Na Mwandishi Maalum, Mwanza
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk. Bashiru Ally amezindua mafunzo ya mawakala wa CCM katika Uchaguzi Mkuu mkoa wa Mwanza na kueleza kuwa, mafunzo hayo sasa yanaendelea nchi nzima.
Uzinduzi huo ulifanyika jana, Ijumaa,Oktoba 16, 2020 katika Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza.
"Nimeamua kuja Mwanza kufanya kazi ya kuzindua mafunzo kwa viongozi wa Chama na mawakala wa uchaguzi kwa niaba ya Chama kwa sababu za kimkakati, Kwanza, tumeshakubaliana na Mwenyekiti wa Mkoa kwamba hakuna jimbo lolote la mkoa huu litakalotoka mikononi mwa CCM ", alisema Dk. Bashiru
Baadaye Katibu Mkuu, alishiriki ibada ya Ijumaa katika msikiti wa Mkoa wa Mwanza, ambapo alitumia fursa hiyo kutoa shukrani kutoka kwa Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. John Magufuli, kwa viongozi wa dini zote nchini kuendelea kuhimiza amani na mshikamano bila kuchoka wakati wote hasa wakati huu wa kampeni za uchaguzi Mkuu hadi siku ya uchaguzi mkuu wenyewe utakaofanyika siku ya Jumatano, Oktoba 28, mwaka huu na pia baada ya uchaguzi huo.
Said Said Nguya ambaye ni Afisa Habari katika Ofisi ya Katibu Mkuu wa CCM amesema Dk. Bashiru ambaye pia ni mlezi wa mkoa wa Mwanza , atakuwa mkoani hapa katika ziara hiyo ambayo ni ya siku nne na leo alitarajiwa kuwa katika Wilaya ya Nyamagana.
Post a Comment