.
CCM Blog, Dar es Salaam
Rais Dk. John Magufuli ameahirisha maadhimisho 59 ya sherehe za Uhuru wa Tanzania Bara zilizotarajiwa kufanyika Desemba 9, mwaka huu, na kuagiza fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kugharamia sherehe hizo zitumike kununulia vifaa mbalimbali kwa ajili ya Hospitali ya Uhuru.
Taarifa iliyotolewa leo, Desemba 3, 2020 na Ofisi ya Waziri Mkuu imesema Rais ameagiza kiasi cha zaidi ya Sh milioni 835 (sh. 835,498,700) zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kufanikisha sherehe za maadhimisho hayo zitumike kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya hospitali hiyo.
Taarifa hiyo imesema Waziri Mkuu Kassi8m Majaliwa ametoa taarifa hiyo kwenye sherehe za kuadhimisha miaka 60 ya kuanzishwa kwa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) zilizofanyika katika hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam. Amesema Rais Dkt. Magufuli ameagiza siku hiyo itumike kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali za kijamii nchini.
Novemba 20, 2018, Rais Dk. Magufuli aliagiza kiasi cha sh. 995,182,000.00 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya maadhimisho ya 57 ya Uhuru wa Tanzania Bara tarehe 9 Desemba, zitumike kujenga Hospitali ya Uhuru, ambayo kwa sasa ujenzi wake umefikia asilimia 92.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya 59 ya Uhuru wa Tanzania Bara kwa mwaka huu inasema; ‘Miaka 59 ya Uhuru na Miaka 58 ya Jamhuri: Tanzania yenye Uchumi Imara Itajengwa na Watanzania Wenyewe, Tufanye Kazi kwa Bidii, Uwajibikaji na Uadilifu.’
Waziri Mkuu amesema hadi kufikia sasa ujenzi wa hospitali hiyo ya Uhuru umegharimu shilingi bilioni 4.2. Januari 2019 wakati akipokea gawio la hisa za kampuni ya Simu ya Airtel Rais Dkt. Magufuli aliagiza kiasi cha shilingi 2,415,151,650.00 zilizotolewa na kampuni hiyo zitumike katika ujenzi wa hospitali hiyo.
Post a Comment