Na Scolastica Msewa, Kibiti.
Katibu wa CCM wilaya ya Kibiti mkoani Pwani Muhidini Zakaria amewataka wananchi wa Kata ya Rualuke tarafa ya Kikale Wilayani hapa wasifanye makosa tena ya kuchagua diwani wa upinzani badala yake wachague mgombea wa CCM katika nafasi hiyo ili watekelezewe miradi yao ya maendeleo kwa wakati.
Amesema hayo katika mkutano wa kampeni za Uchaguzi mkuu katika kijiji cha Nyamatanga wakati akiwanadi Wagombea wa CCM kuanzia ngazi ya Urais, Ubunge na Udiwani.
Amesema katika miaka mitano iliyopita kata hiyo walichagua Diwani wa chama cha CUF ambaye alikuwa peke yake katika maamuzi ya mikutano ya Baraza la madiwani ilimuwia ngumu kupitishiwa miradi ya maendeleo na kusababisha kuchelewa kukamilishwa kwa kituo cha afya cha kata ya Rualuke.
Zakaria amesema iwapo mwaka huu wakichagua Diwani wa CCM kituo hicho cha afya kitakamilishwa na huduma zitaanza kutolewa.
Amefafanua kuwa kwenye vikao vya maamuzi sifa ya kiongozi kutoka upinzani ni kupinga kila kinachotolewa maamuzi hata kama kina tija kwa jamii yake.
Naye mgombea Ubunge wa Jimbo la Kibiti Twaha Mpembenwe katika mkutano huo amesema zaidi ya sh. mibioni 290 zimetolewa kwa mikopo ya kinamama, vijana na wanaoishi na ulemavu katika halmashauri ya wilaya ya kibiti hivyo wananchi hao wachague CCM kwa maendeleo yao.
Mpembenwe amesema watakapo mchagua kuwa mbunge wao atasimamia na kuongeza vyanzo vya ukusanyaji wa mapato ili kuongeza asilimia 10 inayotolewa kwa ajili ya mikopo ya akinamama, vijana na walemavu ili mikopo hiyo iwe ya tija zaidi.
Post a Comment