Katibu wa Halmshauri Kuu ya Taifa Organaizesheni na Mjumbe wa Kamati Kuu ndugu Pereira A. Silima Jumapili 21/2/2021 amemwakilisha Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi kwenye sherehe za Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW) yaliyofanyika Chuo Kikuu cha Kiislam Morogoro.
Katibu alipowasili Chuo Kikuu cha Kiislaam alipokelewa na uongozi wa Chuo cha Kiislam pamoja na Viongozi Chama na Serikali wa Mkoa na Wilaya ya Morogoro. Baadae aliweka saini vitabu vya wageni na kupokea taarifa fupi ya shughuli ya Maulid itakavyo endeshwa kutoka kwa Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Prof Mussa Assad.
Baadae alishiriki katika shughuli ya Maulid ambayo yalisomwa na wanafunzi pamoja na kusikiliza mada mbali mbali zinazohusu uislamu zilizotolewa na baadhi ya Masheikh walioshiriki. Lengo kuu la mada zote ni kujitambua kwenye uislamu kwa kufuata Quran Tukufu na Sunna za Mtume Muhammad SAW.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa Organaizesheni na Mjumbe wa Kamati Kuu kwenye nasaha zake alizozitoa kwa niaba ya Katibu Mkuu wa CCM, amewashukuru kwa kumualika. Katibu alisema jambo lililofanyika ni zuri na lenye faida kwenye maisha ya kila siku na ameshauri kwamba Maulid ni muhimu yaendelee kwani ni muhimu kwa taasisi kubwa kama MUM. Amewakumbusha wanafunzi wote wanaochukua taaluma mbalimbali zenye lengo la kuwasaidia wao kwenye maisha yao lakini lazima kuwasaidia wenzao ambao hawakupata fursa za kifikia viwango hivyo vya elimu.
Katibu aliwakumbusha washiriki wote kuzingatia maadili hasa ya watoto ambao ndio wanaanza misingi ya maisha yao je wanazingatia maadili aliyotufundisha Mtume SAW. Aidha, aliwasihi na kuwataka kuwa na huruma kwa watu wenye shida mbalimbali. Mgeni rasmi aliwakumbusha washiriki wote kuchukua tahadhari kutokana na ugonjwa uliopo nchini na kuwataka warudi kwenye Qurani na sunna za Mtume Muhammad SAW sambamba na kuwakumbusha kutenda mema na kuacha mabaya hasa katika mwezi huu wa Rajab.
Katibu kabla ya kushiriki kwenye Maulid aliwatembelea wanachama wa CCM wa Tawi la Chuo Kikuu cha Kiislaam ambapo alipokea taarifa ya Tawi na kukabidhi kadi za uanachama wa CCM kwa baadhi ya wanachama kwa niaba wenzao. Katika salamu zake aliwapongeza kwa kushiriki na kushinda uchaguzi Mkuu wa Madiwani, Wabunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa mwaka 2020.
Imeandaliwa na Ofisi ya
Katibu wa NEC Organaizesheni.
Post a Comment