Dodoma Tanzania
Rais Mteule wa Tanzania ambaye ni Rais aliyemaliza mhula wake wa kwanza , Dk. John Magufuli amesema ushindi alioupata ni deni kubwa kwa analostahili kulilipa kwa Watanzania na kuwashukuru wagombea wa vyama vya upinzani akisema, upinzani umesaidia kufahamu wanachotaka Watanzania.
''Nawashukuru pia na kuwapongeza kwa kukubali matokeo na kuja kushiriki hafla hii. Hii ni ishara ya kukomaa kwenu kisiasa - hongereni sana. Uchaguzi umeisha sasa ni wakati wa kufanya kazi, siasa sio vita, chuki wala ugomvi sisi sote ni Watanzania, napenda kuwaahidi nitashirikiana nanyi katika kuhakikisha tunasukuma mbele gurudumu la maendeleo ya nchi yetu. Tanzania kwanza mambo mengine baadae" Magufuli amesema.
Ni kweli kwamba wananchi wametupatia ushindi mkubwa sana, lakini hiyo haiwezi kuwa sababu ya kudharau maoni na ushauri wenu''. amesema Dk. Magufuli.
Rk. Magufuli amesema hayo, baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage kuwakabidhi yeye na Makamu wake Samia Suluhu Hassan vyeti kufuatia ushindi alioupata katika matokeo ya Uchaguzi Mkuu uliofanyika hapa nchini Oktoba 28, mwaka huu
Dk. Magufuli amewashukuru Watanzania kwa kukipa ushindi chama chake cha Mapinduzi (CCM) katika nafasi ya Urais, Ubunge na kule Zanzibar katika nafasi ya uwakilishi na nafasi ya Udiwani.
''Kupata asilimia 84.4 ni imani kubwa sana kwa Watanzania na nasema kwa dhati nina deni kubwa sana kwa Watanzania, imani yao nitaitimiza kwa kufanya kazi sana usiku na mchana'', Dk. Magufuli amesema.
Dk. Magufuli amewashukuru pia viongozi wa dini ambao kwa kipindi chote cha uchaguzi waliweza kuwaongoza kwa dua na sala na hatimae kumaliza uchaguzi kwa usalama na taifa lao kuendelea kubaki kwa amani.
''Navishukuru pia vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kwa kufanya kazi kwa weledi mkubwa na kuhakikisha amani na usalama vinatawala katika kipindi chote cha uchaguzi,'' amesema Bwana Magufuli huku akielezea matumaini yake kuwa usalama utaendelea hata baada ya uchaguzi.
"Uchaguzi umeisha sasa ni wakati wa kufanya kazi, siasa sio vita, chuki wala ugomvi sisi sote ni Watanzania, napenda kuwaahidi nitashirikiana nanyi katika kuhakikisha tunasukuma mbele gurudumu la maendeleo ya nchi yetu. Tanzania kwanza mambo mengine baadae" Magufuli amesema huku akiwashukuru viongozi wa nchi nyingine waliomtumia salamu za pongezi.
Post a Comment