Uganda imeikosoa vikali Marekani kwa kuingilia masuala ya ndani ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki.
Msemaji wa serikali ya Uganda, Ofwono Opondo amesema Marekani inajaribu kudunisha na kudhalilisha mchakato wa uchaguzi wa urais wa wiki iliyopita.
Hii ni baada ya Balozi wa Marekani mjini Kampala, Natalie E Brown kujaribu kumtembelea kinara wa upinzani aliyeshindwa katika uchaguzi huo, Robert Kyangulani maarufu kama Bobi Wine katika makazi yake.
Hata hivyo mwanadiplomasia huyo wa Marekani nchini Uganda alizuiwa na maafisa usalama kuingia katika makazi hayo ya Wine viungani mwa mji mkuu.
Msemaji wa serikali ya Uganda amesisitiza kuwa, "alichojaribu kufanya Brown ni kuingilia wazi mambo ya ndani ya Uganda, na hususan uchaguzi wetu. Anajaribu kudunisha uchaguzi na matakwa ya wananchi. Hana biashara yoyote ya kumzuru Wine ambaye yuko katika kifungo cha nyumbani."
Opondo amesema balozi huyo wa Marekani mjini Kampala hapaswi kufanya jambo lolote linalokwenda kinyume na taratibu na majukumu yake ya kidiplomasia.
Siku ya Jumamosi, Tume ya Uchaguzi Uganda ilimtangaza rasmi Yoweri Museveni kuwa mshindi wa uchaguzi wa Alkhamisi ya Januari 14, kwa kura milioni 5.85 sawa na asilimia 58.64 ya kura zote wakati mpinzani wake wa karibu, Bobi Wine akipata kura milioni 3.48 sawa na asilimia 34.83 ya kura zote.
Post a Comment