Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipokabidhi magari mawili aina Toyota Land Cruiser moja kwa ajili ya Kituo cha Polisi cha Mtama katika Halmashauri ya Mtama na jingine kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi. Makabidhiano ya magari hayo yalifanyika kwenye viwanja vya Kituo cha Polisi cha Mtama, Februari 21, 2021.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi, Mbunge wa Mtama Nape Nnauye ufunguo wa gari aina ya Toyota Land Cruiser Pickup yenye namba za usajili PT 2615 alilolitoa kwa ajili ya Kituo cha Polisi cha Mtama katika Halmashauri ya Mtama Mkoani Lindi, kwenye viwanja vya Kituo hicho, Februari 21, 2021. Kulia ni Mkuu wa Kituo hicho, Nyabusani Wikama.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Februari 21, 2021 alikabidhi magari mawili kwa Polisi Mkoa wa Lindi. Magari hayo Toyota Land Cruiser Pickup lenye namba za usajili PT 2615 limetolewa kwa Kituo cha Polisi cha Mtama na jingine Toyota Land Cruise V6 lenye namba za usajili namba PT 4378 limekabidiwa kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
…..……………………………………..
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amekabidhi magari mawili kwa ajili ya matumizi ya Jeshi la Polisi mkoa wa Lindi yatakayowezesha askari kutoa huduma katika maeneo ya mkoa huo.
Amekabidhi magari hayo jana (Jumatatu, Februari 21, 2021) baada ya kuzungumza na wananchi katika kituo cha Polisi Mtama ambako makabidhiano hayo yalifanyika.
Magari yaliyokabidhiwa ni Toyota Land Cruiser Pickup yenye namba za usajili PT 2615 na Toyota Land Cruiser V6 lenye namba za usajili PT 4378.
Kati ya magari hayo gari moja TP 4378 ni kwa ajili ya ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi na gari lingine PT 2615 ni kwa ajili ya kituo cha polisi cha Mtama.
Waziri Mkuu alisema Serikali itaendelea kutoa vitendea kazi kwa jeshi la polisi kadiri inavyowezekana ili kuwawezesha askari nchini kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
`Akizungumza baada ya kupokea magari hayo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi Mtatiro Kitinkwi alisema magari hayo yatawezesha shughuli za doria kufanyika kwa uhakika.
”Magari haya unayotukabidhi leo (jana) yatawezesha shughuli za usafiri wa polisi, doria na usafirishaji wa mahabusu kufanyika kwa uhakika kulingana na jiografia ya halmashauri ya Mtama.”
Kamanda Kitinkwi aliiomba Serikali kukimalizia kituo cha Polisi cha Mtama kwa kuweka samani na kujenga kambi ya makazi ya askari katika kituo hicho.
Naye, Mbunge wa Jimbo la Mtama, Nape Nnauye kwa niaba ya wananchi aliishukuru Serikali kwa kutoa magari hayo ambayo yatawezesha shughuli za ulinzi na usalama katika jimbo hilo na Mkoa kufanyika kwa ufanisi zaidi.
Post a Comment