Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Humphrey Polepole (Mb) akitoa maelekezo ya kuboresha mfumo wa bwawa la maji la Kijiji cha Kaloleni kata ya Ubena Zomozi kwa niaba ya kamati anayoiongoza.
Baadhi ya wananchi wa Kaloleni kata ya Ubena Zomozi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze wakisikiliza Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Humphrey Polepole (Hayupo pichani) wakati akitoa maelekezo ya kuboresha mfumo wa bwawa la maji la kijiji chao.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Humphrey Polepole (Mb) akikagua mradi wa bwawa la maji la Kijiji cha Kaloleni kata ya Ubena Zomozi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Humphrey Polepole (Mb) akiteta jambo na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi mara baada ya kukagua mradi wa bwawa la maji la Kijiji cha Kaloleni kata ya Ubena Zomozi.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi akiiahidi Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuboresha mfumo wa bwawa la maji Kijiji cha Kaloleni kata ya Ubena Zomozi ili kuwapatia wananchi wa eneo hilo maji safi na salama.
Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Ladislaus Mwamanga akiiahidi Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuleta wataalam kufanya tathmini ya namna bora ya kuboresha bwawa la Kijiji cha Kaloleni kata ya Ubena Zomozi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Humphrey Polepole (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wajumbe wa kamati yake na watendaji wa Serikali mbele ya mradi wa bwawa la maji la Kijiji cha Kaloleni kata ya Ubena Zomozi.
****************************************
Na. James K. Mwanamyoto-Chalinze
Tarehe 14 Machi, 2021
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi ameiahidi Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kuboresha mfumo wa bwawa la maji Kijiji cha Kaloleni kata ya Ubena Zomozi iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze ili kuwapatia wananchi wa eneo hilo maji safi na salama.
Mhe. Ndejembi ametoa ahadi hiyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya kamati iliyoitaka Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kurekebisha mfumo wa bwawa hilo ili kuwapatia maji safi na salama wananchi wa kaloleni na vijiji jirani.
Mhe. Ndejembi amefafanua kuwa, licha ya mradi wa bwawa hilo kujengwa wakati wa awamu ya kwanza ya utekelezaji wa TASAF lakini kutokana na changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama inayowakabili wananchi wa eneo la Kaloleni na vijiji jirani, Serikali itafanya marekebisho kuwawezesha wananchi kupata huduma hiyo ya maji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Bw. Ladislaus Mwamanga amesema, ofisi yake itapeleka wataalam mapema iwezekanavyo ili kufanya tathmini ya namna bora ya kuboresha bwawa hilo.
Bw. Mwamanga ameongeza kuwa, fedha ya kufanya maboresho hayo ipo kwani mradi huo ni kipambule cha Serikali katika Utekelezaji wa Mradi wa kipindi cha pili cha Awamu ya Tatu kilichozinduliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
Awali akitoa maelekezo juu ya uboreshaji wa bwawa hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa Mhe. Humphrey Polepole (Mb) amesema, kamati imelazimika kutoa maelekezo hayo kutokana na umuhimu wa bwawa hilo kwa wananchi wa kijiji hicho na vijiji jirani.
Aidha, Mhe. Polepole amewataka wasimamizi wa mradi na wananchi kuhakikisha wanalitunza bwawa hilo ili wanufaike na uwepo wake kama Serikali ilivyokusudia.
Mradi wa bwawa la maji Kaloleni ulijengwa katika kipindi cha kwanza cha utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Awamu ya Kwanza kwa lengo la kuwapatia maji safi na salama wananchi wa Kaloleni na vijiji jirani, ikiwa ni pamoja na kuiwezesha mifugo yao kupata maji ya kunywa.
Post a Comment