Rais Uhuru Kenyatta akizungumza wakati wa tukio la kuuaga mwili wa Hayati Dk. Magufuli Kitaifa, katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, leo.
CCM Blog, Dodoma
Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amesema Jumuiya ya Afrika Mashariki imempoteza rafiki na mwanamageuzi wa kweli ambaye aliziunganisha nchi zote zinazounda Jumuiya hiyo.
Rais Kenyatta Rais amesema katika uongozi wake Dk. Magufuli kupitia maono yake aliwafundisha wana-Jumuiya ya Afrika Mashariki kujitegemea kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuacha kutegemea misaada kutoka mataifa ya Nje.
"Dada yangu Rais Samia Suluhu Hassan Barabara umeshaoneshwa, sisi tupo nyuma yako nikuombe uendeleze kazi kubwa iliyoanzishwa na ndugu yetu Hayati Dk. John Magufuli, ninawaomba Watanzania muungane mumpe ushirikiano Rais Samia ili aweze kuendeleza falsafa ya Dk. Magufuli ya Hapa Kazi Tu, " akasema Rais Kenyatta
akizungumza katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, wakati wa tukio la kuaga Kitaifa mwili wa aliyekua Rais wa Tanzania, Hayati Dk. John Magufuli.
Rais Kenyatta amesema Afrika imempoteza mwanamageuzi wa kweli na kwamba yeye binafsi amempoteza rafiki wa kweli ambaye walikuwa wakipigiana simu kila siku tukishirikiana katika mambo mbalimbali ya kujenga mataifa ya Nchi zao na Afrika Mashariki kwa jumla.
Amesifu jitihada kubwa zilizofanywa na Dk. Magufuli katika kipindi chake cha uongozi kwa kujenga miundombinu ya barabara, nishati ya umeme, ujenzi wa kisasa huku akisema mchango wake katika ukuaji wa uchumi hautofutika kwa miaka yote.
Rais Kenyatta ametoa pole kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Mama Janneth Maguli na familia yote ya Hayati Magufuli na Watanzania kwa ujumla kufuatia kifo cha Dk Magufuli kilichotokea Machi 17 mwaka huu.
Post a Comment