Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU imefanya mawasilino na Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), ili kuchunguza ushiriki wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Wallace Karia katika kashfa ya ubadhilifu wa fedha iliyomuweka hatiani aliyekua Rais wa CAF Ahmad Ahmad.
Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) Jumatatu (Novemba 23), ilimfungia miaka mitano Ahmad Ahmad kutojihusisha na masuala ya soka kutokana na kashfa ya ubadhilifu.
Taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zinadai kuwa, Rais wa TFF Wallace Karia huenda akawa miongoni mwa wanufaika kwa kupata mgao wa dola 20,000, kutoka kwa Ahmad Ahmad.
“Tumewasiliana na CAF, tumeanza uchunguzi, unajua hili suala ni jipya na ndio kwanza tumeanza uchunguzi, siwezi kuahidi itachukua muda gani, lazima kila hatua izingatiwe kwenye uchunguzi huu ili kama Wallace Karia amehusika na wote walionufaika na ubadhirifu huo waweze kubainika na kuchukuliwa hatua za kisheria” Brigedia John Mbungo Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU.
Hata hivyo tayari Shirikisho la soka nchini TFF limekanusha madai ya kuhusishwa kwa Rais wao Wallace Karia katika kashfa hiyo kwa kuandika barua iliyosambazwa kwenye vyombo vya habari
.
Post a Comment