Na Bashir Nkoromo, Dar es Salaam
Rais Dk. John Magufuli ametangaza siku 3 za maombi na kufunga na amewataka Watanzania kuondoa hofu katika kipindi hiki ambacho dunia inapitia wakati mgumu wa kukabiliana na janga la Korona na badala yake wachukue tahadhari na kumtanguliza Mungu, ambapo kuhusu maombi na kufunga amewataka Waislamu kuanza leo Ijumaa, Wasabato kesho Jumamosi na Wakristo wengine keshokutwa Jumapili.
Pia ameeleza kusikitishwa kwake na vitendo vya kutishana na uzushi vinavyofanywa na baadhi ya watu kupitia mitandao ya kijamii ikiwemo uzushi uliofanywa dhidi ya Waziri wa Fedha na Mipanoo Dk. Philip Mpango aliyezushiwa kafariki dunia ilihali yupo hai na anaendelea vizuri na matibabu na kusisitiza kuwa Serikali haina mpango wa kufungia watu majumbani mwao na kwamba Mungu aliyeiepusha Tanzania na madhara makubwa ya ugonjwa huo mwaka jana ataiepusha na mwaka huu.
Rais Dk. Magufuli ametoa kauli hizo alipozungumza wakati akiongoza viongozi na wananchi kutoa heshima za mwisho na kuuaga mwili wa aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Mhandisi John Kijazi katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam, leo.
Katika salamu zake Rais Magufuli amemuelezea Marehemu Balozi Kijazi kuwa alikuwa kiongozi mahiri, mwadilifu, mnyenyekevu, msikivu, mcha Mungu, asiyejikweza, asiyetaka makuu na mwenye huruma na upendo mkubwa kwa viongozi wenzake, watumishi na jamii kwa ujumla jambo lililomfanya kuwa kipenzi cha watu.
Rais Magufuli amesema kutokana na uadilifu wake wa hali ya juu tangu akiwa Mhandisi wa Barabara wa Mkoa wa Dodoma na baadaye kuwa Mkurugenzi wa Barabara wa Wizara ya Ujenzi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Balozi wa Tanzania nchini India aliamua kumteua kuwa Katibu Mkuu Kiongozi kuanzia mwaka 2016 hadi mauti yalipomkuta juzi, Februari 17, 2021 kazi ambayo ameifanya vizuri, na kumalizia kwa kutoa pole kwa familia ya Marehemu Balozi Kijazi na amemuomba Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi.
Pia Rais Magufuli amerudia kutoa salamu za rambirambi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kufuatia kifo cha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad aliyefariki dunia juzi, Februari 17, 2021 na kuzikwa jana Kisiwani Pemba.
Amemuelezea Maalim Seif kuwa alikuwa kiongozi aliyependa amani na umoja licha kufanya siasa zake kupitia vyama vya upinzani pamoja na utayari wake wa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa Visiwani Zanzibar ambapo mpaka mauti yanamkuta alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais.
Amefafanua kuwa hata alipokutana naye Jijini Dar es Salaam baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na pia alipomtembelea nyumbani kwake Chato Mkoani Geita tarehe Januari 14, 2021, alisisitiza kuwa hatowahamasisha wafuasi wake kufanya vurugu na kuvunja amani na alipenda kuwepo umoja wa Wazanzibari na Watanzania wote kwa ujumla.
Kufuatia hali hiyo, Rais Dk. magufuli amewataka Wazanzibar na Watanzania kwa jumla kumuenzi Maalim Seif kwa kudumisha amani na umoja uliopo ili kuendeleza ndoto aliyokuwa ameanza kuitekeleza kabla ya kufariki dunia.
Baadhi ya viongozi wengine waliotoa heshima za mwisho kwa mwili wa Kijazi ni Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla, Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma, Naibu Spika Tulia Ackson, Rais Mstaafu wa Jakaya Kikwete, Mawaziri, Makatibu Wakuu, Viongozi Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama na viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Aboubakar Kunenge.
Post a Comment