Dodoma, Tanzania
Katika hali inayodhihirisha kuwa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli ni Shujaa wa Afrika, Marais wa nchi zaidi ya kumi, na mamia ya viongozi mbalimbali wa nchi za nje wakiwemo Mabalozi zaidi ya 50 wanatarajiwa kuhudhuria utoaji heshima na kuuaga mwili katika tukio la Mazishi ya Kitaifa ya Dk. Magufuli, yatakayofanyika kesho kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Akizungumza leo jijini Dodoma, Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbas amesema baadhi ya Maraisi hao ni kutoka nchi za Kenya, Malawi, Commoro, Msumbiji, Zimbabwe, Zambia, Namibia, Botswana, Afrika Kusini na Congo DRC na pia wawakilishi kutoka Asasi za Kikanda na Mabalozi hao zaidi ya 50 wamethibitisha kuwepo katika tukio hilo la maziko ya Kitaifa.
Dk. Abbas amesema Rais wa Rwanda amemtuma Mwakilishi wake ambaye ni Waziri Mkuu wake, Rais wa Angola amemtuma Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi hiyo kumuwakilisha wakati Rais wa Burundi amemtuma Makamu wake wa Rais kumuwakilisha.
” Mwili wa mpendwa wetu Hayati Dk. Magufuli utawasili jioni ya leo hapa Dodoma na utaelekea Ikulu Chamwino ambapo wananchi wa jiji la Dodoma mnaombwa kujitokeza barabarani wakati mwili ukipita ili tumpe heshima kiongozi wetu.
Mara baada ya kuwasili mwili huo utaelekea Ikulu ya Chamwino kwa kupitia barabara za Chako ni chako, Barabara ya Nyerere, Round about ya Mkuu wa Mkoa, Bunge, Morena, Bwigiri- Chamwino-Ikulu, wanachi wote wa maeneo haya wanaombwa kujipanga kwenye barabara hizo kutoa heshima zao”, amesema Dk. Abbas
Dk. Abbas amesema kuwa kesho Mwili utatoka Ikulu Chamwino na utaanzia Bungeni ili Wabunge wapate fursa ya kuaga na baadaye mwili upelekwa Uwanja wa Jamhuri na kwamba Viongozi ndiyo wataanza kuaga na kufuatiwa na Wananchi ambapo watapewa fursa ya kuaga hadi usiku.
Alikumbusha kuwa kama ilivyotangazwa na Rais Samia Suluhu Hassan kesho itakuwa ni mapumziko na halikadhalika Machi 26 ambayo ndio Mwili wa Dk. Magufuli utapumzishwa kwenye makazi yake ya milele pia itakuwa ni siku ya mapumziko kitaifa
Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk. Hassan Abbas akizungumza na Waandishi wa habari leo jijini Dodoma, kuhusiana na mambo mbalimbali yatakayojiri katika utoaji heshima za mwisho katika tukio la Mazishi ya Kitaifa ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Magufuli, katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, kesho.
Post a Comment