Mohammed al-Menfi amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Baraza la Urais la Libya huku Abdulhamid al-Dabaiba akichaguliwa kuwa waziri mkuu katika zoezi ambalo limesimamiwa na Umoja wa Mataifa siku ya Ijumaa. Wajumbe kutoka kambi hasimu nchini Libya wameafiki kunda serikali hiyo ya mpito katika kikao ambacho kimefanyika karibu na mji wa Geneva nchini Uswisi.
Al-Menfi na al-Dabaiba (Dbeibah), ambaye ni mfanyabiashara na mwanasiasa kutoka Misrata, walifanikiwa kuiangusha orodha iliyokuwa inaongozwa na Fathi Bashaga ambaye ni mkuu wa usalama katika serikali inayotambuliwa kimataifa ya Libya yenye makao yake Tripoli. Mgombea mwingine katika orodha iliyoshindwa alikuwa Aguila Saleh.
Kaimu mjumbe wa Umoja wa Mataifa Libya Stephanie Williams ametoa pongezi zake kwa mafanikio hayo ambayo ameyataja kuwa ya kihistoria. Amesema orodha ya Dbeibah imepata kura 39 kati ya 73 huku orodha ya Bashagha ikipata kura 34.
Uongozi mpya wa Libya utaitayarisha nchi hiyo kwa ajili ya ucahguzi wa bunge utakaofanyika Disemba 24. Aidha uongozi mpya unatarajiwa kuwahakikishia Walibya kuwa wameshirikishwa katika utawala.
Ni vyema kuashiria kuwa, kwa muda mrefu Libya imekuwa na serikali mbili hasimu, moja ikiwa na makao yake mjini Tobruk, iliyoko karibu na Jenerali Haftar, na nyingine ya Serikali ya Mapatano ya Kitaifa Libya inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa. Haftar anapata uungaji mkono wa kijeshi kutoka Umoja wa Falme za Kiarbau, Misri, Saudi Arabia na baadhi ya nchi za Ulaya.
Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) lilishambulia nchi hiyo na kusaidia harakati za kumuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Muammar Gaddafi hapo mwaka 2011.
Tangu wakati huo, nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika imekuwa ikishuhudia vita vya ndani na machafuko ambayo yameharibu na kuvuruga kabisa maisha ya raia wa nchi hiyo na kutishia kutokea maafa ya kibinadamu.
Post a Comment