Vikosi vya usalama nchini Myanmar vimeua kwa akali waandamanaji 50 hapo jana na kuwajeruhi makumi ya wengine katika moja ya siku mbaya zaidi za ukandamizaji kuwahi kushuhudiwa nchini humo tangu jeshi lilipotwaa madarakani ya nchi mwanzoni mwa mwezi uliopita.
Mauaji hayo yamefanyika katika hali ambayo kiongozi wa kijeshi wa nchi hiyo ametoa ahadi ya kuitisha uchaguzi katika muda uliotangazwa na kuirejesha nchi hiyo katika mkondo wa utawala wa kidemokrasia.
Mauaji hayo jana yamefanyika sambamba na maadhimisho ya Siku ya Jeshi iliyoadhimiwa jan nchini Myanamr, na kuandamana na hafla za magwaride katika miji mbalimbali ya Myanmar.
Jeshi la Myanmar limeadhimisha Siku ya Jeshi baada ya kuua watu wasiopungua 300 tangu lifanye mapinduzi na kutawaa madaraka ya nchi. Baadhi ya vyombo vya habari vimeitaja siku ya jana kuwa ya fedheha kwa jeshi la Myanmar.
Ikumbukwe kuwa, tarehe Mosi mwezi uliopita wa Februari jeshi la Myanmar lilitwaa madaraka ya nchi baada ya kumkamata Rais wa nchi hiyo, Win Myint na viongozi wengine akiwemo Aung San Suu Kyi, kiongozi wa chama tawala mwenye ushawishi mkubwa, kufuatia siku kadhaa za mivutano nchini humo.
Kisingizio cha jeshi cha kufanya mapinduzi hayo ni madai yake ya kutokea wizi na udanganyifu katika zoezi la uchaguzi wa Bunge wa Novemba mwaka jana (2020), ambapo kwa mujibu wa matokeo, chama tawala cha National League for Democracy (NLD) kinachoongozwa na Aung San Suu Kyi kiliibuka na ushindi.
Post a Comment