Spika wa Bunge, Mhe. Job Ndugai (kulia) akizungumza na Waheshimiwa Wabunge wakati wa uwasilishwaji wa Mapendekezo ya Serikali ya Mpango, Kiwango na Ukomo wa Bajeti kwa mwaka wa Fedha 2021/22 katika Ukumbi wa Pius Msekwa Jijini Dodoma. Katikati ni Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa na kushoto ni Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango.
Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwasilisha Mapendekezo ya Serikali ya Mpango, Kiwango na Ukomo wa Bajeti kwa mwaka wa Fedha 2021/22 katika Ukumbi wa Pius Msekwa Jijini Dodoma.
Waheshimiwa Mawaziri, Wabunge na Watendaji wa Serikali wakifuatilia uwasilishwaji wa Mapendekezo ya Serikali ya Mpango, Kiwango na Ukomo wa Bajeti kwa mwaka wa Fedha 2021/22 katika Ukumbi wa Pius Msekwa Jijini Dodoma.
PICHA NA BUNGE
…………………………………………………………………………………..
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA FEDHA NA MPANGO
MAELEZO YA MHE. DKT. PHILIP I. MPANGO (MB), WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO, AKIWASILISHA BUNGENI MAPENDEKEZO YA SERIKALI YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA NA KIWANGO CHA UKOMO WA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2021/22
DODOMA
11 MACHI, 2021
UTANGULIZI
- Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kutumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, kwa kuendelea kutujalia uhai na afya njema na kutuwezesha wote kukutana tena hapa Jijini Dodoma kupokea Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Kiwango cha Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/22. Aidha, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuendelea kuijalia nchi yetu umoja, amani na utulivu.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchukua fursa hii kutoa pole kwa Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge, ndugu, jamaa na marafiki kwa vifo vilivyotokea wakati wa mkutano uliopita: Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum (CCM) Manyara; na Mheshimiwa Atashasta Justus Nditiye aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Muhambwe (CCM). Tunamwomba Mwenyezi Mungu azipumzishe roho zao kwa amani. Aidha napenda kuchukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Yustina Arcadius Rahhi (Mb.), kwa kuteuliwa kwake kuwa Mbunge, Viti Maalum CCM, Manyara.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa hii inawasilisha Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Kiwango cha Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/22. Wasilisho hili ni kwa mujibu wa Kanuni ya 116 fasili ya (1) na (2) ya Kanuni za Kudumu za Bunge Toleo la Juni 2020. Aidha, taarifa hii imegawanyika katika sehemu kuu tatu: Sehemu ya Kwanza ni Tathmini ya Mwenendo wa Hali ya Uchumi; Sehemu ya Pili ni Mapitio ya Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21 na Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2021/22; na Sehemu ya Tatu ni Tathmini ya Utekelezaji wa Bajeti kwa Kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021 na Mapendekezo ya Kiwango cha Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/22.
SEHEMU YA KWANZA
TATHMINI YA MWENENDO WA HALI YA UCHUMI
- Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto mbalimbali zilizoikumba dunia ikiwemo mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu, uchumi wa Tanzania umeendelea kuwa imara. Kuendelea kukua kwa uchumi kumetokana na utekelezaji madhubuti wa sera za bajeti na fedha chini ya uongozi thabiti wa jemedari wetu, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2020, Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 4.7. Aidha, mfumuko wa bei ulifikia wastani wa asilimia 3.5 Januari 2021 ikilinganishwa na asilimia 3.7 Januari 2020. Riba za amana kwa kipindi cha mwaka mmoja zilipungua kufikia asilimia 8.41 Desemba 2020 kutoka asilimia 8.90 Desemba 2019 na riba za mikopo ya kipindi cha mwaka mmoja imepungua na kufikia wastani wa asilimia 15.72 Desemba 2020 kutoka asilimia 16.28 Desemba 2019. Thamani ya shilingi ya Tanzania dhidi ya dola ya Marekani na sarafu nyingine duniani imeendelea kuwa tulivu kutokana na utekelezaji wa sera thabiti za fedha na bajeti pamoja na kupungua kwa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho wa mali nje ya nchi.
2
- Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21, urari wa malipo ya kawaida unaojumuisha biashara ya bidhaa, huduma, mapato ya vitega uchumi na uhamisho mali wa kawaida uliimarika kufikia nakisi ya dola za Marekani milioni 331.3 kutoka nakisi ya dola za Marekani milioni 344.3 katika kipindi kama hicho mwaka 2019/20. Hii ilitokana na kuongezeka kwa mauzo ya bidhaa nje kwa asilimia 17.6 na kupungua kwa uagizaji wa bidhaa kutoka nje kwa asilimia 14.1. Aidha, mapato na malipo ya huduma yalipungua kutokana na kupungua kwa huduma za usafiri ikijumuisha utalii na safari za nje. Hadi Desemba 2020, akiba ya fedha za kigeni ilifikia dola za Marekani bilioni 4.8 inayokidhi uagizaji wa bidhaa na huduma nje ya nchi kwa kipindi cha miezi 5.6.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi Desemba 2020, deni la Serikali lilikuwa shilingi trilioni 59.0, sawa na ongezeko la asilimia 7.6 ikilinganishwa na shilingi trilioni 54.8 kipindi kama hicho mwaka 2019. Kati ya kiasi hicho, deni la nje ni shilingi trilioni 42.8 na deni la ndani ni shilingi trilioni 16.2. Ongezeko hilo limetokana na: kupokelewa kwa fedha za mikopo kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, viwanja vya ndege, umeme na maji; na malimbikizo ya riba ya deni la nje, hususan nchi zisizo wanachama wa kundi la Paris Club ambazo Serikali inaendelea kujadiliana nazo. Aidha, matokeo ya tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika Desemba 2020 yanaonesha kuwa deni ni himilivu kwa muda mfupi, wa kati na mrefu.
SEHEMU YA PILI
TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MWAKA 2020/21 NA MAPENDEKEZO YA SERIKALI YA MPANGO WA MAENDELEO
WA TAIFA KWA MWAKA 2021/22
- TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2020/21
- Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2020/21, Serikali ilitenga jumla ya shilingi trilioni 12.8, sawa na asilimia 37 ya bajeti ya Serikali kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 10.0, sawa na asilimia 78.6, ni fedha za ndani na shilingi trilioni 2.7, sawa na asilimia 21.4, ni fedha za nje. Hadi Januari 2021, ridhaa ya matumizi ya fedha za kugharamia miradi ya maendeleo ilikuwa shilingi trilioni 4.7, ikijumuisha shilingi trilioni 3.4 fedha za ndani na shilingi trilioni 1.2 fedha za nje.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021, Serikali iliendelea kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2020/21, ambao pia ni mpango wa mwisho wa utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa 2016/17-2020/21 . Baadhi ya mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na:
(i) Reli: Serikali inaendelea na ujenzi wa reli ya kati ya kiwango cha Kimataifa (Standard Gauge Railway – SGR) ambapo ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (km 300) umefikia asilimia 90 na kipande cha Morogoro – Makutupora
3
(km 422) umefikia asilimia 52.2, kusainiwa kwa mkataba wa ujenzi wa kipande cha Mwanza – Isaka (km 341) utakaogharimu shilingi trilioni 3.07; na kuendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa vipande vya Makutupora – Tabora (km 294) na Tabora – Isaka (km 133). Jumla ya shilingi bilioni 596.8 zimetumika katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021. Aidha, ukarabati wa miundombinu ya reli ya kati kutoka Dar es Salaam – Isaka (km 970) umekamilika na huduma za usafirishaji wa abiria na mizigo katika reli ya Tanga hadi Arusha (km 439) zimerejeshwa baada ya ukarabati kukamilika;
(ii) Uboreshaji wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL): kupokelewa kwa ndege mpya mbili aina ya Bombadier Dash 8-Q400 na Boeing 787-8 Dreamliner; kukamilika kwa malipo ya awali ya ununuzi wa ndege tatu (3), ambapo ndege mbili (2) ni aina ya Airbus A220-300 na moja (1) ni Dash 8-Q400 De-Havilland na hivyo kuwezesha Serikali kuwa na ndege mpya 11 kutoka ndege moja (1) iliyokuwepo mwaka 2015 na kuifanya ATCL kuwa na jumla ya ndege 12 ambapo ndege tatu (3) zinatarajiwa kuwasili mwaka 2021/22. Katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021 jumla ya shilingi bilioni 31.6 zimetolewa;
(iii) Viwanja vya Ndege na Rada: kuendelea na ujenzi wa viwanja vya ndege vya Geita (asilimia 98), Songea (asilimia 95) na Mtwara (asilimia 53.2); kukamilika kwa maandalizi ya mradi wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato ambao utagharimu dola za Marekani milioni 330, sawa na shilingi bilioni 759; uzinduzi wa ujenzi na upanuzi wa viwanja vya ndege vya Shinyanga, Kigoma, Tabora na Sumbawanga (Rukwa) vinavyogharimu Euro milioni 50, sawa na shilingi bilioni 136.85. Jumla ya shilingi bilioni 5.0 zimetumika katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021;
(iv) Mradi wa Kufua Umeme wa Maji – Julius Nyerere MW 2,115: kuendelea na ujenzi wa tuta kuu la bwawa; kukamilika kwa handaki la kuchepushia maji; kuendelea na ujenzi wa mgodi wa kuzalisha umeme, ujenzi wa njia za kupeleka maji kwenye mitambo na ununuzi wa vifaa mbalimbali vya mradi. Shilingi bilioni 249.3 zimetumika katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021;
(v) Miradi ya Umeme: kukamilika kwa ujenzi na upanuzi wa vituo vya kupoza umeme pamoja na njia za kusafirisha umeme katika Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa KV 220 Bulyanhulu – Geita; kuendelea na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa KV 400 Singida – Arusha – Namanga ambapo utekelezaji umefikia asilimia 86; kukamilika kwa asilimia 73.3 ya mradi wa Kufua Umeme – Rusumo MW 80; kuendelea na mradi wa Kinyerezi I Extension MW 185 ambapo utekelezaji umefikia asilimia 84; kukamilika kwa usanifu wa miradi ya Kakono MW 87 na Malagarasi MW 45; kuendelea kuhuisha upembuzi yakinifu na usanifu wa miradi ya kufua umeme wa maji ya Ruhudji MW 358 na Rumakali MW 222; na kukamilika kwa upembuzi yakinifu na kuendelea na uthamini wa mali za wananchi watakaopisha mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 400 Rufiji – Chalinze – Dodoma na Chalinze – Kinyerezi. Hadi Januari 2020, jumla ya vijiji 10,018 kati ya vijiji 12,317 viliunganishiwa umeme, sawa na asilimia 81.3 ya vijiji vyote. Katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021 shilingi bilioni 323.7 zimetumika;
4
(vi) Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania): kukamilika kwa tathmini ya athari za mazingira; kuendelea na utoaji wa elimu kwa umma kwa maeneo ya pembezoni mwa eneo la mradi; kukamilika kwa majadiliano ya maeneo mawili (2) kati ya matatu (3) ya mikataba ikiwemo ya nchi hodhi na wawekezaji, mkataba wa ubia, mkataba wa bandari na mkataba wa pango la ardhi;
(vii) Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia – Lindi: kukamilika kwa ulipaji wa fidia kwa wananchi watakaopisha mradi; na kuendelea na majadiliano baina ya Serikali na kampuni za uwekezaji kuhusu mikataba hodhi ya utafutaji wa gesi na uendelezaji wa mradi. Hadi Desemba 2020, shilingi bilioni 6.0 zimetumika katika maandalizi ya mradi, ikijumuisha kulipa fidia kwa wananchi watakaopisha mradi;
(viii) Ujenzi wa Barabara na Madaraja Makubwa: kujengwa kwa mtandao wa barabara kwa kiwango cha lami wenye urefu wa kilomita 3,537 (barabara kuu na za mikoa kilomita 2,208.6 na barabara za halmashauri kilomita 1,328) na hivyo kufanya mtandao wa barabara uliojengwa kwa kiwango cha lami hadi mwaka 2020/21 kufikia kilomita 13,044 ambapo kilomita 10,939 ni barabara kuu na kilomita 2,105 ni barabara za mikoa. Miradi iliyotekelezwa ni pamoja na: kuzinduliwa na kuanza kutumika kwa barabara ya juu (Interchange) ya Kijazi; kuendelea na ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi (Mwanza) lenye urefu wa kilomita 3.2 na upana wa mita 28.45 ambapo utekelezaji umefikia asilimia 14.5; na daraja la Tanzanite lenye km 1.03 (Dar es Salaam) na barabara unganishi zenye jumla ya urefu wa km 5.2 ambapo ujenzi umefikia asilimia 62. Shilingi bilioni 623.2 zimetumika katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021;
(ix) Uendelezaji wa Bandari: katika Bandari ya Dar es Salaam shughuli zilizofanyika ni pamoja na kuboreshwa kwa gati namba 1 – 4; kukamilika kwa ujenzi wa gati la kupakia na kushushia magari (RoRo); na kuendelea na uboreshaji wa gati na 5 hadi 7. Shilingi bilioni 42.6 zimetumika katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021. Aidha, katika Bandari ya Mtwara, ujenzi wa gati jipya lenye urefu wa mita 300 na yadi ya kuhudumia makasha umekamilika. Katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021 shilingi bilioni 45.0 zimetumika.
Vile vile, katika Bandari ya Tanga kina cha lango la kuingia meli kimeongezwa kutoka mita nne (4) hadi mita 13 na ujenzi wa gati mbili (2) kwenye kina kirefu umekamilika. Katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021 shilingi bilioni 20.4 zimetumika;
(x) Kuboresha Usafiri wa Abiria na Mizigo katika Maziwa Makuu: Kukamilika kwa ukarabati wa meli mbili (2) za New Butiama Hapa Kazi Tu na New Victoria Hapa Kazi Tu; kuendelea na ujenzi wa meli mpya ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo; kukamilika kwa ujenzi wa Chelezo cha kujengea na kukarabati meli katika Bandari ya Mwanza
chenye uwezo wa kubeba meli yenye uzito wa kuanzia tani 1 hadi 4,000, kikiwa na reli na mfumo unaowezesha kupandisha meli zaidi ya moja kulingana na ukubwa; kukamilika kwa ujenzi wa matishari mawili (2) yenye uwezo wa kubeba tani 1,000 kila moja; na ujenzi wa meli moja mpya ya MV Mbeya II yenye uwezo
5
wa kubeba abiria 200 na mizigo tani 200 umekamilika na kuanza kufanya kazi. Shilingi bilioni 20.2 zimetumika katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021;
(xi) Uendelezaji wa Viwanda: Baadhi ya viwanda vilivyojengwa ni: Kilimanjaro International Leather Industries Co Ltd (awamu ya kwanza) katika mkoa wa Kilimanjaro; Taifa Leather Company Ltd, Murzar Wilmar Rice Mills Ltd na Mahashree Agro-processing Tanzania Ltd vilivyopo Morogoro; majengo ya viwanda (Industrial Sheds) kwa ajili ya wajasiriamali katika mikoa ya Kagera, Kigoma, Geita, Mtwara na Ruvuma; kiwanda cha chai cha Kabambe (Njombe); kiwanda cha Yalin Cashewnut Company Ltd kinachobangua korosho (Mikindani –
Mtwara); na jengo la kiwanda kipya cha kuunganisha matrekta TAMCO – Kibaha. Katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021 shilingi bilioni 6.0 zimetumika;
(xii) Kilimo: Kuendelea kujenga na kuboresha miundombinu ya umwagiliaji ambayo imeongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 461,376 mwaka 2015 hadi hekta 694,715 mwaka 2020; kuongezeka kwa uzalishaji wa mbegu bora kutoka tani 36,614 mwaka 2015 hadi tani 76,726 mwaka 2020; kuongezeka kwa upatikanaji wa mbolea kutoka tani 302,450 mwaka 2015 hadi tani 727,719 mwaka 2020; kusambazwa kwa tani 40,592.6 za salfa na lita 1,314,465 za viuatilifu maji kwa wakulima wa korosho; na kuendeshwa kwa minada nane (8) ya kahawa katika mikoa ya Kilimanjaro (2), Songwe (4) na Ruvuma (2). Shilingi bilioni 29.5 zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21;
(xiii) Mifugo: kukarabatiwa kwa minada ya mifugo ya upili ambapo utekelezaji umefikia asilimia 95 katika mnada wa Ipuli – Tabora, Igunga – Tabora (asilimia 90) na Nata – Tabora (asilimia 70); kuimarishwa kwa kituo cha Taifa cha Uhimilishaji (National Artificial Insemination Centre – NAIC) kilichopo USA River, Arusha kwa kununua madume nane (8) ya mbegu; kuzalishwa na kusambazwa kwa mitamba 2,224 katika Mashamba ya Serikali; kuzalishwa na kusambazwa kwa dozi 84,801,750 za chanjo za mifugo katika halmashauri 184; kuendelea na ujenzi wa jengo la kuzalisha chanjo za bakteria katika Kituo cha Kuzalisha Chanjo cha Kibaha (Tanzania Vacccine Institute – TVI) ambapo ujenzi umefikia asilimia 87. Katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021 shilingi bilioni 2.3 zimetumika;
(xiv) Uvuvi: kukamilika kwa upembuzi yakinifu wa awali (pre – feasibility study) kwa ajili ya ujenzi wa bandari ya uvuvi; kuimarishwa kwa mialo sita (6) ya kupokelea samaki katika Ukanda wa Ziwa Victoria, minne (4) Ukanda wa Ziwa Tanganyika; na mitatu (3) katika Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi; kuendelea na ukarabati wa kituo cha ukuzaji viumbe maji cha Kingolwira – Morogoro; kuanzishwa kwa vituo vya ubora na uthibiti wa mazao ya uvuvi Singida, Kisesya na Murusagamba; kusambazwa kwa matenki 22 ya kukuzia vifaranga vya samaki; na kukarabatiwa kwa mabwawa nane (8) katika vituo vinne (4) vya kuendeleza ukuzaji viumbe maji vya Kingolwira – Morogoro, Mwamapuli – Tabora, Ruhila – Ruvuma na Nyengedi – Lindi. Katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021 shilingi bilioni 1.0 zimetumika;
(xv) Madini: kupitia na kutunga Sheria, Sera na mikataba ya madini; kuanzishwa kwa Kampuni mpya ya Twiga Minerals Corporation inayomilikiwa kwa ubia kati ya
6
Tanzania (hisa asilimia 16) na Kampuni ya Barrick (hisa asilimia 84) ambapo imetoa gawio la shilingi bilioni 100; kuanzishwa kwa kampuni ya Tembo Nickel Corporation ambayo ni ubia kati ya Serikali ya Tanzania (hisa asilimia 16) na kampuni ya LZ Nickel Mining Ltd (hisa asilimia 84) kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya nickel Kabanga; kujengwa kwa masoko 39 ya madini na vituo 41 vya kuuzia madini; kukamilika kwa ujenzi wa vituo vinne (4) vya umahiri katika maeneo ya Bariadi, Musoma, Bukoba na Handeni na kuendelea na ujenzi wa vituo vya Songea, Mpanda na Chunya. Aidha, ukusanyaji wa maduhuli katika sekta ya madini umeongezeka hadi shilingi bilioni 360.7, sawa na asilimia 117.4 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 307.3 katika kipindi Julai 2020 hadi Januari 2021. Shilingi bilioni 3.3 zimetumika katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021;
(xvi) Miradi ya Afya: kuendelea kutoa huduma za kupandikiza uloto; kukamilika kwa ujenzi wa jengo la huduma za dharura na ukarabati wa jengo la X-ray katika Hospitali ya Rufaa Dodoma; kukamilika kwa asilimia 98.2 ya ujenzi wa Hospitali ya Uhuru – Dodoma; ununuzi wa mashine ya Positron Emmission Tomography (PET Scan) kwa ajili ya Hospitali ya Ocean Road; kujenga na kuboresha miundombinu ya hospitali za rufaa za Mara, Geita, Songwe, Katavi, Sekou Toure (Mwanza), na hospitali za rufaa za kanda ya kusini Mtwara na kanda ya nyanda za juu kusini Mbeya na Hospitali ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) na Hospitali ya Kanda ya Ziwa ya Burigi (Geita). Aidha, mafanikio mengine ni: kuongezeka kwa idadi ya zahanati kutoka 4,922 mwaka 2015 hadi 6,120 mwaka 2020; vituo vya afya kutoka 535 mwaka 2015 hadi vituo 710 mwaka 2020; na Hospitali za Halmashauri za Wilaya kutoka 77 mwaka 2015 hadi 179 mwaka 2020. Shilingi bilioni 69.4 zimetumika katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021;
(xvii) Miradi ya Maji Mijini na Vijijini: katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021, Serikali imekamilisha miradi 422 ya maji mijini na vijijini, ambapo miradi 355 ni ya vijijini na 67 ni ya mijini. Aidha, miradi 924 ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji. Shilingi bilioni 241.3 zimetumika katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021;
(xviii) Elimu: kujengwa kwa miundombinu muhimu katika shule 3,904 (Msingi 3,021 na Sekondari 883), mabweni 547, nyumba za walimu 101, majengo ya utawala 25 na maktaba 43; kukamilika kwa ujenzi wa maboma 2,815 katika shule za msingi 2,133; kuendelea kugharamia elimumsingi bila ada; kukarabatiwa shule kongwe 86 kati ya 89, sawa na asilimia 97 ya lengo; na kuboreshwa kwa miundombinu ya vyuo 54 vya Maendeleo ya Wananchi. Shilingi bilioni 178.0 zimetumika katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021;
(xix) Mawasiliano na Teknolojia ya Habari: kukamilika kwa mradi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano awamu ya tatu ambayo inajumuisha ujenzi wa Kituo cha Taifa cha Data cha Dar es Salaam na uunganishwaji wa Zanzibar kwenye Mkongo wa Taifa; kuendelea na utekelezaji wa Mradi wa Mfumo wa Anuani za Makazi na Postikodi ambapo uwekaji wa miundombinu ya Mfumo umefanyika katika kata 110 za mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na wadi 8 za Zanzibar; na kuanza kwa Programu ya kuendeleza wajasiriamali wadogo wanaotengeneza bidhaa za
7
TEHAMA nchini. Katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021 shilingi bilioni 2.2 zimetumika;
(xx) Maliasili na Utalii: kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Burigi ambapo jumla watalii 1,171 walitembelea hifadhi hii kati yao 996 ni wa ndani na 175 ni wa nje ambapo jumla ya shilingi milioni 492.7 zimekusanywa kuanzia Novemba, mwaka 2019 hadi Desemba, 2020; kuanzishwa kwa Hifadhi ya Taifa ya Nyerere ambapo jumla ya watalii 9,938 (6,189 wa nje na 3,749 wa ndani) walitembelea hifadhi hiyo tangu mwezi Novemba, 2019 hadi Desemba, 2020 ambapo jumla ya shilingi bilioni 1.6 zimekusanywa; kutangazwa kwa vivutio vya utalii katika nchi mbalimbali duniani; kulinda rasilimali za misitu na kutunza mazingira ambapo jumla ya Tani 4.9 za aina mbalimbali za mbegu bora za miti na miche ya miti milioni 24 zimezalishwa; na kuongeza rasilimali za mazao ya misitu na uoto wa asili ambapo jumla ya hekta 1,876.5 zimepandwa miti. Aidha katika hatua za kufanya maboresho ya mandhari ya Jiji la Dodoma, jumla ya miche 21,678 ilipandwa katika maeneo mbalimbali ya Jiji. Shilingi bilioni 183.4 zimetumika katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021;
(xxi) Ajira: katika kipindi cha kuanzia Julai, 2020 hadi Januari, 2021 jumla ya ajira 450,416 zimezalishwa katika sekta mbalimbali. Kati ya ajira hizo, ajira 169,475 zimetokana na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya Serikali na ajira 280,941 zimezalishwa katika sekta binafsi. Aidha, ajira 16,067 zimezalishwa katika sekta ya umma, ikijumuisha ajira 13,529 za walimu, 1,000 za madaktari na 1,538 katika taasisi mbalimbali za Serikali; na
(xxii) Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi: kuandaliwa kwa taarifa za mipango ya matumizi ya ardhi kwa vijiji 59; kuandaliwa kwa Hati za Hakimiliki za Kimila 20,841 katika wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi; kukamilika kwa ujenzi wa ofisi za ardhi za halmashauri za wilaya za Kilombero na Ulanga; kupimwa kwa viwanja 95,329 kwenye maeneo ya mradi katika mikoa 19; kurasimisha jumla ya makazi 1,496,357 katika halmashauri mbalimbali nchini; kuboreshwa kwa Mfumo Unganishi wa Taarifa za Ardhi; na kununuliwa kwa vifaa vya kisasa vya upimaji. Shilingi bilioni 5.1 zimetumika katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021.
- MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2021/22
- Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22 ni wa kwanza katika utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano 2021/22 – 2025/26 wenye dhima ya “Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya Watu”. Uandaaji wa Mapendekezo ya Serikali ya Mpango umezingatia: Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Ilani ya CCM kwa Ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020; Hotuba za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli wakati akizindua Bunge la 11 na 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Sera na Mikakati mbalimbali ya kisekta, kikanda na kimataifa zikiwemo Dira ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) 2050; Dira ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) 2050; Ajenda 2063 ya Maendeleo ya Afrika; na Malengo ya Maendeleo Endelevu 2030.
8
- Mheshimiwa Mwenyekiti, vipaumbele vitakavyozingatiwa katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22 ni pamoja na:
(i) Miradi ya Kielelezo: Mradi wa Kufua Umeme wa Maji – Julius Nyerere MW 2,115; Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL); Ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha kimataifa (Standard Gauge); Makaa ya Mawe – Mchuchuma na Chuma – Liganga ikijumuisha ujenzi wa reli ya kiwango cha Kimataifa (Standard Gauge Railway – SGR) kutoka Mtwara hadi Mbambabay na matawi ya Mchuchuma na Liganga; Bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania); Mradi wa Kuchakata Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG) – Lindi; Mradi wa Kufua Umeme wa Maji – Ruhudji MW 358; Mradi wa Kufua Umeme wa Maji – Rumakali MW 222; Uchimbaji wa madini ya Nickel; Ujenzi wa Madaraja Makubwa na Barabara za Juu za Daraja la Kigongo – Busisi (Mwanza), Tanzanite (Dar es Salaam) na Interchange ya Kamata (Dar es Salaam); Bandari ya Uvuvi (Mbegani) na Ununuzi wa Meli za Uvuvi; Kiwanda cha Sukari Mkulazi; Utafutaji wa mafuta katika vitalu vya Eyasi Wembere na Mnazi Bay North; Mradi wa Magadi Soda – Engaruka; Kuongeza Rasilimali Watu yenye Ujuzi Adimu na Maalum (Ujuzi wa Kati na Wabobezi) kwa Maendeleo ya Viwanda na Ustawi wa Jamii; Kanda Maalum za Kiuchumi;
(ii) Kuchochea Uchumi Shindani na Shirikishi: ukarabati wa njia kuu ya reli ya kati; ununuzi wa injini na mabehewa; ujenzi wa barabara za kufungua fursa za kiuchumi, kuunganisha nchi jirani, kuondoa msongamano mijini na kuboresha barabara za vijijini; ujenzi wa madaraja makubwa ikiwemo madaraja ya New Wami (Pwani), Kitengule (Kagera), Kirumi (Mara) na Mkenda (Ruvuma); ujenzi na ukarabati wa meli kwenye maziwa makuu ikijumuisha MV Mwanza Hapa Kazi Tu, MV Liemba na MV Umoja; uboreshaji wa bandari za Dar es Salaam, Tanga, Mtwara na bandari za maziwa makuu; miradi ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme mijini na vijijini; mapinduzi ya TEHAMA ikijumuisha mradi wa mkongo wa Taifa wa mawasiliano na kutekeleza mradi wa Tanzania ya Kidigitali;
(iii) Kuimarisha Uwezo wa Uzalishaji Viwandani na Utoaji Huduma: Kuendeleza viwanda vinavyolenga kuongeza uzalishaji na thamani ya mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na madini pamoja na kuzalisha bidhaa zitakazotumia malighafi na rasilimali zinazopatikana nchini. Miradi hiyo ni pamoja na: miradi ya kuongeza tija kwenye kilimo ikiwemo tafiti za mbegu bora, miundombinu ya umwagiliaji, masoko ya bidhaa za kilimo, huduma za ugani, zana za kilimo, tiba na udhibiti wa magonjwa ya mifugo; viwanda vya kuongeza thamani ya madini ikiwemo kiwanda cha kuchenjua dhahabu – Mwanza; na kufufua Shirika la Uvuvi (TAFICO). Aidha, eneo hili linajumuisha pia miradi na programu inayolenga kuboresha sekta ya utalii, huduma za fedha na bima;
(iv) Kukuza Biashara na Uwekezaji: Eneo hili linajumuisha miradi ya kuboresha mazingira ya kufanya biashara na uwekezaji ikiwemo kuendelea kutekeleza Mpango wa Kuboresha Biashara na Uwekezaji (Blueprint) kwa: kutekeleza miradi ya kuimarisha mifumo ya kitaasisi ili kuchochea biashara na uwekezaji; kuanzisha vituo vya kutoa huduma pamoja kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa; kurekebisha sheria na kanuni zinazokinzana; na kuboresha na kuunganisha
9
mifumo ya TEHAMA katika mamlaka za udhibiti. Kwa upande wa uboreshaji wa masoko, miradi itakayotekelezwa inajumuisha: uendelezaji wa masoko ya bidhaa; kuboresha mifumo ya taarifa za Soko la ajira ili kuwezesha ukusanyaji, uchambuzi na utoaji wa taarifa; na kuimarisha udhibiti wa viwango vya ubora wa bidhaa;
(v) Kuchochea Maendeleo ya Watu: miradi itakayotekelezwa inajumuisha: kuimarisha miundombinu ya Hospitali ya Taifa Muhimbili; uboreshaji wa hosptitali za rufaa za kanda na za mikoa, halmashauri, vituo vya afya na zanahati; ununuzi na usambazaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi; kuimarisha huduma za tiba asili na tiba mbadala; kuendelea na udhibiti wa magonjwa yasiyoambukizwa; kuendelea na utoaji wa elimumsingi bila ada; kuendelea na utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu; kuendelea na uboreshaji wa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika ngazi zote za elimu ikijumuisha vyuo vya mafunzo ya ualimu; kuendelea kuboresha miundombinu na huduma za maji safi na maji taka mijini na vijijini; kuendelea na kupanga, kipima na kumilikisha ardhi mijini na vijijini; kusimamia na kuendeleza rasilimali za maji; na kuendelea na utekelezaji wa programu za kulinda mazingira na kuhimili mabadiliko ya tabianchi; na
(vi) Kuendeleza Rasilimali Watu: Eneo hili linajumuisha programu na mikakati inayolenga kuendeleza maarifa na ujuzi wa rasimali watu nchini. Miradi itakayotekelezwa ni pamoja na: kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia katika taasisi za mafunzo ya ufundi na vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi; kufanya mapitio ya mitaala inayotumika katika taasisi za mafunzo ya ufundi na vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi ili kukidhi mahitaji ya soko la ajira; kukuza ujuzi na uhawilishaji wa teknolojia; kuendeleza wabunifu ili kuongeza matumizi ya ubunifu katika mifumo rasmi ya uchumi na viwanda kwa maendeleo na ushindani wa kibiashara; kujenga uwezo wa vikundi na kampuni za ndani ili ziweze kufaidika na fursa za zabuni za ndani; na kutambua na kuainisha teknolojia mbalimbali.
SEHEMU YA TATU
TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI KATIKA KIPINDI CHA JULAI 2020 HADI JANUARI 2021 NA MAPENDEKEZO YA KIWANGO CHA UKOMO WA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2021/22
- TATHMINI YA UTEKELEZAJI WA BAJETI KATIKA KIPINDI CHA JULAI 2020 HADI JANUARI 2021
- Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2020/21, Serikali ilipanga kukusanya jumla ya shilingi trilioni 34.9 ikijumuisha: mapato ya ndani ya shilingi trilioni 24.1; misaada na mikopo nafuu shilingi trilioni 2.9; mikopo ya ndani shilingi trilioni 4.9; na mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara shilingi trilioni 3.0. Aidha, Serikali ilipanga kutumia shilingi trilioni 34.9 ambapo shilingi trilioni 22.1 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 12.8 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka 2020/21, yaliandaliwa kwa kuzingatia misingi (assumptions) pamoja na shabaha mahususi za uchumi ujumla. Mafanikio yaliyopatikana katika shabaha za uchumi jumla ni
10
kama ifuatavyo: Pato la Taifa lilikuwa kwa wastani wa asilimia 4.7 kati ya Januari hadi Septemba 2020, ikilinganishwa na lengo la mwaka la asilimia 5.5; mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 3.3. mwaka 2020 ikiwa ni ndani ya lengo la kutozidi asilimia 5; akiba ya fedha za kigeni ilitosheleza uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi 5.6 ikiwa ni zaidi ya lengo la miezi minne (4); na nakisi ya bajeti inatarajiwa kutozidi asilimia 3 ya Pato la Taifa kwa mwaka 2020/21.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021, Serikali ilikusanya jumla ya shilingi trilioni 17.1 kutoka vyanzo vyote vya ndani na nje, sawa na asilimia 87.7 ya makadirio ya shilingi trilioni 19.5. Mapato ya ndani yakijumuisha mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa yalifikia shilingi trilioni 12.0, sawa na asilimia 87.9 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 13.7. Kati ya mapato hayo: mapato yaliyokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) yalikuwa shilingi trilioni 10.4, sawa na asilimia 88.3 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 11.7; mapato yasiyo ya kodi kutoka Wizara, Idara zinazojitegemea, Wakala na Taasisi za Serikali yalikuwa shilingi trilioni 1.2, sawa na asilimia 83.2 ya lengo la kukusanya shilingi trilioni 1.5; na mapato ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa yalifikia shilingi bilioni 462.5, ikiwa ni asilimia 93.1 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 496.7. Aidha, Desemba 2020, Mamlaka ya Mapato iliweza kukusanya kiasi cha juu ambacho hakijawahi kufikiwa katika historia cha shilingi trilioni 2.1.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2020/21, Bunge liliidhinisha mapendekezo ya Serikali ya kuboresha sera za mapato kwa lengo la kupanua wigo wa kodi pamoja na kuendeleza na kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara. Marekebisho hayo ya mfumo wa kodi yalitarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa shilingi milioni 3,504.2. Katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2020, mapato halisi yaliyotokana na vyanzo hivyo vipya yalifika shilingi milioni 1,440.1, ikiwa ni ufanisi wa asilimia 82.2 ya lengo la kukusanya shilingi milioni 1,752.1 kwa kipindi hicho. Hatua nyingine zilizochukuliwa zililenga kuboresha mazingira ya Biashara na uwekezaji kwa kufuta ama kupunguza kodi na tozo mbalimbali, pamoja na kuwa hatua hizo zilipunguza mapato kwa ujumla wake.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha malengo ya ukusanyaji wa mapato yanafikiwa, Serikali itaendelea kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa sheria, kanuni na taratibu za kodi; Kuboresha mifumo ya TEHAMA ya kukusanya kodi na maduhuli, ikiwemo Electronic Fiscal Device Management System (EFDMS) ambao hupokea na kutunza kumbukumbu za utoaji wa risiti za mauzo. kuimarisha mifumo ya usimamizi na ufuatiliaji wa makusanyo ya mapato kwa kutoa elimu ya kodi na umuhimu wa kutoa na kudai risiti ili kuhamasisha ulipaji kodi wa hiari; kuimarisha ushirikiano miongoni mwa mamlaka zinazokusanya mapato ya Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama ili kudhibiti biashara za magendo; kukasimisha jukumu la kukusanya kodi ya majengo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa; kufanya mapitio ya mfumo wa mapato na matumizi ya Serikali ili kuwa na bajeti endelevu; na kukamilisha uanzishwaji wa ofisi ya msuluhishi wa masuala ya kikodi (Tax Ombudsman) ili kushughulikia malalamiko ya walipakodi nje ya Mahakama.
11
- Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inakamilisha utafiti kuhusu visababishi muhimu vya kiwango cha chini cha uhiari wa walipakodi kusajili biashara zao, ulipaji wa kodi kwa wakati na uwazi katika utoaji wa taarifa sahihi kuhusu biashara wanazofanya, hususan kwa wafanyabiashara wadogo. Utafiti huu unahusisha kuchunguza changamoto za kitaasisi, tabia sababishi na hatua zinazopaswa kuchukuliwa. Aidha, Mamlaka ya Mapato Tanzania inatekeleza mradi wa kujirejeshea kutoka kwa mawakala jukumu la kusimamia EFD ili kuongeza ufanisi katika usambazaji wa mashine za EFD pamoja na utoaji wa huduma za kiufundi pindi mashine hizo zinapopata hitilafu. Vile vile, Serikali inafanya mapitio ya mfumo wa mapato na matumizi kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa mapato yatakayokidhi ugharamiaji wa mahitaji ya Serikali na hivyo kuwa na bajeti endelevu.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, Washirika wa Maendeleo walitoa jumla ya shilingi trilioni 1.4 sawa na asilimia 82.4 ya makadirio ya shilingi trilioni 1.7. Kati ya kiasi kilichotolewa, mikopo nafuu ya kibajeti ilikuwa shilingi bilioni 150.9, miradi ya maendeleo ilikuwa shilingi trilioni 1.1 sawa na asilimia 75.1 ya makadirio kwa kipindi hicho na mifuko ya kisekta ilipokea shilingi bilioni 149.0 sawa na asilimia 62.9 ya makadirio.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021, Serikali ilipanga kukopa katika soko la ndani jumla ya shilingi trilioni 3.0. Katika kipindi hicho, shilingi trilioni 2.7 zilipatikana, sawa na asilimia 88.7 ya lengo. Kati ya kiasi kilichokopwa, shilingi trilioni 1.7 zimetumika kulipia mikopo ya ndani iliyoiva na shilingi bilioni 988.9 zimetumika kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo. Serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali kuhakikisha kuwa kiasi kilichopangwa kukopwa katika soko la ndani kinapatikana. Mikakati hiyo ni pamoja na kutoa elimu zaidi kwa wananchi na wadau wengine ili waweze kuwekeza katika hatifungani na dhamana za Serikali.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilipanga kukopa kiasi cha shilingi trilioni 3.0 kutoka vyanzo vyenye masharti ya kibiashara. Katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021, Serikali imefanikiwa kukopa kiasi cha shilingi trilioni 1.1 sawa na dola za Marekani milioni 463.8 kutoka Standard Chartered Bank (SCB) kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kimataifa. Aidha, Serikali inaendelea na majadiliano ili kukamilisha upatikanaji wa mkopo kutoka Benki ya Credit Suisse AG (Dola za Marekani milioni 200) kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa miundombinu mbalimbali. Vilevile, majadiliano na benki mbalimbali yanaendelea ili kukopa kiasi chote kilichopangwa kwenye bajeti ya mwaka 2020/21. Mikopo hii inachelewa kupatikana kutokana na majadiliano kuchukua muda mrefu hususan kutokana na masharti magumu ya mikopo hiyo.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa matumizi, ridhaa ya matumizi iliyotolewa katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021, ilikuwa shilingi trilioni 16.7, sawa na asilimia 86.7 ya lengo. Kati ya kiasi kilichotolewa, shilingi trilioni 12.1 ni fedha za matumizi ya kawaida, sawa na asilimia 93.7 ya lengo na shilingi trilioni 4.7 ni fedha za maendeleo, sawa na asilimia 74.1 ya lengo. Fedha za matumizi ya kawaida zilizotolewa zinajumuisha: shilingi trilioni 4.4 kwa ajili ya mishahara, sawa na asilimia 97.6 ya lengo; shilingi trilioni 4.5 kwa ajili ya kugharamia deni la Serikali, sawa na asilimia 89.4 ya
12
lengo; na shilingi trilioni 3.2 kwa ajili ya matumizi mengineyo, sawa na asilimia 96.3 ya lengo. Aidha, fedha za maendeleo zilizotolewa zinajumuisha shilingi trilioni 3.4 fedha za ndani na shilingi trilioni 1.2 fedha kutoka kwa Washirika wa Maendeleo. Vile vile, kiasi cha shilingi bilioni 402.2 ni fedha ambazo zimetengwa mahsusi kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa miradi mikubwa baada ya kukamilishwa kwa uhakiki wa hati za madai pamoja na hati mpya za madai zitakazowasilishwa.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika utekelezaji wa sera za matumizi katika kipindi cha Julai 2020 hadi Januari 2021 ni kuelekeza rasilimali fedha kwenye maeneo yaliyolindwa, yasiyoepukika pamoja na vipaumbele vinavyochochea ukuaji wa shughuli za kiuchumi. Maeneo hayo ni pamoja na: kulipa Deni la Serikali, ambapo jumla ya shilingi trilioni 4.5 zilitolewa; kulipa mishahara ya watumishi kwa wakati, ambapo shilingi trilioni 4.4 zilitolewa; kugharamia shughuli za uendeshaji wa Serikali, ambapo jumla ya shilingi trilioni 3.2 zilitolewa; kugharamia kwa mara ya kwanza Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kwa kutumia fedha za ndani, ambapo jumla ya shilingi bilioni 268.5 zilitumika; ulipaji wa madeni yaliyohakikiwa ya shilingi bilioni 340.0, ambapo kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 52.1 ni madai ya watumishi ya kimshahara na yasiyo ya kimshahara, shilingi bilioni 21.7 ni madai ya wazabuni, shilingi bilioni 201.3 makandarasi, shilingi bilioni 32.0 watoa huduma na shilingi bilioni 32.9 ni madai mengineyo; kugharamia mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, uimarishaji wa vyuo vya ufundi stadi (VETA) na kukuza ujuzi kwa vijana ambapo shilingi bilioni 248.5 zilitolewa; na kugharamia elimumsingi bila ada ambapo shilingi bilioni 145.6 zilitolewa. Aidha, Serikali imeendelea kusimamia nidhamu ya matumizi, kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima na kuongeza kasi ya matumizi ya TEHAMA katika usimamizi wa matumizi ya Serikali.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha Februari hadi Juni 2021, mapato ya ndani yanatarajiwa kufikia lengo la mwaka kwa kutekeleza mikakati mbalimbali ya kuimarisha usimamizi na kuhimiza matumizi ya mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato. Misaada na mikopo nafuu kutoka nje inatarajiwa kufikia lengo kwa kuimarisha ushirikiano na Washirika wa Maendeleo kwa kutekeleza Mpango Kazi wa Mwongozo wa Ushirikiano (Development Cooperation Framework – DCF); na Mikopo ya ndani na nje yenye masharti ya kibiashara inategemewa kufikia lengo la bajeti. Aidha, katika kipindi cha Februari hadi Juni 2021, Serikali itaendelea kupeleka fedha kwenye Mafungu kwa kuwianisha mapato na matumizi ikiwa ni pamoja na kutoa kipaumbele kwa mahitaji yasiyoepukika kama vile ugharamiaji wa deni la Serikali, ulipaji wa mishahara ya watumishi, uendeshaji wa ofisi na utekelezaji wa miradi muhimu yenye maslahi mapana kwa Taifa.
- MAPENDEKEZO YA KIWANGO CHA UKOMO WA BAJETI YA SERIKALI KWA MWAKA 2021/22
Sera za Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2021/22
- Mheshimiwa Mwenyekiti, sera za mapato na hatua za kiutawala kwa mwaka 2021/22 zitalenga: kutoa kipaumbele katika utekelezaji wa mikakati na miradi ya kuongeza mapato; kuimarisha usimamizi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa kuhimiza matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA; kuimarisha usimamizi wa sheria za
13
kodi ili kutatua changamoto za ukwepaji kodi na kupunguza upotevu wa mapato; kuboresha mazingira ya ulipaji kodi kwa hiari na upanuzi wa wigo wa kodi; kuendelea kutekeleza Mwongozo wa Ushirikiano wa Maendeleo Tanzania; na kuendelea kukopa kutoka katika vyanzo vyenye masharti nafuu, hususan kwa utaratibu wa Export Credit Agency (ECA).
- Mheshimiwa Mwenyekiti, Katika mwaka 2021/22, Serikali itaendelea kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma ili kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za umma na kuelekeza rasilimali fedha kwenye miradi ya kielelezo na kimkakati. Aidha, Serikali itaendelea kuhakiki, kulipa na kuzuia ongezeko la malimbikizo ya madai kwa Serikali. Hivyo, Sera za matumizi kwa mwaka 2021/22 zitajumuisha yafuatayo: kuelekeza fedha kwenye maeneo ya kipaumbele yatakayochochea ukuaji wa uchumi na kuhakikisha kuwa miradi inayoendelea inapewa kipaumbele kabla ya miradi mipya; kuhakikisha kuwa nakisi ya bajeti haizidi asilimia 3.0 ya Pato la Taifa; kudhibiti ulimbikizaji wa madai; kuendeleza nidhamu ya matumizi ya fedha za umma; na kuongeza matumizi ya TEHAMA katika shughuli za Serikali ili kuongeza ufanisi ikiwa ni pamoja na kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani kwenye eneo la usalama wa mifumo.
Kiwango cha Ukomo wa Bajeti kwa Mwaka 2021/22
- Mheshimiwa Mwenyekiti, uandaaji wa Kiwango cha Ukomo wa Bajeti ya Serikali katika kipindi cha mwaka 2021/22 umejengwa katika misingi (assumptions) ifuatayo:
(i) Kuendelea kuwepo kwa amani, usalama, umoja, utulivu wa ndani na nchi jirani;
(ii) Kuhimili athari za majanga ya asili;
(iii) Ushiriki mpana wa sekta binafsi;
(iv) Hali nzuri ya hewa itakayowezesha uzalishaji wa chakula cha ziada; na (v) Kuimarika kwa uchumi wa dunia na utulivu wa bei katika masoko ya kimataifa.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, malengo na shabha za uchumi jumla ni kama ifuatavyo:
(i) Ukuaji wa Pato Halisi la Taifa kufikia asilimia 6.0 mwaka 2021 na asilimia 6.3 ifikapo mwaka 2023;
(ii) Kuhakikisha kuwa mfumuko wa bei unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja ya wastani wa asilimia kati ya 3.0 – 5.0 katika muda wa kati;
(iii) Mapato ya ndani kufikia asilimia 15.9 ya Pato la Taifa mwaka 2021/22 na asilimia 16.3 ya Pato la Taifa mwaka 2023/24;
(iv) Mapato ya kodi kufikia asilimia 13.5 ya Pato la Taifa mwaka 2021/22 kutoka matarajio ya asilimia 12.9 mwaka 2020/21;
(v) Kuhakikisha nakisi ya bajeti haizidi asilimia 3.0; na
(vi) Kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne (4).
14
- Mheshimiwa Mwenyekiti, shabaha za uchumi jumla zimeandaliwa kwa kuzingatia hali halisi ya uchumi wa Tanzania na ulinganisho wa chumi nyingine duniani, hususan kusini mwa Jangwa la Sahara. Wastani wa mapato ya ndani kwa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara ni asilimia 14.5 ya Pato la Taifa, nakisi ya bajeti ni wastani wa asilimia 7.6 na wastani wa mfumuko wa bei ni asilimia 10.5.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, vigezo vilivyotumika katika uandaaji wa kiwango cha ukomo wa bajeti za matumizi za Mafungu ni pamoja na: miradi inayoendelea; matumizi yaliyolindwa; vibali vya miradi mipya; miradi yenye vyanzo maalumu; vibali vya ajira mpya na upandishwaji wa madaraja kwa watumishi; matumizi yasiyojirudia; na mahitaji ya Mamlaka za Uhifadhi zilizoathiriwa na kushuka kwa biashara katika sekta ya utalii.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kuwa, yapo mafungu yenye vyanzo maalum yenye mahitaji makubwa ikilinganishwa na uwezo wa kibajeti kwa sasa kama vile barabara na maji vijijini (TARURA NA RUWASA). Ili kukabiliana na upungufu uliopo, Serikali inafanya tathmini ya utendaji wa taasisi zinazosimamia maeneo hayo ili kuongeza tija na kuangalia uwezekano wa kuwa na bajeti endelevu ya maeneo hayo. Aidha, Serikali ipo katika majadiliano na Benki ya Dunia ili kuwezesha upatikanaji wa mkopo nafuu wa dola za Marekani milioni 300 kwa ajili ya kugharamia ujenzi na matengenezo ya miradi ya barabara za TANROADS na TARURA.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia sera, misingi na vigezo vya ukomo, jumla ya shilingi trilioni 36.3 zinatarajiwa kukusanywa kwa mwaka 2021/22, ikiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 4.0 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka 2020/21. Kati ya mapato hayo: mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 26.0, sawa na asilimia 71.8 ya bajeti yote; misaada na mikopo nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo shilingi trilioni 2.9; mikopo ya ndani shilingi trilioni 5.0; na mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara shilingi trilioni 2.4.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2020/21, Serikali inapanga kutumia jumla ya shilingi trilioni 36.3 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo. Kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 23.0 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ikiwa ni asilimia 63 ya bajeti yote na shilingi trilioni 13.3 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo, sawa na asilimia 37 ya bajeti yote. Bajeti ya maendeleo inajumuisha shilingi trilioni 10.4 fedha za ndani, sawa na asilimia 78.2 ya bajeti ya maendeleo na shilingi trilioni 2.9 fedha za nje, sawa na asilimia 21.8 ya bajeti ya maendeleo. Aidha, shilingi, trilioni 10.7 sawa na asilimia 29.5 ya Bajeti yote zimetengwa kwa ajili ya kulipa fedha zilizokopwa kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo imekamilika na inayoendelea. Fedha hizo zilitengwa kwenye kasma za Matumizi ya Kawaida lakini kimsingi sio za kulipa mishahara wala posho.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia maelezo hayo, kiwango cha ukomo wa bajeti kwa mwaka 2021/22 ni kama ilivyo katika Jedwali lifuatalo:
15
Mapendekezo ya Kiwango cha Ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/22
Shilingi Milioni
Mapato 2021/22 A. Mapato ya Ndani-Serikali Kuu 25,168,718 (i) Mapato ya Kodi (TRA) 22,097,676 (ii) Mapato yasiyo ya kodi 3,071,042 B. Mapato ya Halmashauri 863,858 C. Misaada na Mikopo nafuu kutoka Washirika wa Maendeleo 2,884,990 (i) Misaada na Mikopo nafuu – GBS * 0 (ii)Misaada na Mikopo nafuu ya Miradi 2,602,684 (iii)Misaada na Mikopo nafuu ya Kisekta 282,306 D. Mikopo ya Ndani na Nje 7,341,240 (i) Mikopo ya Nje 2,352,107 (ii) Mikopo ya Ndani 1,838,796 (iii)Mikopo ya Ndani- Rollover 3,150,337 JUMLA YA MAPATO YOTE (A+B+C+D) 36,258,806
Matumizi
- Matumizi ya Kawaida 23,002,951
o/w (i) Mfuko Mkuu wa Serikali 10,663,278 -Malipo ya Riba Ndani 1,561,637 -Malipo ya Mtaji Ndani (Rollover) 3,150,337 -Malipo ya Mtaji Nje 3,015,070 – Malipo ya Riba Nje 1,151,376 – Michango ya Serikali kwenye Mifuko ya Hifadhi za Jamii 1,247,149 -Matumizi Mengine ya Mfuko Mkuu 537,710 (ii) Mishahara 8,150,509 (iii)Matumizi Mengineyo (OC) 3,944,164 – Malipo ya Madeni yaliyohakikiwa 200,000 – Matumizi ya Halmashauri (own source) 532,768 – Matumizi mengineyo 3,211,396 (iv) Mahitaji ya TANAPA, NCAA na TAWA 0 245,000
- Matumizi ya Maendeleo 13,255,855 (i) Fedha za Ndani 10,370,865 o/w Malipo ya Madeni yaliyohakikiwa 400,000 o/w Ugharamiaji wa SGR 1,174,246 o/w Ugharamiaji wa Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere 1,440,000 o/w Matumizi ya Halmashauri 331,090 o/w Miradi mingine 7,025,529 (ii) Fedha za Nje 2,884,990 JUMLA YA MATUMIZI YOTE (E+F) 36,258,806 NAKISI YA BAJETI (ASILIMIA YA PATO LA TAIFA) 1.8% Chanzo: Wizara ya Fedha na Mipango
16
HITIMISHO
- Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutekeleza hatua mbalimbali za kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kupunguza utegemezi, kugharamia mahitaji yasiyoepukika kama vile ugharamiaji wa miradi ya kipaumbele na kimkakati, deni la Serikali, mishahara ya watumishi, mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, elimumsingi bila ada na uendeshaji wa ofisi. Aidha, Serikali itaendelea kusimamia nidhamu ya matumizi ya fedha za umma kwa kuzingatia Sheria ya Bajeti, SURA 439, Sheria ya Fedha za Umma, SURA 348, Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, SURA 290 na Sheria ya Ununuzi wa Umma, SURA 410. Lengo ni kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuziba mianya ya uvujaji wa fedha za umma. Vile vile, Serikali itaendelea kuhakiki, kulipa na kuzuia ongezeko la malimbikizo ya madai kwa Serikali.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22 pamoja na Bajeti ya mwaka 2021/22, unatarajiwa kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi, upatikanaji wa huduma za kijamii, kuongeza fursa za ajira na maendeleo ya watu na nchi kwa ujumla.
- Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
17
Post a Comment