********************************
Na Damian Kunambi, Njombe.
Shule ya msingi Mfalanyaki iliyopo katika kata ya Mavanga wilayani Ludewa mkoani Njombe inakabiliwa na upungufu wa vyumba tisa vya madarasa na kupelekea baadhi ya wanafunzi kusomea chini ya miembe.
Akizungumza hayo mratibu wa elimu kata ya Mavanga Hosea Chaula wakati akimueleza mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga changamoto zinazoikabili sekta ya elimu katika kata hiyo pindi mbunge huyo alipotembelea kata hiyo kwa lengo la kusikiliza changamoto za wananchi.
Chaula amesema kuwa shule hiyo inawanafunzi 816 ambapo kwa idadi hiyo wanatakiwa kuwa na vyumba 18 vya madarasa lakini wanavyumba tisa kitu ambacho hupelekea wanafunzi hao kukaa chumba kimoja kwa idadi ya 120 mpaka 130 badala ya 40 kwa chumba huku wengine wakilazimika kusomea chini ya miembe.
“Hii shule ni ya pili kwa ukubwa katika wilaya yetu na ina wanafunzi wengi, hivyo inasikitisha sana kuona mazingira wanayosomea wanafunzi si rafiki hata kidogo hasa katika kipindi hiki cha kifuku tunapata tabu sana jinsi ya kuwafundisha wanafunzi hao kwani mvua zinanyesha ni vigumu kuwaweka nje”, Alisema Chaula.
Sanjari na hilo pia mratibu huyo alizungumzia changamoto ya bweni la wanafunzi pamoja na uhaba wa vitanda katika shule ya sekondari Mavanga ambapo kuna bweni moja tu la wanafunzi wakike na wanalala chini na kupelekea bweni hilo kutotosha na wanafunzi wengine kulazimika kulala madarasani.
Aliongeza kuwa kutokana na wanafunzi hao kulala madarasani wanekuwa wakitoroka nyakati za usiku kwenda mitaani ambapo huko wamekuwa wakibakwa na kupata mimba na kusababisha kukatisha masomo yao.
Aidha kwa upande wa mbunge wa jimbo hilo Joseph Kamonga amesema serikali ya sasa imelenga kuwasaidia wananchi wake hivyo changamoto hizo amezipokea na anaendelea kuzifanyia kazi kwani mpaka sasa katika kijiji cha Mavanga tayari zimeshakuja milioni 50 kwa ajili ya shule ya sekondari Mavanga ambapo milioni 20 kati ya hizo ni kwaajili ya ujenzi wa chumba cha darasa na milioni 30 kwaajili ya maabara.
Ameongeza kuwa kuhusu wanafunzi kulala chini diwani wa kata hiyo ya Mavanga Daud Luoga alisha mshirikisha kwa kumuomba amsaidie kupata kibali cha kucharanga mbao katika moja ya mashamba ya miti yaliyopo katika kata hiyo ambapo mbunge huyo alifanya hivyo kwa kuongea na mkurugenzi wa maliasi na ombi hilo lilikubaliwa.
“Hili tatizo diwani wenu alikwisha nieleza na nikafanya mawasiliano na mkurugenzi wa maliasi na kumuunganisha diwani wenu amuelekeze eneo iliyopo miti hiyo ambapo mkurugenzi alikubali na kuwataka waandike barua ikiwa ni hatua ya kupata kibali hicho”, Alisema Kamonga.
Aidha kwa upande wa wananchi wa kata hiyo walifurahia hatua mbalimbali za msaada uliotolewa na mbunge wao katika kutatua matatizo yao sambamba na kusoma lisala iliyoelezea misaada hiyo waliyoipata.
Akisoma taarifa hiyo ya pongezi kwa niaba ya wananchi hao afisa mtendaji kata Hakimu Katabazi alianza kwa kumshukuru mbunge huyo kwa kumnunulia mwananchi mlemavu wa miguu baiskeli, kuwapa mifuko ya saruji 120 kwa fedha za mfuko wa jimbo kwaajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa na ofisi ya walimu shule ya misingi Mavanga.
Pia kuibua upya mradi wa maji wa kijiji cha Mbugani ambao tayari ulikuwa umefifia ambapo kwa sasa mafundi wanaendelea na uboreshwaji wa mradi huo, kuboresha miundombinu ya barabara, kupata fedha za uboreshaji majengo ya shule, kupata kibali cha kupasua mbao na mengineyo.
“Kwakweli tunamshukuru sana! Mbunge wetu kwani ndani ya kipindi kifupi cha uongozi ametekeleza mambo mengi sana katika kata yetu, hatuna budi kusema viatu alivyoviacha marehemu Deo Filikunjombe vimemtosha sawasawa”, walisema wananchi.
Post a Comment