Mtafiti kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Juvinary John akiwaelezea waandishi wa habari jijini Dodoma Desemba 4,2020, kuhusu utafiti wa Rushwa ya Ngono katika Taasisi za Elimu ya Juu nchini.
Baadhi ya mambo aliyoyaeleza yaliyomo kwenye utafiti huo ni;
Matokeo yanaonesha zaidi ya 50% ya wahojiwa (wenye uelewa) walieleza uwepo wa rushwa ya ngono katika vyuo vikuu vilivyofanyiwa utafiti. Matokeo haya yanamaanisha kwamba rushwa ya ngono ni tatizo katika vyuo vikuu hivi.
Matokeo haya yanathibitishwa na taarifa za kitaamuli (Qualitative data) ambapo wahojiwa walionesha uelewa na uwepo wa rushwa ya ngono katika vyuo vikuu vilivyofikiwa katika utafiti huu. Baadhi ya wahojiwa walieleza yafuatayo:
“……rushwa ya ngono ni pale ambapo mtu anahitaji huduma fulani lakini hapewi na aliye na nafasi ya kumpa huduma hiyo kwa kumtaka kutoa ngono ndipo apate huduma husika….” “……rushwa ya ngono kuwa ni kitendo cha mwenye mamlaka kulazimisha ngono ndipo atoe haki……”
“…rushwa ya ngono ni mtu kutumia nafasi yake ya kimadaraka ili kujinufaisha kingono…."
“………. rushwa ya ngono ipo na kwa sasa hali ni tete …mtu akijitokeza kufuatilia rushwa ya ngono anakuwa amejiingiza katika hatari kubwa hata kutishiwa maisha ……ni sawasawa na kupambana na madawa ya kulevya….”
“……. Mwalimu alimtongoza mwanafunzi wa kigeni katika programu ya postgraduate, wakati wanafanya majadiliano ya Tasnifu (dessertation) yake, mwalimu alianza kumshikashika, mwanafunzi alipiga kelele baada ya taarifa kuenea mwalimu huyo alipelekwa mafichoni kwa muda wa miaka mitatu na baadaye kurudishwa chuoni hapo.” Kutokana na taarifa za kitakwimu na kitaamuli, dhana ya rushwa ya ngono katika vyuo vikuu inaeleweka na kwamba tatizo la rushwa ya ngono lipo katika vyuo vikuu na linatakiwa kuwekewa mkakati wa kulidhibiti. Matokeo ya utafiti huu yanashabihiana na utafiti uliowahi kufanywa na Mukama (2017) kuhusu mapambano dhidi ya rushwa ya ngono kwa wanafunzi wa Taasisi za elimu ya juu nchini Tanzania.
Katika utafiti wake alibaini kuwa kuna rushwa ya ngono katika Taasisi za elimu ya juu na kwamba waathirika wakuu ni wanafunzi wa kike. Aidha, watafiti walitajiwa majina ya watu wanaotuhumiwa kujihusisha na vitendo vya rushwa ya ngono, hata hivyo kutokana na maadili ya utafiti majina hayo yamehifadhiwa. Matokeo haya yanadhihirisha kukiukwa kwa kifungu cha 25 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11/2007 kulikofanywa na baadhi ya watu wenye mamlaka katika vyuo hivi.
Hivyo, ni muhimu kutafuta vyanzo/sababu za kuwepo kwa vitendo vya rushwa ya ngono, kuchunguza mifumo iliyopo ya udhibiti ili kupima ufanisi wake na kubaini mbinu zinazotumika kuendeleza vitendo vya rushwa ya ngono katika vyuo hivi.
Kwa kufanya hivyo kutasaidia kuweka mikakati ya kudhibiti na kuondoa athari zitokanazo na rushwa ya ngono. Kuna athari nyingi zinazotokana na rushwa ya ngono katika taasisi za elimu ya juu zikiwemo: vyuo kuzalisha watendaji wenye uwezo mdogo kifikra; kuathiri utendaji wa taasisi;
kudhalilisha utu wa mtu na kusababisha mtu kushindwa kujiamini; kuathiri saikolojia ya waathiriwa wa vitendo vya rushwa ya ngono; magonjwa ya kuambukiza kama UKIMWI; mimba zisizotarajiwa; kushusha morali ya utendaji kazi kwa watumishi; upendeleo kwa baadhi ya wanafunzi wanaotoa rushwa ya ngono; kuporomoka kwa maadili ya wanafunzi, wahadhiri na watumishi wasio wahadhiri na kuharibu taswira ya vyuo ndani na nje ya nchi. Kwa upande mwingine, Mukama (2017) katika utafiti wake ameeleza kuwa rushwa ya ngono huvunja heshima ya mtu binafsi na Taasisi.
4.3 Sababu za kuwepo vitendo vya rushwa ya ngono Kwa mujibu wa modeli ya Klitgaard (1998), rushwa hushamiri katika mazingira ya ukiritimba, uhuru wa kufanya maamuzi usiodhibitiwa na mahali ambapo hakuna uwazi na uwajibikaji.
Kwa kuzingatia modeli hii, utafiti ulitaka kujua sababu zinazochochea rushwa ya ngono katika vyuo vikuu kwa kuwataka wahojiwa kueleza chanzo cha kuwepo vitendo vya rushwa ya ngono.
Matokeo yanashabihiana kwa vyuo vyote viwili vilivyotafitiwa. Aidha, kwa mujibu wa matokeo ya kitakwimu matokeo yanaonesha kuwepo kwa sababu tano ambazo ni ukosefu wa maadili, ushawishi wa mtu mwenye mamlaka, mfumo wa utoaji taarifa kutokuwa rafiki, mifumo dhaifu ya kushughulikia rushwa ya ngono na mamlaka ya kutoa alama za mitihani kuachwa chini ya walimu pekee
Afisa Uhusiano wa Takukuru, Doreen Kapwani akielezea umuhimu wa wanahabari kuandika kwa ufasaha bila kupotosha habari kuhusu Utafiti wa Rushwa ya Ngono uliofanywa na taasisi hiyo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Dodoma. PICHA ZOTE NA RICHARD MWAIKENDA
Ofisa kutoka Kurugenzi ya Uzuiaji Rushwa ya Takukuru, Sabina Seja akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Mtafiti Juvinary John kuwasilisha katika mkutano na wanahabari kuhusu Utafiti wa Rushwa ya Ngono kwa Taasisi za Elimu ya Juu jijini Dodoma Desemba 4, 2020.
Baadhi ya wanahabari kutoka vyombo mbalimbali vya habari wakiwa katika mkutano huo uliofanyika African Dream, jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk. Ombeni Msuya akielezea mikakati mbalimbali iliyowekwa chuoni hapo kupambana na Rushwa ya Ngono.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma ya Jinsia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Lulu Mahai akielezea mikakati mbalimbali iliyowekwa chuoni hapo kupambana na Rushwa ya Ngono.
Wanahabari wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Takukuru na baadhi ya watafiti wa Rushwa ya Ngono kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Chuo Kikuu cha Dodoma.
Post a Comment