Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Philip Mpango amelitaka baraza la wafanyakazi Wizara hiyo kufanyakazi kwa kufuata misingi yao na hatasita kumchukulia hatua mtumishi atakayebainika kukiuka misingi na kutoa siri na taarifa nyeti za serikali.
Dkt. Mpango ameyabainisha hayo leo Januari 25,2021 Jijini Dodoma wakati alipokuwa akifungua mkutano wa baraza kuu la wafanyakazi wa wizara hiyo amesema mtumishi yeyote atakayekiuka taratibu na miongozo hatavumilika.
“Natanguliza onyo kali kwa mtumishi yeyote atakayebainika kukiuka taratibu ,miongozo na miiko ya kazi yake ndani ya Wizara ya Fedha na Mipango utajutia ukaidi wake” amesema Dkt Mpango.
Aidha amesema wafanyakazi hao kuwa wana majukumu makubwa katika mstakabali wa Taifa hasa wakati huu wa kutekeleza bajeti ya serikali katika majukumu yake.
“Hii ina maana tunaowajibu wa kuongeza tija na ufanisi katika kutekeleza majukumu yetu na naamini kuwa mtatumia mkutano huu kutathimini utendaji kazi,” amesema.
Pia ametaka viongozi hao kuwa na utaratibu wa kuwasikiliza watumishi ili kupunguza au kuondoa malalamiko na manung’uniko ya wafanyakazi pindi wanapokuwa kazini ili wafanyekazi kwa utulivu kufikia malengo.
Ameongeza kuwa “Lazima tutambue na kukubali kuwa ufanisi sehemu ya kazi hutegemea uhusiano uliopo baini ya viongozi na wafanyakazi ,hivyo basi nawaasa viongozi wenzangu tufanye kila tuwezalo kujenga uhusiano mzuri” amesema.
Awali Mwenyekiti wa Baraza la wafanyakazi wa Wizara fedha na mipango, bwana Doto James amesema mkutano huo utakuwa pamoja na mambo mengine watachagua viongozi wapya pamoja na kujadiliana mambo mbalimbali kuboresha utendaji kazi.
Post a Comment