Featured

    Featured Posts

MWILI WA DK. MAGUFULI WAAGWA BUNGENI DODOMA, MAJALIWA " NIMEISHIWA NGUVU KILA NINAPOANGALIA JENEZA NAHISI DK. MAGUFULI ANANIPIGIA SIMU AKINIPA MAAGIZO

Na Ripota CCM Blog, Dodoma

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema mengi yamezungumzwa kuhusu aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dk. John Pombe Magufuli lakini kwake imekuwa siku ngumu kwani kila anapoangalia jeneza anahisi kama vile Dk. Magufuli anampigia simu akimpa maagizo na maelekezo.


"Sina kubwa la kusema, waliotagulia wamesema mengi kuhusu mpendwa wetu, binafsi napata shida kusema, naona kama vile ananipigia simu, ananipa maagizo, naomba mnivumilie, ni siku ngumu kwetu.


Kila mmoja ana neno la kumuelezea Dk. Joh Magufuli, tukianza kuelezea hatutamaliza, amefanya mambo mengi kwenye majimbo yetu, tunachokifanya leo hapa ni kumuombea dua, ni majonzi makubwa kwetu, na sio kwetu tu Watanzania bali Afrika inamlilia, inasikitika, nchi za SADC ,Bara la Afrika linamlilia, alikuwa sehemu ya viongozi wa bara hili, hivyo majonzi haya siyo ya kwetu peke yetu", Majaliwa amesema hayo wakati akizungumza kabla ya Wabunge kutoa heshima zao za mwisho kwa Dk. Magufuli na kumuombea Dua, katika Viwanja vya Bunge Mjini Dodoma, leo. 


"Jukumu letu ni kumuombea, tunamlaza katika nyumba yake ya milele machi 26, leo tumepata fursa ya kuja kumuombea, kwa uzoefu ambao tumeupata Dar es Salaam watu walikuwa wengi sana, hivyo kwa hapa Dodoma tumeamua kubadilisha utaratibu, badala ya kwenda kuaga na kumuangalia, tutakachofanya ni kuzungusha mwili mara mbili au tatu uwanjani," amesema Waziri Mkuu Majaliwa.


Ameongeza kuwa baada ya hapo mwili wa kipenzi cha Watanzania na Afrika kwa jumla Dk. Magufuli utapitishwa katika barabara mbalimbali ili Wananchi waone jeneza lenye Mwili wa Dk. Magufuli na baadaye kuwekwa katika uwanja wa jamhuri kwa ajili ya tukio la kutoa heshina na kuaga mwili wa marehemu Kitaifa na kesho mwili utapelekwa  Zanzibar, halafu mwanza na kisha Chato ambako nao watapata nafasi ya kumuaga kwa siku nzima na kisha kumpumzisha  Hayati Dk. Magufuli katika nyumba yae ya milele.


Majaliwa amesema wakati wakimuombea Dk. Magufuli na kumuaga katika viwanja hivyo vya Bunge, mama mzazi wa Dk. Magufuli yupo kitandani kwa mwaka wa pili sasa akiugua, "hivyo Watanzania tumuombee mpendwa wetu na wakati huo huo tumuombee mama yetu apate nguvu na aweze kunyanyuka kitandani".


Akitoa salamu zake Job Ndugai amemzungumzia Hayati Dk. John Pombe Magufuli akisema "Rais wetu katika historia yake amekuwa mwenzetu hapa bungeni kwa miaka 26, amekuwa sehemu ya jumuiya hii tangu mwaka 1995 kama Mhe. Mbunge, Naibu Waziri, Waziri na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Rais wetu katika historia yake amekuwa mwenzetu hapa bungeni kwa miaka 26, amekuwa sehemu ya jumuiya hii tangu mwaka 1995 kama  Mbunge, Naibu Waziri, Waziri na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania".


“Leo ni siku ya majonzi makubwa hapa bungeni kwa kuwa tumefiwa na mwenzetu, tumelemewa, tumechanganyikiwa, watanzania tunalia, sisi wabunge tunasema asante Mungu kwa ajili ya Rais John Pombe Magufuli aliyeishi siku zote kwa kumtanguliza Mungu mbele,”. Amesema Job Ndugai


Namshukuru Mungu kwa kunipa fursa ya kufanya kazi na Hayati Rais Magufuli kwa miaka 20  Bungeni kama rafiki yangu, ndugu yangu na kama kiongozi wangu, safari imetimia na mwendo ameumaliza, rafiki yangu John leo amelala mbele yetu


Dk. Magufuli ulikuwa mtu mwema, alipanda mbegu, alikuwa mpanzi kama yule mpanzi wa kwenye Biblia naamini mbegu aliyopanda imedondoka kwenye udongo mzuri, amepanda barabara za lami kila sehemu ya nchi yetu, madaraja ambayo hatukuamini kama tungeyaweza, amejenga Masoko, amejenga Meli, viwanja vya ndege, Reli ya kisasa SGR, Bwawa la umeme la Nyerere Rufiji, Shule, Viwanda, Vyuo, Vituo vya afya, Hospitali, Amejenga. Amejenga. Amejenga.


Asante Mungu kwa kutupatia Rais Samia Suluhu, tunaomba umpe siha njema, awe hodari, mwenye subira, awe mstahimilivu, pia usimpungukie hekima, na sisi wabunge tunaahidi kusimama na Mama Samia, Akasema Ndugai.

Naye Naibu Spika Tulia Ackson, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akimzungumzia Hayati Rais John Pombe Magufuli amesema alikuwa  mtu mcha Mungu, "tumeuona wema wake, lakini kama kitabu cha Mungu ‘Biblia’ kisemavyo kuwa mwanadamu siku zake za kuishi si nyingi basi kazi ya Mungu haina makosa".


"Hakuna ambaye hakuona yale mazuri na mengi aliyoyafanya Hayati John Pombe Magufuli, kila mtu ni shahidi. Tuliwachagua viongozi wetu wapendwa Rais Magufuli na Mama Samia, sasa tumeachiwa Rais Samia Suluhu tunaamini kuwa atatufikisha Kanaani, hivyo tuna imani naye,”. Akasema Dk Tulia


Dk. Tulia Amewapa pole watanzania, mke wa Hayati Rais Magufuli, Waziri Mkuu na viongozi wengine wote kwa msiba huu mkubwa kwa taifa la Tanzania.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza wakati wa kuaga mwili wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Hayati Dkt John Pombe Magufuli kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma leo.
Wabunge mbalimbali wakitoa heshima za mwisho kwenye Jeneza lenye mwili wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Hayati Dkt John Pombe Magufuli,ambapo baada ya hapo atapelekwa uwanja wa Jamhuri kwa kutolewa heshima za mwisho Kitaifa.👇




author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana