Denmark imekuwa nchi ya sita ya Ulaya kusimamisha matumizi ya chanjo ya kukabiliana na ugonjwa wa Covid-19 ya AstraZeneca kutokana na madhara yake kwa damu za watu waliopigwa chanjo hiyo.
Taarifa iliyotolewa jana Alkhamisi na Wizara ya Afya ya Denmark imesema: Kufuatia ripoti zinaonesha kuwa chanjo ya AstraZeneca imekuwa na taathira hasi kwa damu za watu waliochanjwa, tumesimamisha kwa muda matumizi ya chanjo hiyo.
Wizara hiyo imesema inafanya uchunguzi kubaini iwapo kuna uhusiano wowote baina ya chanjo ya AstraZeneca na matatizo ya damu kuganda yaliyowapata watu waliopigwa chanjo hiyo nchini humo.
Siku ya Jumatatu, Austria ilisimamisha pia utumiaji wa chanjo ya AstraZeneca baada ya muuguzi aliyekuwa na umri wa miaka 49 kuaga dunia baada ya kupewa chanjo ya AstraZeneca.
Mbali na Denmark na Austria, nchi nyingine za Ulaya zilizotangaza kusimamisha kwa muda matumizi ya chanjo ya AstraZeneca kutokana na athari zake hasi kwa damu za wanaochanjwa ni Estonia, Latvia, Lithuania, na Luxemburg. Duru za habari zinaarifu kuwa, Norway pia imesimamisa matumizi ya chanjo hiyo.
Nchi kadhaa za Afrika zikiwemo Kenya, Kongo DR na Uganda zimepokea mamilioni ya dozi za chanjo ya AstraZeneca kupitia mpango wa kimataifa wa COVAX; na kwa sasa zinaendelea na kampeni za kuwachanja wananchi wao.
Mwezi uliopita wa Februari, Wizara ya Afya ya Afrika Kusini ilisema imevunjwa moyo na habari kuwa chanjo ya AstraZeneca haina taathira kwa virusi vipya vya Corona na kuagiza shehena ya chanjo hiyo iliyonunuliwa na Pretoria kutoka Uingereza kuuzwa kwa nchi nyingine.
Post a Comment