Na Lydia Lugakila, Misenyi
Wanaonufaika na mikopo katika katika makundi mbalimbali katika Halmashauri ya Misenyi mkoani Kagera yameaswa kuachana na tabia ya kuzitumia pesa za mikopo kwa matumizi tofauti ikiwemo baadhi ya vijana kutumia pesa hizo kuoa.
Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera Godfrey Mheluka amesema hayo, katika hafla ya kukabidhi mikopo isiyo na riba ya jumla ya Sh. Milioni 139.2 kwa vikundi vya ujasiliamali vinavyonufaika na asilimia 10 ya fedha zinazotokana na mapato ya ndani ya Halmashauri ya wilaya ya Misenyi.
Mheluka amesema kuwa kwa vijana wengi imekuwa ni kama kawaida kwao kwani wakichukua mikopo wengine wamekuwa wakienda kuifanyia mambo tofauti ambapo mwingine anachukua fedha za mkopo kwa ajili ya kufanyia biashara lakini badala ya kufanya hivyo anakwenda kuoa.
"Utakuta kijana akishapata mkopo anafanya harusi kubwa na mwingine ambaye alikuwa ameishaoa anaoa tena mke wa pili kwa kutumia fedha hizo za mkopo ambao ameupokea ili kufanya biashara ajiinue kiuchumi", alisema Mheluka.
Amesema kuwa Tanzania ya sasa imefikia Uchumi wa Kati lakini wenye kushikilia uchumi wa kati ni vijana hivyo fedha wanazopewa sio zawadi bali ni fedha zinazozunguka ambapo zikirejeshwa zinatoa nafasi kwa mtu mwingine kukopa.
Shughuli ya kukabidhi mikopo hiyo limefanyika wakati wa mkutano wa Baraza Maalum la Madiwani wa Halmashauri hiyo kujadili mipango na bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 ambapo Halmashauri hiyo imetoa mikopo hiyo isiyo na riba.
Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii katika Halmashauri hiyo Beatrice Nicholous alitaja vikundi vilivyokopeshwa kuwa vikundi 41 vya wanawake vimepokea sh. milioni 61, vikundi 12 vya vijana (Sh. milioni 75) huku kikundi Cha watu wenye ulemavu kikikopeshwa sh. milioni 3.
Beatrice alitaja changamoto katika ukopeshaji kwa makundi hayo kuwa ni pamoja na wakopaji kukosa uaminifu na kuchelewesha marejesho na hivyo kuwakosesha fulsa ya kupata mikopo vikundi vingine vyenye sifa kwa wakati.
Alisema moja ya sababu za kushindwa kutoa marejesho ni baadhi ya vikundi kubadili matumizi ya fedha zinazokopeshwa pamoja na mwitikio mdogo wa vijana kuanzisha miradi ya pamoja na yenye tija na kuomba mikopo.
Mikopo hiyo imehusisha pikipiki pamoja na fedha ambapo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Misenyi Projestus Tegamaisho amevitaka vikundi hivyo vilivyokopeshwa kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa huku akikemea matatizo yaliyojitokeza kipindi cha nyuma ambapo walilazimika kuwatafuta kwa nguvu.
Aidha kwa upande wao wanufaika wa mikopo hiyo akiwemo Faidha Majula, Avitus Kamgisha na Jovin Ishengoma Audax wametoa pongezi kwa Halmashauri hiyo na serikali kwa ujumla huku wakiahidi kutumia mikopo hiyo kwa malengo na pia kurejesha mikopo hiyo kwa wakati.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Misenyi Projestus Tegamaisho na viongozi wenzake wakionyesha mfano wa Hundi ya fedha zilizokopeshwa kwa wajasiriamali wakati wa hafla hiyo. Baadhi ya Vijana wakiwa kwenye Pikipiki walizokopeshwa.
Post a Comment