCM.
Wamesema katika kipindi cha miaka mitano wameshuhudia ujenzi wa miradi mikubwa ya maendeleo ya maendeleo kwa ajili ya nchi yetu ya Tanzania na kinacholeta raha zaidi miradi hiyo inatekelezwa kwa fedha za Watanzania wenye na yote hiyo imewezekana kutokana na uongozi safi wa Dk.Magufuli huku wakieleza katika miaka mitano iliyopita Serikali ya Awamu ya Tano imekuwa ni ya vitendo zaidi kuliko maneno.
Shaban Seleman ambaye ni mkazi wa mkoani Singida amesema kwamba Rais Magufuli katika miaa mitano amesaidia sana katika kusimamia na kuboresha huduma za jamii huku akipongeza juhudi ambazo zimefanyika katika ujenzi wa miundombinu katika sekta ya afya ndani ya mkoa huo."Tunachomuahidi Rais wetu tutampigia kura ili arudi tena kuongoza nchi kwa miaka mitano mingine."
Kwa upande wake Asha Jabiri na Sospeter Nduta ambao ni wakati wa mkoa wa Tabora wamesema kuwa Dk.Magufuli katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu wala asiwe na wasiwasi kwani kwa yale ambayo ameyafanya kwa ajili ya wananchi wa mkoa huo atashinda kwa kishindo na kwa sasa wanachokifanya ni kuendelea kuhamasisha siku ya Oktoba 28,mwaka huu kura zote za ndio ziende kwa Dk.Magufuli.
Wamesema mwaka 2015 wakati Rais Magufuli anaingia madarakani , mkoa wa Tabora ulikuwa na changamoto nyingi zikiwemo za uhaba wa maji, uhaba wa madarasa kwa shule za msingi na sekondari, vijiji kukosa umeme na hata kwenye afya nao walikuwa na changamoto ya kukosekana kwa hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati lakini hivi sasa wana hospitali za Wilaya katika wila zote za mkoa huo ,wamejengewa vituo vya afya na zahabati kila mahali.
Wameongeza kutokana na hayo yote ambayo yamefanywa na Rais Magufuli, wanachoweza kukifanya ni kumchagua ili ashinde kwa kishindo kwani wana matarajio na matumani makubwa na yeye kwani kwa sehemu kubwa ametatua changamoto zao na miaka mitano ianayokuja wana uhakika yale ambayo yameanza yatatekelezwa.
Wakati huo huo Josefina Thomas na Daud Maganga ambao ni wakazi wa Mkoa wa Shinyanga wamesema kuwa Rais Magufuli kwenye miaka mitano ya kwanza aliyoyafanya katika mkoa wao hakuna asiyeona , na katika uchaguzi mkuu mwaka huu wamesema wamefurahishwa na mgombea huyo kwani kupitia mikutano yake ya kampeni ndani ya mkoa huo amekuwa akieleza hatua kwa hatua yale ambayo yamefanyika na yatakayokwenda kufanyika baada ya uchaguzi mkuu.
Wamesema utaratibu wa elimu bure kuanzia elimu ya msingi na sekondari, imekuwa faraha kubwa kwa watu wengi wa mkoa huo na nchi kwa ujumla na kwamba ni matumaini yao Dk.Magufuli atakaporudi tena madarakani ataendelea na mfumo wa kutoa elimu bure ili watoto wa masikini waendelee kusoma.
Kwa upande wa wakazi wa Mkoa wa Simiyu pamoja na mambo mengine ya maendeleo ambayo yamefanyika wamemsifu Dk.Magufuli kwa jinsi ambavyo Serikali anayoisimamia ilivyofanikiwa kuboresha huduma za afya, elimu,maji, miundombinu ya babarabara ambazo zinyi zimejengwa kwa kiwango cha lami.
Wamesema kwa hali ya kawaida na yale ambayo Rais Magufuli ameyafanya katika kipindi cha miaka mitano hakukuwa na sababu ya kufanyika Uchaguzi Mkuu zaidi ya kumuapisha tu lakini kwasababu ya uwepo wa Katiba ndio maana wanasubiri tu ifike Oktoba 28 wakampigie kura arudi kuendelea na kazi ya kuijenga nchini.
Wakazi wa Mkoa wa Mwanza ambao wamezungumza na Michuzi TV na Michuzi Blog wamesema ujasiri wa Dk.Magufuli ambao ameuweka na hasa katika kukabiliana na waliokuwa wanaiba rasilimali za nchi hii, ni moja ya sifa ambayo wanaona inatosha kumpa miaka mitano mingine.Pia wamesema katika usafiri wa meli , Rais Magufuli amewatendea haki wananchi wa mkoa huo pamoja na mikoa inayozunguka Ziwa Victoria kwani wayanayofanya katika kuboresha na kuimarisha usafiri katika Ziwa Victoria wote ni mashahidi.
Wamesema wanachosubiri ni siku ya uchaguzi ifike ili wakamchague tena kwa ajili ya kuendelea na miradi mingine ya maendeleo huku miongoni mwa miradi ambayo wanatamani kuona inamalizika ni ule wa ujenzi wa daraja lenye urefu wa kilometa 3.2 la Kigongo-Busisi ambalo litagharimu Sh.bilioni 700.
Kwa upande wa wananchi wa Mkoa wa Geita wao wamesema katika mkoa huo kuna maendeleo makubwa ambayo yamefanywa na Rais Magufuli katika miaka mitano katika nyanja mbalimbali, lakini kikubwa ambacho kimewafurahisha ni jinsi ambavyo Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM inavyofafanua kuhusu mipango iliyopo katika sekta ya uchimbaji madini na hasa kwa wachimbaji wadogo ambao wanakwenda kupata fursa zaidi ya kuwekewa mazingira mazuri zaidi ya kuchimba madini ya dhahabu.
Pia wamesema kingine ambacho kimewafurahisha kwa Dk.Magufuli katika miaka mitano ya kwanza ni kusimama imara katika kujenga nchini na leo hii Tanzania imefikia uchumi na hivyo matarajio yao ni kwamba miaka mitano ijayo nchi yetu itapiga hatua zaidi.
Kwa kukumbusha tu hadi sasa Dk.Magufuli ameshafanya mikutano ya kampeni katika mikoa nane ambayo ni Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, Simiyu, Mara, Mwanza na Geita ambako amefanya mikutano juzi na jana .Mikutano yake imekuwa ikihudhuriwa na maelfu ya Watanzania ambao wana matumaini makubwa na yeye na kote wamekuwa wakimhakikisha kumpa kura ambazo zitamuwezesha kushinda kwa kishindo.
Post a Comment