Kwa muda wa zaidi ya miaka 10 sasa kile kinachotajwa kuwa ni 'mazungumzo jumuishi' kimebadilika na kuwa jukwaa la kueneza madai yasiyo na msingi dhidi ya Iran katika fremu ya haki za binadamu. Jukwaa hili na mielekeo yake yote ya upande mmoja lina malengo ambayo tayari yameainishwa na hayahusiana hata kidogo na huduma kwa haki za binadamu.
Esmaeil Baghaei Hamaneh, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Iran katika ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Geneva akizungumza Jumamosi katika Kikao cha 46 cha Baraza la Haki za Binadamu alibainisha ukweli huo ambapo alikosoa vikali taarifa zisizozingatia uadilifu na zilizojaa upotoshaji za ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu nchini Iran. Aidha amesema taarifa ya Javaid Rehman, ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Iran imetolewa kwa malengo ya kisiasa yaliyoungwa mkono na madola ya Magharibi.
Kuhusiana na madai kuwa wanawake wa Iran wanatazamwa kama raia wa daraja la pili, ameashiria mafanikio makubwa yaliyoweza kufikiwa na wanawake nchini katika sekta za kielimu, kijamii na usimamizi wa nchi na kusema: "Wanawake nchini Iran si raia wa daraja la pili na madai kama hayo hayakubaliki. Si sawa kutaja nusu ya watu wa nchi kuwa ni raia wa daraja la pili katika hali ambayo wana hadhi maalumu."
Tukiangazia taarifa ya haki za binadamu ya madola ya Magharibi dhidi ya Iran kuna nukta kadhaa za kuzingatiwa. Moja ya nukta hizo ni hii kuwa, taarifa hiyo ina utambulisho wa kisiasa wenye kupendelea upande mmoja. Ni wazi kuwa taarifa kama hizo zina malengo fiche.
Ukweli wa mambo ni kuwa, iwapo ukatili na ubaguzi wa rangi ulioshuhudiwa hivi karibuni Marekani na nchi za Ulaya ungejiri katika nchi zingine, kungetolewa makumi ya maazimio na hata nchi husika zingewekewa vikwazo. Aidha ni wazi kuwa hakuna ripota maalumu wa Umoja wa Mataifa ambaye huteuliwa kuchunguza ukiukwaji wa haki za binadamu katika nchi za Magharibi.
Madola ya kibeberu ya Magharibi ambayo yanadai kutetea haki za binadamu yanatoa taarifa na maazimio dhidi ya nchi zingine katika hali ambayo yenyewe yanawakandamiza wanaolalamikia ubaguzi. Aidha nchi hizo za Magharibi zinaruhusu kuvunjiwa heshima thamani na matukufu ya kidini hasa matukufu ya Uislamu. Hali kadhalika katika nchi za Magharibi tunashuhudia namna ambavyo Waislamu wanavyokandamizwa na kuwekewa mashinikizo. Pia katika nchi hizo hizo za Magharibi, yaani Umoja wa Ulaya na Marekani, wahajiri hasa kutoka nchi za Afrika na Asia wako chini ya mashinikizo, mateso makali na ubaguzi.
Kuhusu hali ya wanawake, kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2019 ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ufaransa, kati ya wahanga 149 wa ukatili wa ndani ya familia 121 walikuwa ni wanawake. Aidha nchini Ujerumani, kwa mujibu wa takwimu za polisi ya jinai nchini humo, kwa wastani ukatili wa ndani ya familia hupelekea mwanamke mmoja kupoteza maisha kila baada ya siku tatu.
Nchini Marekani pia, mauaji ya Mmarekani mwenye asili ya Afrika George Floyd, ambayo yaliibua hasira kote duniani, yemebadilika na kuwa nembo ya kimataifa ya kupinga ubaguzi wa rangi katika nchi za Magharibi. Walimwengu katu hawatamsahau Floyd.
Wanaodai kutetea haki za binadamu wanasema wana wasi wasi kuhusu hali ya haki za binadamu Iran katika hali ambayo vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran vimewasababishia Wairani wa kawaida matatizo ya kimaisha na kiafya.
Hivi sasa pia wakati ambao dunia inashuhudia kusambazwa chanjo ya corona, Iran ingali inawekeweza vikwazo vya dawa na chanjo. Iwapo taasisi au serikali hazitabainisha wasi wasi kuhusu haki za binadamu za watu hao, basi kuna wengi watakaopoteza maisha kutokana na vikwazo.
Mirqasem Muumini, mtaalamu wa masuala ya kimataifa anasema haki za binadamu katika nchi za Umoja wa Ulaya na Marekani hutumika tu kama chombo cha mashinikizo ili kufikia malengo ya kisiasa.
Kwa mfano pamoja na kuwa Saudi Arabia, haina uhuru wowote wa kijamii na wala haizingatii haki za binadamu lakini ni mshirika wa kistratijia wa Marekani na Ulaya. Wanaodai kutetea haki za binadamu wanailenga Iran kwa sababu sera zake zinakinzana na maslahi ya Marekani na Magharibi kwa ujumla.
Kwa maelezo hayo, ni wazi kuwa sera za kindumakuwili zinaonyesha kukosekana uzingatiwaji haki na ukweli miongoni mwa nchi hizo za Magharibi ambazo zinaitazama kadhia ya haki za binadamu kwa jicho la kisiasa.
Post a Comment