CCM Blog, Temeke, Dsm.
Wakazi wa jiji la Dar es Salaam na Watanzania wote bila kubagua dini au itikadi za kisiasa wameombwa kufika kwa wingi kwenye uzinduzi wa Kitabu cha 'ufahamu ulioanzia Tanzania kwenda katika maataifa mengine' ili kusikia na kuupokea upendeleo ambao Mungu Baba ameipa Tanzania na kung'ara katika kila jambo ikiwemo kuwa na amani, utulivu na uchumi wake kukua kwa kasi ya kushangaza.
Uzinduzi huo Ulioandaliwa na Kanisa Halisi la Mungu Baba la Tegeta jijini Dar es Salaam, utafanyika kesho katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, na unatarajiwa kuhudhuriwa na maelfu ya watu walioalikwa kutoka mikoa mbalimbali na kutoka nchi zaidi ya sita, ikiwemo Congo DRC, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Msumbiji.
Akizungumza leo kwenye Uwanja huo wa Uhuru, baada ya kukagua maandalizi ya mwisho ya Uzinduzi huo, Kiongozi Mkuu wa Kanisa hilo anayetambuliwa kwa jina la Baba wa Uzao amesema, Maandalizi yote yamekamilika na karibu Makuhani wote kutoka mikoani na waalikwa wa kutoka katika nchi jirani wameshawasili mbali na wale wa kutoka Burundi ambao wanatarajiwa kuwasili kesho mapema.
"Kwa kweli tunatarajia hata viongozi mashuhuri wa kitaifa, wakiwemo wabunge watafika kwenye uzinduzi huu, maana hadi ninavyoongea hii leo, woote tuliowapa mwaliko au njia nyingine hakuna hata mmoja aliyetujulisha kuwa hatakuja', amesema Baba wa Uzao kujibuswali la mwandishi aliyetaka kujua ni viongozi gani watakaohudhuria.
"Ndugu wakazi wa Dar es Salaam, nataka mjue kwanza kuwa uzinduzi huu, siyo kwa ajili ya kushindana na yeyote, wala siyo tamasha, au 'Crusade' au Kanisa letu 'kujimwambafai', bali kuna mambo makuu manne ambayo natamani Watanzania wayajue, ikiwemo kuwafahamisha kwa neema hii inayoipata Tanzania hadi kuvuma duniani katika kufanikiwa kwenye mambo mengi ikiwemo kundokana na janga la Corona ambalo bado linayasumbua mataifa mengi, ni kwa sababu Mungu Baba amelipa Taifa hili upendeleo wa makusudi", amesema Baba wa Uzao.
Amesema, kutokana na upendeleo huo wa Mungu Baba kwa Tanzania ndiyo sababu Mataifa mengi Duniani sasa yanaitazama nchi Tanzania kwa namna ya kustaajabishwa kiasi kwamba wengine kuamua kuja, ili kushuhudia ufahamu huu ulioanzia katika taifa hili.
Baba wa Uzao amesema, Uzinduzi utaanza saa nane mchana na kumalizika saa kumi jioni, lakini milango ya Uwanja wa taifa itakuwa wazi kuanzia saa mbili asubuhi ili kila atakayehitaji kuwahi nafasi nzuri itakayomwezesha kuhsuhudia vyema kila hatua itakayofanyika kwenye uzinduzi huo asikwazike.
Kuhusu hali ya usalama, Baba wa Uzao amesema Kanisa Halisi katikia maandalizi yake jambo hilo ililipa kipaumbele, hivyo usalama utakuwepo wa kutosha kwa kuwa vyombo vinavyohusika kusimamia ulinzi na usalama vimeshaahidi kulipa kanisa hilo ushirikiano mkubwa mwanzo hadi mwisho wa shughuli hiyo.
Post a Comment