Featured

    Featured Posts

MAALIM SEIF HAMAD AFARIKI DUNIA LEO, PATA HISTORIA YAKE TANGU 1943 ALIPOZALIWA

Maalim Seif Sharif Hamad


Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad amefariki Dunia, jijini Dar es Salaam.


Akitangaza kifo hicho, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi amesema, Maalif Seif amefariki leo saa 5 asubuhu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikokuwa amelazwa tangu tarehe 9 mwezi huu akipatiwa matibabu.


Kufuatia kifo hicho Rais Dk. Mwinyi ametangaza siku saba za maombolezo, akisema pia kwamba taratibu za mazishi zitatolewa na Uongozi wa Chama cha ACT Wazalendo. 


Maalim Seif pamoja na kuwa Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo pia alifanikiwa kuwa Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar baada ya kugombea Urais wa Zanzibar kupitia chama hicho katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba mwaka jana.


Kufuatia kifo hicho Rais Dk. John Magufuli ameelezea kushtushwa na kuandika katika mtandao wa Twitter  akisema; 👇


Historia fupi ya Maalim Seif Sharif Hamad

Maisha

Maalim Seif Shariff Hamad alizaliwa eneo la Nyali, Mtambwe Kisiwani Pemba, Oktoba 22, 1943

Alipata elimu yake ya msingi katika skuli ya msingi Uondwe, 1950 na baadaye alijiunga na elimu ya sekondari katika skuli ya watoto wa kiume Wete Pemba 1952. 

Baadaye aliendelea na elimu ya sekondari katika skuli ya King George na kuhitimu kidato cha sita mwaka 1963 ambapo baadaye kati ya mwaka 1972 na 1975 alihitimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kutunukiwa shahada ya kwanza ya Sayansi ya Siasa (Political Science).


Kazi

Kati ya mwaka 1972 na 1975 alifundisha katika skuli mbalimbali za Unguja na Pemba, zikiwemo Fidel Castro na Lumumba.

Siasa

Baadaye Maalim Seif alianza kuingia katika masuala ya siasa, ambapo mwaka 1977 aliteuliwa kuwa Waziri wa Elimu na Utamaduni na Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi.

Mwaka 1977 hadi 1987, alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM na kuwa Mjumbe wa Kamati kuu ya chama hicho.

Mwaka 1982 hadi 1987 alikuwa Mkuu wa Idara ya Uchumi na Mipango ya Chama cha Mapinduzi na 1984 aliteuliwa kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hadi mwaka 1988.

Baada hapo, misukosuko mikubwa ya kisiasa ilianza kumkumba ambapo Januari 1988 alipoteza nafasi ya Uwaziri Kiongozi na Ujumbe wa Baraza la Wawakilishi baada ya aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Idrisa Abdulwakil kutangaza kulivunja Baraza la Mawaziri.

Kujiengua na CCM na kujiunga na upinzani

Mnamo Mei 1988, Maalim Seif alitoka katika chama cha CCM. 

Mwaka 1992, Maalim Seif alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama cha Upinzani cha Civic United Front (CUF)  na kuwa Katibu Mkuu wa Chama hicho kwa muda mrefu hadi alipoondoka kuhamia ACT- Wazalendo 2019.

Tarehe 18 Machi 2019 alitangaza kujiunga na chama cha ACT Wazalendo: maamuzi hayo yalifanywa muda mchache baada ya kesi iliyokuwa Mahakamani kuishia kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa ndiye Mwenyekiti halali wa chama cha CUF.

Maali  Seif alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, nafasi aliyopewa Kando ya Kiongozi wa Kitaifa Zitto Kabwe na akiwa Mwenyekiti wa chama hicho, aligombea Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama hicho katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba mwaka jana.


Hatua hiyo ya kugombea Urais wa zanzibar kupitia ACT Wazalendo ndiyo hatua iliyomwezesha kuwa Makamu wa kwanza wa Rais kufuatia Chama hicho kuwa cha pili kwa wingi wa kura baada ya CCM iliyoshinda kiti cha Urais wa Zanzibar.


Ina Lilah waina Ilayhi Rajiuun

Imetayarishwa na Bashir Nkoromo, Msimamizi Mkuu wa Blog hii ya Taifa ya CCM.
author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana