Featured

    Featured Posts

NAIBU WAZIRI KIPANGA ATAKA UJENZI WA VYUO VYA VETA KUFUATA MICHORO SAHIHI

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga

 Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Kipanga ameitaka Mamlaka ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kuhakikisha miradi yote ya ujenzi wa vyuo vya VETA vya Wilaya inatekelezwa kwa kufuata michoro sahihi iliyopitishwa.


Mhe. Kipanga ameyasema hayo 14 Machi, 2021 wakati wa ziara ya kukagua mradi wa ujenzi wa chuo cha VETA cha Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya ambapo amesema hajaridhishwa na kazi ya ujenzi inayoendelea chuoni hapo kwa kuwa haina ubora unaotakiwa kutokana na mafundi kujenga bila kuzingatia michoro sahihi ya majengo.


"Niwatake VETA ambao ndio wasimamizi wakuu wa miradi ya ujenzi wa vyuo vya VETA vya Wilaya nchini kuhakikisha ujenzi wa miradi hiyo unafanyika kwa kufuata michoro sahihi iliyopo ili majengo yaendane na thamani ya pesa iliyotolewa.  Ujenzi unaofanyika hapa hauna ubora unaotakiwa sababu ya usimamizi mbovu, laiti mngekuwa mnasimamia ipasavyo mngeyaona makosa mapema na kuyarekebisha," amesema  Kipanga.


Aidha, Naibu Waziri Kipanga amewapongeza wasimamizi wa mradi huo kwa kufanikiwa kukamilisha sehemu kubwa ya ujenzi na amewasisitiza kuhakikisha wanakamilisha ujenzi uliobakia kwa kufuata michoro.


"Pamoja na mapungufu yaliyopo niwapongeze kwa kumaliza sehemu kubwa ya  ujenzi, nimeona majengo 13 kati ya 17 tayari yameshapauliwa na kuezekwa na niwatahadharishe kuwa nikirudi tena kukagua  nikakuta kazi  mbovu mtalazimika kubomoa na kujenga upya kwa gharama zenu wenyewe," amesisitiza Mhe.  Kipanga.


Akizungumza katika ziara hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Kivuma Msangi amempongeza Mhe. Kipanga  kwa kuonesha utendaji mzuri na kuahidi kushirikiana na VETA kusimamia Mradi huo ili kuhakikisha kazi inakamilika kwa wakati na ubora unaotakiwa.


"Nikupongeze mheshimiwa Naibu Waziri kwa utendaji mzuri wa kazi zako na niahidi kushirikiana bega kwa bega na wasimamizi wa mradi huu kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa ubora unaotakiwa," amesema Msangi.


Naye Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dkt. Pancras Bujuru akizungumza katika ziara hiyo amekiri kuwepo mapungufu katika ujenzi huo na kuahidi kufanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa na Mhe. kipanga.

author

Author Name

Author Description!

Get Free Email Updates to your Inbox!

Post a Comment

www.CodeNirvana.in

Magazeti Ya Leo

Copyright © Magazeti ya Leo, Habari Leo Tanzania, Mwananchi, Michuzi, mwanaspoti, nipashe, Udaku | Designed By Code Nirvana