NA IS-HAKA OMAR, PEMBA.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dk. Abdulla Juma Saadalla Mabodi, amewataka wananchi wa Jimbo la Pandani Kisiwani Pemba kumchagua mgombea wa kiti cha Uwakilishi kwa tiketi ya CCM Mohamed Juma ili awaletee maendeleo katika jimbo hilo.
Hayo ameyasema wakati akizindua mkutano wa kampeni za CCM huko Pandani, alisema mgombea huyo ana nia ya dhati ya kuleta maendeleo endelevu ndani ya jimbo hilo.
Dk. Mabodi, amesema CCM imechagua mgombea makini,mweledi,mchapakazi,mcha mungu, msomi na mzalendo mwenye vigezo vya kuleta mapinduzi ya kimaendeleo ndani ya jimbo hilo.
Aliwahakikishia wananchi wa jimbo hilo kuwa mgombea huyo anaelewa vizuri changamoto za jimbo hilo na yupo tayari kuzitatua kwa haraka endapo watampatia ridhaa.
Alisema CCM ndio Chama pekee chenye sera,malengo,muelekeo na Ilani ya Uchaguzi inayotekelezeka kwa kutatua kwa wakati changamoto za wananchi.
Alisema Chama kitafanya kampeni za nyumba kwa nyumba kwa kunadi sera zake pamoja na kuomba ridhaa ya wananchi ili wamchague kwa kura nyingi mgombea huyo.
“ Tunaenda nyumba kwa nyumba kwa mtindo wa nyakua nyakua ili kuwafikia wananchi wote ndani ya jimbo hili, tukiomba baraka zenu na mgombea wetu mnamjua vizuri kwani ni mzawa wa jimbo hili”, . alisema Dk. Mabodi.
Akitaja maendeleo yaliyofikiwa ndani ya jimbo hilo alisema serikali imetekeleza vizuri Ilani ya uchaguzi iliyopita kwa kujenga barabara ya kiwango cha lami,huduma za maji safi na salama, shule za msingi na sekondari pamoja kuimarisha huduma za afya kwa kujenga vituo vya Afya ndani ya jimbo hilo.
Alisema tayari taasisi mbalimbali za Kibenki zimetoa mafunzo ya kuwajengea uwezo wanawake na vijana ili wawe na uelewa wa masuala ya mikopo yenye masharti nafuu na kuweza kukopesheka.
Katika maelezo yake Dk. Mabodi, alisema hivi karibu kuna mradi mkubwa kupitia Wilaya ya Wete wa kutoa mafunzo ya ushoni kwa akin a mama ambapo tayari vyerehani vimeashanunuliwa na wanawake wa jimbo hilo nao ni miongoni mwa watakaonufaika.
Alisema Serikali inapanga kujenga viwanda vikubwa vya kusalifu mazao ya baharini na kutoa ajira nyingi kwa wananchi wa kisiwa cha Pemba.
Alieleza kwamba ahadi zote zilizoahidiwa kupitia kampeni za uchaguzi mkuu uliopita serikali tayari imeanza kuzitekeleza kwa kuhakikisha wananchi wananufaika na fursa mbalimbali za kujikwamua kiuchumi.
Alisema makundi hayo yataendelea kupewa mafunzo ya ujasiriamali na mafunzo ya amali kwa vijana ili waweze kufanya biashara na kutengeneza bidhaa zenye viwango kwa lengo la kujikwamua kiuchumi.
Alieleza kwamba CCM katika uchaguzi huo inatarajia kushinda kutokana na uimara wa sera na utekelezaji mzuri wa Ilani yake ya uchaguzi hatua inayoleta maendelero kwa wananchi wote bila ubaguzi wa rangi,dini,kabila na kisiasa.
Kupitia uzinduzi huo Dk. Mabodi, alimnadi na kumuombea kura mgombea huyo sambamba na kumkabidhi Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020/2025.
Alisifu juhudi kubwa za kuasisi maridhiano ya kisiasa zilizofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa lengo la kuendeleza amani na utulivu wa nchi.
“Kwa sasa Pemba amani ipo watu wanazikana,wanafanya ibada pamoja na kushirikiana katika masuala mbalimbali hivyo tunakuombeni maridhiano haya yaenziwe ili kuleta umoja miongoni mwetu’, .alisema Dk. Mabodi.
Kwa upande wake mgombea uwakilishi kwa tiketi ya CCM Jimboni humo Mohamed Juma Ali, alivitaja vipaumbele vyake kuwa endapo atapewa ridhaa ya kuchaguliwa kuwa mwakilishi atahakikisha anamaliza changamoto zote zilizomo jimboni humo.
Alisema atahakikisha vijana wasiokuwa na ajira rasmi ndani ya jimbo hilo anawapata mafunzo ya amali ili wawe na ujuzi wa fani mbalimbali zitakazowawezesha kujiajiri wenyewe.
Aliahidi kuviwezesha kiuchumi na kuvitafutia miradi vikundi vya akina mama ili wafanye shughuli za ujasiriamali na kujiajiri wenyewe.
Alisema anafahamu wananchi wana matarajio mengi ya kupata maendeleo hivyo matarajio hayo yatatimia endapo watampigia kura na kuhakikisha anashinda mgombea anayetokana na CCM.
Alisema atatua changhamoto za upungufu wa huduma za maji,umeme na afya katika maeneo mbalimbali ya vijiji vya Jimbo hilo.
Alieleza kwamba nia yake ya kuwania nafasi hiyo ni kuleta ukombozi wa kimaendeleo ambayo yamekosekana kwa miaka mingi na kupelekea wananchi kuishi katika mateso ya muda mrefu kipindi jimbo hilo lilipokuwa mikononi mwa chama cha upinzani.
“Nimezaliwa hapa na kukulia hapa shida na changamoto za jimbo letu ninazifahamu kwani nami pia ni mmoja wa vijana niliyesoma kwa tabu hivyo naomba mniamini na kunipa nafasi ya kukutumikieni’’,.alisema mgombea huyo.
Aliwaomba wananchi hao wasipoteze tena nafasi hiyo kwa kuwachagua wapinzani bali wamchague mgombea wa CCM ambaye anatokana na chama chenye uzoefu wa kuongoza na kuleta maendeleo.
Mapema akizungumza Mwenyekliti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mbwerwa Hamad Mbwera alisema wamejipanga vizuri kwa kuhakikisha mgombea wa CCM anashinda ili awatumikie wananchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kusini Pemba, Yussuf Ali Juma aliwaomba wananchi wa jimbo hilo kufanya maamuzi yanayofaa ya kukipa ridhaa ya nafasi ya uwakilishi ili CCM iwatumikie.
Uzinduzi wa kampeni hizo unatokana na kufariki kwa aliyekuwa Mwakilishi Mteule wa ACT Wazalendo marehemu Abubakar Khamis Bakar aliyefariki Novemba mwaka 2020.
Uchaguzi mdogo wa Jimbo hilo la Pandani unatarajiwa kufanyika Machi 18,mwaka 2021.
Post a Comment