Featured

    Featured Posts

DK. BASHIRU: CCM ITAPATA USHINDI MNONO AMBAO HAUJAPATA KUTOKEA TANGU KUWEPO MFUMO WA VYAMA VINGI TANZANIA

Katibu Mkuu wa CCM Dk. Bashiru Ally akizungumza na Waandishi wa habari baada ya mazungumzo yake na Balozi wa Kenya hapa nchini Dan Kazungu (aliyevaa barakoa).


Na Juma Issihaka


KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk. Bashiru Ally, amesema ubora wa wagombea na Ilani ya CCM ya Uchaguzi ya mwaka 2020, ndio mambo yanayokibeba Chama kuelekea safari ya ushindi wa kishindo katika uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.


Amesema matarajio ya Chama hicho, ni kupata ushindi mnono na wa kihistoria zaidi ya ilivyowahi kutokea tangu kuanza kwa mfumo wa siasa za vyama vingi nchini, hiyo ni kutokana na udhaifu wa vyama vya upinzani.


Hayo aliyasema jana baada ya mazungumzo na Balozi wa Marekani Dk. Donald Wright, yaliyofanyika Ofisi ndogo ya CCM iliyopo Lumumba, jijini Dar es Salaam.


Alisema ushindi wa Chama hicho, unabebwa na ubora wa wagombea wake na Ilani ya uchaguzi yenye ahadi nyingi na zinazotekelezeka.


“Ushindi wa CCM unatokana na ubora wa wagombea wake na Ilani bora yenye ahadi nzuri na zinazotekelezeka, hakuna mambo mengine zaidi,” alisema.


Alisema wanayo matarajio ya ushindi zaidi wa chama hicho kuliko ilivyowahi kutokea tangu kuanza kwa mfumo wa siasa za vyama vingi, hiyo ni kutokana na udhaifu wa vyama vya upinzani katika uchaguzi wa mwaka huu.


“Mwaka huu tunashindana na vyama dhaifu sana na vingine vipya kabisa, kuna chama kilikuwa na Mbunge mmoja, sasa kimesimamisha mgombea Urais ambaye hajulikani alipo hadi leo, mimi ningekuwa ndiye Katibu Mkuu wa chama hicho ningemshitaki.


“Vyama hivi angalau vilikuwa na nguvu kwenye uchaguzi wa mwaka 2015 na hiyo ilitoka na kuwa na washauri wazuri ambao ni Mzee Edward Lowassa na Fredrick Sumaye ambao kwa sasa wote wapo CCM wanafanya kampeni za wagombea,” alisema.


Dk. Bashiru, aliongeza kuwa mambo mengine yanayosafisha njia ya ushindi wa CCM, kwenye uchaguzi wa mwaka huu ni ukweli kwamba, kumekuwa na mshikamano mkubwa baina ya wanachama ambao umetokana na kuendeshwa kwa mchakato wa kura za maoni wenye haki, uwazi na usawa.


Pia Dk. Bashiru, alifafanua ratiba ya kampeni ya Rais Dk. John Magufuli, kwamba baada ya kumaliza Dar es Salaam, ataelekea Pwani kisha mikoa ya Kaskazini, kwamba baadhi ya mikoa imeshafikiwa na viongozi wengine wa chama hicho akiwemo Mgombea mwenza Mama Samia Suluhu Hassan na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM taifa, Kassim Majaliwa.

author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana